Ahukumiwa kifungo cha jela miaka 3 au faini milioni 7 kwa "kumdhihaki Rais" kupitia Facebook

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa a Arusha, imemhukumu Isaac Habakuki (40) mkazi wa Olasiti, kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya shilingi milioni 7 kwa kosa la kumtukana Rais Magufuli kupitia mtandao wa Facebook.

Mshtakiwa amekiri kutenda kosa hilo na amekubali kulipa faini ambapo mahakama imeamuru alipe fedha hizo kwa awamu mbili. Katika awamu ya kwanza atalipa Julai 8, 2016 shilingi mililioni 3.5 na Agosti 8, 2016 atalipa kiasi kilichobakia.

Isack anayeishi Kata ya Olasiti, anadaiwa kutoa lugha ya matusi na dhihaka kwa Magufuli kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook na alikamatwa Machi 23, mwaka huu mjini Arusha na kupelekwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam kisha alirejeshwa tena Arusha Aprili 14, mwaka huu kwa ajili ya kufunguliwa mashtaka.

Mbele ya Hakimu Mkazi, Augustine Rwizile, Wakili wa Serikali, Gaudensia Massanja, alidai kuwa Isaac alikuwa akikabiliwa na kosa moja ambapo kwa kufahamu na kwa makusudi mtuhumiwa huyo alitumia mtandao wa Facebook kwa nia ya kumtukana Magufuli.

Alidai kwamba mtuhumiwa katika ukurasa wake wa Facebook alichangia maneno yanayosema: “Hizi ni siasa za maigizo halafu mnamfananisha huyu bwege na Nyerere wapi buana.”

Wakati huo huo sheria ya mtandao wa Facebook imewafungia watu wanne wanaotumia mtandao huo vibaya ikiwamo kukiuka sheria.

Mmoja wa waliopewa adhabu na mtandao wa Facebook, Malisa Golisten aliliambia gazeti hili kuwa amepewa adhabu ya kufungiwa kutumia mtandao huo kwa muda wa siku saba kutokana na kutolewa kwa taarifa na watu 50 kuwa anatumia mtandao huo kinyume na matakwa ya jamii yake

Pia amesema hivi karibuni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kupitia kituo cha luninga cha TBC ilitoa elimu juu ya kutoa taarifa kwa umiliki wa mtandao.

Malisa amesema kulikuwa na ufahamu juu ya uwepo wa sheria hiyo ambayo mtandao wa Facebook ulikuwa unataka watu watoe taarifa juu ya uvunjifu wa sheria na maadili kama kutuma picha za ngono, kutoa taarifa ambayo siyo ya kweli na ya kichochezi.