Loading...
Wednesday

[update: Taarifa rasmi] Waziri avunja Bodi ya TCU na kuwasimamisha kazi watendaji wakuu


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA

Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi

Taarifa kwa Vyombo vya Habari kuhusu kuhusu chuo cha Mtakatifu Josefu cha Tanzania (SJUIT)
Jukumu la kukagua, kupitisha na kusajili programu za shahada ya kwanza, shahada ya pili na shahada ya tatu liko chini ya mamlaka ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU). Vyuo na taasisi zote zinazoendesha mafunzo hayo kisheria zinatakiwa kupitisha programu zao kwenye tume hii na kupewa kibali kabla ya kuanza kuendesha programu husika. Pia udahili wa wanafunzi kwa shahada ya kwanza unafanywa na TCU.

Kumekuwepo matatizo ya muda mrefu kuhusu chuo cha Mtakatifu Josefu cha Tanzania (SJUIT). Mwezi Februari 2016 Serikali kupitia TCU iliunda Kamati ya Uchunguzi kuhusu ubora wa elimu inayotolewa na chuo hicho na chanzo cha migogoro ya muda mrefu baina ya wanafunzi na chuo. Kamati hizo ziligundua changamoto nyingi ambazo zilihitaji muda mrefu kuzitatua. Hivyo TCU iliamua kufunga kampasi za Songea na Arusha na kuhamishia wanafunzi vyuo vingine. Baadhi ya Changamoto ni kama ifuatavyo:

Aidha, uchunguzi ulionyesha kwamba kulikuwa na upungufu mkubwa wa maabara na vifaa au kutokuwepo kabisa vitu hivyo kwa ajili ya vitendo kwa masomo ya kampasi hizo. Baadhi ya ripoti ziliweka wazi kwamba mchakato wa uanzishaji kampasi hizo haukufuata taratibu ya kuangalia ubora na hivyo ilionekana wazi kwamba si tu kurekebisha bali kampasi hizo hazikutakiwa kupewa ruhusa ya kuanza kutoa mafunzo kwani hazikuwahi kufikia hata kiwango cha chini kabisa cha vigezo vya ubora wa maabara na hivyo vigezo vya ubora wa chuo kikuu. Huu ni udhaifu ambao TCU ilitakiwa kuuona wakati wakitoa kibali cha kuanzishwa kampasi hizo za chuo hiki au hata wakati kinaendeshwa.

Iligundulika kwamba chuo hiki hakikuwa na walimu wa kutosha wenye sifa. Mfano College ya kilimo ya kampasi Songea ni asilimia 17 tu wa walimu ndio walikuwa wanasifa stahiki na asilimia 83 hawakuwa na sifa za ama kufundisha Chuo Kikuu au hawakuwa na sifa za kufundisha masomo waliyopangiwa. Hali hii pia ilijitokeza kampasi ya Arusha. Pia chuo kilikuwa kimeajiri walimu wengi wa kigeni ambao wengi wao hawakuwa na vibali vya kuishi na kufanya kazi nchini na pia vyeti vyao havikuwahi kuhakikiwa na TCU.

Hata hivyo iligundulika kwamba baadhi ya mitaala ambayo ilikuwa inatumika ilikuwa haikidhi mahitaji ya shahada husika na wakati mwingine ilikuwa haifundishwi ipasavyo. Hii imepelekea wanafunzi kukosa maarifa na ufahamu wa masomo yao katika ngazi iliyotakiwa. Udhaifu katika mitaala na ufundishaji katika Chuo Kikuu cha St Joseph umejidhihirisha wazi baada ya kuwahamisha wanafunzi wa St Joseph katika vyuo vingine kutokana na mapungufu yaliyobainika katika vyuo hivyo. Baadhi ya vyuo wamewarudisha mwaka au muhula ili kupata muda wa kuwafundisha zaidi kama inavyoainishwa kwenye mifano:

1. Wanafunzi waliohamishiwa UDOM wamewekewa utaratibu ufuatao:
  • Mwaka wa tatu wote wamerudishwa nyuma mwaka mmoja hivyo kuanza masomo mwaka wa pili muhala wa kwanza.
  • Mwaka wa kwanza na wa pili wamerudishwa nyuma muhula mmoja.
2. Wanafunzi waliohamishiwa SUA walionekana wana udhaifu wa ufahamu kwa ngazi zao na hivyo:
  • Waliokuwa mwaka wa nne wamerudishwa mwaka wa tatu.
  • Wanafunzi wa kwanza na wa pili wanaendelea na miaka yao lakini wanachukua masomo ya ziada ambayo yanafundishwa baada ya ratiba ya kawaida.
3. Wanafunzi waliohamishiwa Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa walionekana wana udhaifu wa ufahamu kwa ngazi zao. Chuo hiki kiliona kwamba wanafunzi wa St. Joseph walikuwa na mapungufu katika masomo mbalimbali ambapo baadhi ya masomo wanatakiwa kuyarudia kabisa na baadhi ya masomo watayarudiwa kwa kiwango cha angalau asilimia 70 ya mada za somo zima.

Aidha, imeonekana kuwepo kwa tatizo la udahili wa wanafunzi wasio na sifa kwa programme ya digrii ya Ualimu wa Sayansi ya miaka 5. Jumla ya wanafunzi 489 waliodahiliwa kusoma Digrii ya Ualimu wameokana hawana sifa hata za kusomea Cheti cha Ualimu. Aidha, Wanafunzi hao walikuwa wanapata mikopo kinyume na taratibu za utoaji mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu.
Wapo wanafunzi ambao hawakuchukua masomo ya sayansi (Physics na Chemistry) na wengine waliochukua mkondo wa Biashara (Commerce na Book-keeping) lakini walikuwa wamedahiliwa kwenye Digrii ya Ualimu wa Sayansi.

Kutokana na udhaifu huu Serikali ilichukuwa hatua zifuatazo:

a) Katika barua yake ya tarehe 12 Mei 2016 yenye kumb Na. CFB 138/413/01D/79 serikali iliiagiza Kamisheni ya TCU kuwapumzisha kutekeleza majukumu baadhi ya watendaji ili kupisha uchunguzi. Hata hivyo Kamisheni haikutekeleza maagizo ya serikali.

b) Kwa barua ya tarehe 18/05/2016 yenye Kumb. Na. CAB. 40/78/01/68, Kamisheni iliieleza kuwa watumishi hao walitekeleza majukumu yao ipasavyo kudahili wanafunzi wa Kidato cha Nne na hatimaye kupeleka majina yao kwenye Bodi ya Mikopo ili wanufaike na mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya juu.

c) Serikali haikubaliani na maelezo ya Kamisheni na inaona kwamba TCU walishindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo wa kuhakiki na kusimamia ubora wa elimu. Udhaifu huo umesababisha wanafunzi wa Kidato cha Nne ambao hawana sifa za kujiunga hata na mafunzo ya Cheti cha Ualimu kudahiliwa kwenye Digrii ya Ualimu wa Sayansi na kupatiwa mikopo.

d) Serikali haiwezi kuvumilia Bodi ambazo zinashindwa kusimamia taasisi ambazo wamepewa kuzisimamia na hivyo maamuzi yafuatayo yamefanyika.

1 Uamuzi wa Serikali

a) Serikali inaunga mkono uamuzi wa TCU wa kufuta udahili kwa wanafunzi 489 waliokwishabainika kuwa hawana sifa. Wanafunzi hao hawakidhi hata hata vigezo vya kuchukua Mafunzo ya Cheti cha Ualimu. Aidha, Serikali imesitisha mara moja utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wenye sifa za kuchukua mafunzo ya Cheti cha Ualimu kwa kuwa ilitolewa kinyume na taratibu.

b) Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Mheshimiwa Profesa Joyce Lazaro Ndalichako, kwa mamlaka aliyopewa chini ya Sheria ya Vyuo Vikuu ya mwaka 2005 ametengua uteuzi wa wajumbe wa Kamisheni ya TCU kuanzia tarehe 25/05/2016.

c) Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye ndiye mamlaka ya Uteuzi wa Mwenyekiti, ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya TCU Prof. Awadhi S. Mawenya.

d) Ili kuleta nidhamu na ufanisi katika kutekeleza majukumu ya TCU, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dr. John Pombe Magufuli kwa mamlaka aliyonayo chini ya Ibara ya 36(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amemwagiza Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, kuwasimamisha kazi watendaji wa TCU waliohusika na suala hili. Kutokana na uamuzi huo, Waziri wa Elimu amewasimamisha kazi watumishi wafuatao:

i) Prof. Yunus Mgaya Katibu Mtendaji wa TCU kwa kushindwa kusimamia kazi za TCU kutokana na kuwepo wanafunzi wasiokuwa na sifa waliodahiliwa katika vyuo vikuu na kupata mikopo.

ii) Dr. Savinus Maronga Mkurugenzi wa Ithibati na Uthibiti Ubora (Director of Accreditation and Quality Assurance) kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake wa kusimamia ubora na ithibati ya vyuo vikuu

iii) Bi. Rose Kiishweko Mkurugenzi wa Udahili na Nyaraka (Director of Admission and Documentation) kwa kushindwa kusimamia udahili wa wanafunzi na kusababisha kudahiliwa wanafunzi wasio na sifa.

iv) Kimboka P. Stambuli – Afisa Msimamizi Mkuu wa Taarifa ambaye alihusika na udahili wa wanafunzi hao.

e) Ili kuwezesha shughuli za TCU ziendelee Waziri wa Elimu Sayansi Teknolojia na Ufundi amewateua wafuatao kukaimu nafasi zifuatazo hadi uchunguzi kuhusu suala hili utakapokamilika na maamuzi kufanyika:

i) Prof. Eleuther Mwageni kukaimu nafasi ya katibu mtendaji (Executive Secretary). Kabla ya uteuzi wa kukaimu nafasi hii Prof. Mwageni alikuwa Naibu Makamu Mkuu (Utawala na Fedha) wa Chuo Kikuu cha Ardhi.

ii) Dr. Kokubelwa Katunzi Mollel – Kukaimu nafasi ya Ukurugenzi wa udahili na Nyaraka (Admission and Documentation). Kabla ya uteuzi wa kukaimu nafasi hii Dr. Mollel alikuwa Coordinator wa Centre for Continuing Education, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Hitimisho

i) Wizara inapenda kuchukua fursa hii kuwataka Wakuu wote wa Vyuo Vikuu nchini kujiridhisha na sifa za wanafunzi wao na kamwe haitasita kumchukulia hatua kali yeyote atakayekiuka Sheria, Kanuni na Taratibu.

ii) Wizara imebaini kuwa wapo “Wanafunzi Hewa” wanaotafuna fedha za Mikopo inayotolewa jwa ajili ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu. Kwa Kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, msako mkali wa “Wanafunzi Hewa” utafanyika kwenye vyuo vyote nchini na hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kuhusika.

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya serikali,
Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi


Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako amevunja Bodi ya Tume ya Vyuo Vikuu nchini Tanzania (TCU) kufuatia Tume hiyo kupitisha majina ya wanafunzi 486 wasio na sifa kusomea Shahada ya Elimu.

Pia, Waziri Ndalichako amewasimamisha kazi Maofisa kadhaa waandamizi wa TCU kwa kushindwa kusimamia na kutekeleza vyema wajibu wa TCU na kuwateua Makaimu wa nafasi za waliosimamishwa.0 comments :

Post a Comment

 
Toggle Footer
TOP