Loading...
Friday

[update] Wanafunzi wamkataa mwalimu wakimtuhumu kulawiti wanafunzi wa kiume

Mei 29, 2016 -- MAKAMU Mkuu wa Shule ya Sekondari Usevya katika Halmashauri ya Mpimbwe wilayani Mlele , Makonda Ng’oka “Membele” (34) amefikishwa katika Mahakama ya mkoa wa Katavi kwa tuhuma za kumlawiti mwanafunzi wake.

Mshtakiwa huyo alifikishwa juzi mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Chiganga Tengwa ambapo alikana shitaka lake na yupo nje baada ya kutimiza masharti ya dhamana yaliyomtaka kulipa kiasi cha Sh 3,000,000 mahakamani.

Mwendesha Mashtaka, Wakili wa Serikali, Gregory Mhangwa alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo katika shule ya sekondari Usevya kati ya Novemba 2015 na Aprili 2016.

Alieleza mahakamani hapo kwamba katika kipindi hicho mshtakiwa alimuingilia mwanafunzi wake huyo kinyume cha maumbile. Hakimu Tengwa aliahirisha shauri hilo hadi Juni 26 , mwaka huu litakapotajwa tena.

Inadaiwa kuwa kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa Makamu Mkuu huyo wa shule hiyo kunafuatia wanafunzi wa kiume wanaosoma Kidato cha Tano katika shule hiyo kumkataa na kutishia kuandamana kupinga vitendo vyake vya kuwalawiti wanafunzi wake.

Kufuatia msimamo wa wanafunzi hao iliwalazimu Ofisa Elimu mkoa wa Katavi, Everest Hunji na Mkurugenzi Mtendaji Halmashari ya Mpimbwe wilayani Mlele, Evaristo Kiwale kufika shuleni hapo Jumatatu jioni na kuzungumza na wanafunzi hao.

Wanafunzi hao walidai kuwa mwalimu huyo amekuwa akiwalawiti baadhi yao ikiwa ni adhabu mbadala wanapobainika kufanya makosa shuleni hapo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mpimbwe, Kiwale alisema vitendo vya ushoga havikubaliki na kwamba tayari hatua stahiki zimeshachukuliwa za kumpeleka katika vyombo vya kisheria.

“Msitaharuki mnapomuona mwalimu huyo mitaani msidhani hajachukuliwa hatua yoyote ile,” alisisitiza.

******************************

Mei 20, 2016 -- Katika hali isiyo ya kawaida wanafunzi wa kiume wanaosoma kidato cha tano katika shule ya Sekondari Usevya, Halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele, Mkoani Katavi wamemkataa Mwalimu wao (jina tunalo) wakimtuhumu kuwafanyia vitendo vya ulawiti.
Wakizungumza kwa masikitiko na waandishi wa habari shuleni juzi jioni mbele ya Afsa Elimu Mkoa wa Katavi, Everest Hunji, baadhi ya manafunzi ambao ni mwenyekiti wa serikali ya wainafunzi wa Sekondari ya Usevya Moshi Ramadhani na Katibu Joniour Mgallah, walisema vitendo anavyofanya mwalimu huyo vimewaathiri kisaikolojia na kudhorotesha ufaulu wao kimasomo.
''Kwa kweli sisi wanafunzi tunakiri mwalimu ambae jina lake tunalo amekuwa akitumia Madaraka yake ya umakamo mkuu wa shule vibaya,Hususani anapokukamata na kosa hapa shuleni badala ya kukupa adhabu ya kulingana na kosa ulilofanya anakuomba kujamiiana naye huku akijua kuwa anayetaka kufanya naye mambo hayo ni mwanaume na utakapokataa anatishia kukufukuza shule,'' walisema.
Wanafunzi hao waliendelea kufafanua kuwa mwalimu huyo tayari ameshatekeleza vitendo hivyo vya ulawiti kwa baadhi ya wanafunzi na kuongeza kuwa wapo tayari kutoa ushahidi mahakamani kama kutahitajika kufanya hivyo.

Sambamba na hayo, walisema kuwa mwalimu huyo amekuwa akiwatumikisha wanafunzi katika shughuli zake binafsi za uzalishaji kwa kuwapeleka kufanya kazi kwenye mashamba yake.

Naye Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Mpimbwe, Erasto Kiwale ambaye aliambatana na Afisa Elimu Mkoa wa Katavi, Everest Hunji alisema Kitendo hicho hakikubaliki na tayari hatua sitahiki zimeshachukuliwa za kumpeleka katika vyombo vya kisheria, hivyo wanapomwona mwalimu huyo mitaani wasidhani hajachukuliwa hatua.

Afisa Elimu Mkoa wa Katavi, Everest Hunji aliwataka wanafunzi kuwa watulivu na kuziacha mamlaka husika kulishughulikia suala hilo huku akiwaahidi kuwa malalamiko yao yatashughulikiwa ipasavyo.
  • Taarifa ya Walter Mguluchuma - Mlele.

1 comments :

 
Toggle Footer
TOP