Loading...
Wednesday

Watuhumiwa 4 wa ujambazi wauawa katika mapango ya Amboni

Watu wanne wameuawa katika mapambano na polisi yaliyotokea kwenye mapango ya Amboni mjini Tamga, eneo ambalo polisi mmoja aliuawa Februari mwaka jana katika tukio lililohusishwa na ugaidi.

Katika tukio hilo la Februari mwaka jana, polisi walilazimika kuomba msaada wa askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) kukabiliana na watu waliokuwa wamejificha kwenye mapango hayo na kupiga kambi hapo hadi walipokisambaratisha kikundi hicho kilichoelezwa kuwa na sura ya ugaidi.

Mapambano ya jana yametokea kwenye eneo hilo la kihistoria wakati polisi wakiendesha operesheni ya kusaka majambazi waliofanya mauaji katika duka la Central Bakery.

Majambazi hao walivamia duka maarufu la Central Bakery mwezi uliopita na kuwaua watu wanne, kujeruhi wawili na kupora Sh2.7 milioni baada ya kufanikiwa kuvunja kasiki.

Jana ilikuwa siku ya tatu tangu milio ya risasi ianze kusikika katika mapango ya Amboni na baadaye taarifa kuenea jijini Tanga kuwa kulikuwa na majibizano ya risasi.

Kamanda wa polisi wa mkoa, Leonard Paulo aliwataja waliouawa katika mashambulizi ya risasi yaliyotokea katika mapango ya Amboni kuwa ni Nasibu Bakari, Abuu Katada, Abuu Mussa na raia wa kigeni aliyetambulika kwa jina la Idrisa Berato.

Kamanda Leonard alisema mbali na kuwathibiti majambazi hao, pia jeshi hilo limefanikiwa kukamata vifaa mbalimbali vinavyosadikika kuwa vilikuwa vinatumika katika matukio ya ujambazi.

Alivitaja vifaa vilivyokamatwa kuwa ni vocha mbalimbali za simu 195, majambia saba, mapanga manne, msumeno mmoja, risasi 17 za shortgun, sare za mgambo, kofia inayofanana na ya sare za JWTZ na pikipiki mbili.

Alisema wakati wakiendelea na uchunguzi, watu wanne walikamatwa na waliwataja wenzao ambao walijificha kwenye mapango hayo na ndipo jeshi likavamia eneo hilo na kufanikiwa kuua watu wanne na kujeruhi mmoja.

Alisema Katika majibizano ya risasi, askari wawili walijeruhiwa, akiwataja kuwa ni Gwantwa Mwakisole, mkaguzi msaidizi wa polisi mkoani Tanga na PC Charles.

Habari zinaarifu kuwa viongozi waandamizi wa Jeshi la Polisi kutoka makao makuu wako jijini Tanga tangu kutokea kwa mauaji hayo.

------------------------------------

JESHI la Polisi mkoani Tanga limewaua watu wanne wanaodhaniwa kuwa ni majambazi.

Watu hao waliuawa jana katika eneo la mapango ya Amboni wakati wa majibizano ya risasi kati yao na polisi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Leonard Paul, alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo alipozungumza na waandishi wa habari.

“Pamoja na kufanikiwa kuwaua watu hao, pia tumefanikiwa kukamata vifaa mbalimbali vinavyosadikika vilikuwa vinatumiwa na wahalifu hao wakati wa kufanya matukio ya ujambazi,” alisema Kamanda Paul.

Alivitaja vitu vilivyokamatwa kuwa ni vocha 195 za mitandao ya simu mbalimbali, majambia saba, mapanga manne, msumeno mmoja, risasi 17 za shotgun, sare za mgambo, kofia inayofanana na sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na pikipiki mbili.

Aliwataja majambazi waliouawa kuwa ni Nassibu Bakari, Abuu Mussa, Abuu Kadati na Idrissa Berratu aliyedaiwa kuwa ni raia wa kigeni.

“Kabla ya kupambana na majambazi hao, tuliwakamata watu wanne waliotaja walipo majambazi wenzao waliokuwa wameweka kambi kwenye mapango ya Amboni.

“Kwa hiyo, tulichokifanya ni kuvamia mapango hayo na tukawaua watu hao wanne na kumjeruhi mmoja baada ya majibizano makali ya risasi.

“Kwa bahati mbaya zaidi, polisi wawili, walijeruhiwa ambao ni Gwantwa Mwakisole ambaye ni mkaguzi msaidizi na PC Charles.

“Kwa, hiyo namuomba sana Mungu awaponye haraka kwa sababu baada ya kuanza kupatiwa matibabu, hali zao zinaendelea vizuri,” alisema Kamanda Paul.

Mapango ya Amboni mkoani Tanga yamekuwa ni kimbilio la majambazi na wamekuwa wakiyatumia kama maficho yao wanapofanya uhlrifu.

Mwaka jana, majambazi hao ambao baadaye walidhaniwa kuwa ni kikundi cha wanamgambo wa Al Shabaab, walitikisa kwa uhalifu mkoani Tanga na kulazimisha vyombo vya ulinzi kuongeza nguvu kupambana nao.

Wakati wa kukabiliana na waharifu hao, Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) lililazimika kwenda eneo la tukio ili kukabiliana na majambazi hao huku wakiwapo askari wa kikosi cha ardhini cha jeshi hilo.

Wakati wa mapambano hayo yaliyokuwa makali, askari kadhaa wa JWTZ na polisi, walijeruhiwa kwa risasi na majambazi hao.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wananchi waliokuwa wakiishi jirani na mapango hayo, wakiwamo waishio katika Kijiji cha Mleni, walilazimika kuhama makazi yao baada ya kuhofia usalama wa maisha yao.
 
Toggle Footer
TOP