Loading...
Monday

TWPG yatoa tamko Bungeni kuhusu kudhalilishwa wabunge wanawakeMwenyekiti wa Chama cha wabunge wanawake Tanzania (TWPG), Magreth Sitta, amelaani vikali vitendo vya kutolewa kwa lugha za matusi na udhalilishaji dhidi ya wabunge wanawake bungeni na kusema hakiwezi kumvumilia mbunge yeyote atakayetoa lugha hizo.

Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa chama hicho leo bungeni baada ya kipindi cha maswali na majibu Bi.Magret ametoa maelezo binafsi kuhusu kitendo kilichotokea Mei 5 mwaka huu, ambapo Mbunge wa Ulanga Mashariki, Goodluck Mlinga alitoa lugha ya kudhalilisha dhidi ya wabunge wanawake wa upinzani kwa kusema kuwa waliingia katika bungeni baada ya kuitwa 'baby' wa mtu. 

Amesema kuwa chama hicho kimejikita katika kuhakikisha haki za wanawake ndani na nje ya Bunge zinafuatwa, ikiwa ni pamoja na kupinga ukatili na udhalilishaji dhidi yao.

Pia amesema katika kutetea na kuangalia haki za wanawake, hakuangaliwi tofauti za kiitikadi za kisiasa bali kinachoangaliwa ni haki za wanawake wote kwa ujumla wao.

"Chama chetu kinatazama umoja wetu wanawake wote humu bungeni na nje ya Bunge, na kupinga udhalilishaji unaoelekezwa kwa wanawake," anasema.

"Kutokana na malengo ya chama chetu tumeona tutoke tamko hili, kwa kuwa kuna wabunge walitoa maneno ya kudhalilisha utu na hadhi ya mwanamke..tunalaami vikali na hatukubaliani na vitendo vya hivi kwa wabunge wanawake iwe humu ndani ya Bunge na hata nje ya bunge"anasisitiza Magreth.

Hata hivyo chama hicho kilikitaka kiti cha Spika kuchukua hatua ya haraka ya kinidhamu dhidi ya mbunge atakayerudia kutoa lugha za namna hiyo dhidi ya wabunge wanawake.

Aidha chama hicho pia kilitoa wito kwa wabunge wote kujiheshimu na kuwaheshimu wabunge wengine ili kuendelea kulinda hadhi na heshima ya Bunge hilo.

"Wabunge tunapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika jamii yetu. Tunaamini kuwa hili litakuwa tukio la mwisho. Tunapaswa kuheshimiana bila kujali tofauti ya kijinsia pamoja na tofauti za kiitikadi za vyama. Pia wabunge wanawake tunapaswa kuendelea kuwa pamoja na tusikubali kugawanywa kutokana na maneno mbalimbali yanayoelekezwa kwetu.'

0 comments :

Post a Comment

 
Toggle Footer
TOP