TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema serikali imeamua kusimamisha kwa muda mfupi usiozidi miezi miwili zoezi la utoaji ajira mpya na upandishaji wa vyeo kwa watumishi wa umma kwa lengo la kupisha uhakiki wa watumishi wa umma katika orodha ya malipo ya mshahara na kuondoa watumishi hewa.
Rais Magufuli amesema hayo leo tarehe 22 Juni, 2016 katika Jubilei ya miaka 50 ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) iliyofanyika katika ukumbi wa Benki hiyo, Mtaa wa Mirambo Jijini Dar es salaam.
Dkt. Magufuli amesema zoezi hilo halina nia ya kuwakatisha tamaa watumishi wa umma na amewahakikishia watumishi wote wa umma kuwa serikali itaendelea kuajiri watumishi wapya na kuwapandisha vyeo waliopo kama kawaida mara baada ya kukamilika kwa zoezi.
"Serikali ninayoiongoza haina nia ya kuwakatisha tamaa wafanyakazi, lengo lake ni kujipanga kwa makosa tuliyoyafanya, na ndio maana nimesema kwa kipindi cha mwezi mmoja hivi au hata mwezi mmoja na nusu, haitazidi miezi miwili, tusiajiri mtumishi yeyote serikalini, lakini pia katika kipindi cha mwezi mmoja hatutawapandisha vyeo wafanyakazi, ninaomba wafanyakazi waelewe hili, kwa sababu tukiendelea tutakuwa tunawapandisha vyeo hata wafanyakazi ambao hawapo, tunafanya ukaguzi wote tukishamaliza wafanyakazi wataendelea kupandishwa vyeo" amesema Rais Magufuli.Wakati huo huo, Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania kwa kazi kubwa iliyoifanya katika kipindi cha miaka 50 katika kusimamia sekta ya fedha na maendeleo, lakini ameitaka benki hiyo kuchukua hatua za haraka dhidi ya baadhi ya changamoto zinazoyahusu majukumu yake.
Miongoni mwa changamoto hizo ni idadi ndogo ya watanzania wanaonufaika na huduma za benki hususani waishio vijijini, benki kutoza riba kubwa na hivyo kusababisha wananchi kuogopa kukopa kwa hofu ya kushindwa kulipa, kuilinda thamani ya Shilingi ya Tanzania, na kukusanya kodi ipasavyo kwa miamala inayofanywa kupitia simu za mkononi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Changamoto nyingine ni kusimamia ipasavyo maduka ya kubadilishia fedha (Bureau de change) ili kuthibiti utakatishaji na utoroshaji wa fedha na kuhakikisha ushukaji wa mfumuko wa bei uliotoka asilimia 28 hadi kufikia asilimia 5.1 katika kipindi cha miaka 15 iliyopita unaonesha matokeo katika nafuu ya maisha ya watanzania.
Aidha, Rais Magufuli ameiagiza Benki Kuu ya Tanzania kuchukua hatua mara moja dhidi ya benki ambazo hazizalishi faida zikiwemo benki za serikali, kufuta account mfu (Domant account) na kuanzisha mara moja akaunti moja ya mapato na matumizi ya serikali (Single Treasury Account)
Jubilei hiyo imehudhuriwa na Magavana na Manaibu Gavana kutoka nchi 18 za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika (SADC), Mabalozi kutoka nchi mbalimbali, Viongozi wa Taasisi za fedha za Afrika na Makatibu wakuu wa Wizara za Fedha na Mipango wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
22 Juni, 2016
SERIKALI imesitisha ajira zote, kama njia ya kukabiliana na wimbi la watumishi hewa.
Kutokana na uamuzi huo hivi sasa hakuna nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa Serikali na wakala zake pamoja na utoaji wa vibali wa likizo ya bila malipo.
Akizungumza na MTANZANIA jana jijini Dar es Salaam Katibu Mkuu Utumishi, Dk. Laurean Ndumbaro, alisema kuwa Serikali imesitisha kwa muda utoaji wa ajira, ili kupitia upya muundo wa Serikali na taasisi zake.
Alisema utekelezaji wa mkakati huo utakwenda sambamba na kusitisha kwa muda utoaji wa vibali vya ajira zote mbadala pamoja na uidhinishaji wa ajira hizo zilizopo Sekreterieti ya Ajira katika utumishi wa umma na kwenye mfumo wa taarifa za kiutumishi.
“Ni kweli tumesitisha kwa muda ili kupitia mfumo wa Serikali na hata kuangalia ulipaji wa mishahara kama upo katika malipo stahiki.
“…na hili litakwenda sambamba na hata kusitishwa malipo ya mishahara yanayotokana na upandishwaji wa vyeo kwa watumishi. Tukimaliza zoezi hili ndipo tunaweza kuanza kutoa ajira za Serikali,” alisema Dk. Ndumbaro.
Alisema muundo mpya wa utumishi wa Serikali unakwenda sambamba na uhakiki wa malipo ya mishahara, hivyo ni lazima ujue ni nani unayemlipa kuliko ilivyo sasa.
Kwa mujibu wa maelekezo hayo uhamisho na uidhinishaji katika mfumo wa watumishi ambao wamehamishwa kutoka kwa mwajiri mmoja kwenda kwa mwajiri mwingine ambao atalipwa mshahara mkubwa kuliko ule wa sasa pia utaangaliwa kwa lengo la kupata taarifa sahihi za mtumishi husika.
“Baada ya kukamilika kwa zoezi la uhakiki watumishi pamoja na tathmini ya muundo wa Serikali na taasisi zake, wote wataarifiwa ni lini utekelezaji utaendelea,” alisema.
Taarifa kutoka maeneo mbalimbali nchini, zililiambia gazeti hili kuwa maelekezo hayo yalitolewa Juni 13, mwaka huu na kusambazwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo kwa makatibu wakuu wote, makatibu tawala wa mikoa, kwa wakuu wa idara za Serikali zinazojitegemea.
Waliotakiwa kutekeleza maelekeo hayo ya Serikali ni wakurugenzi wote wa majiji, manispaa na miji, wakurugenzi watendaji wa halmashauri za wilaya, watendaji wa taasisi za umma na watendaji wa wakala za Serikali kwa upande wa Tanzania Bara.
Kamata kamata
Wiki iliyopita vyombo vya dola vilianza kuwatia mbaroni watumishi hewa kwa kuwafuata na pingu majumbani.
Hatua hiyo imetajwa kuwa ni mkakati wa Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli, kuanza kupambana na watendaji ambao wamekuwa wakiisababishia hasara Serikali ya kulipa mamilioni ya shilingi kwa watumishi hewa.
Kutokana na uamuzi huo ambapo mtumishi mmoja wa moja za za Mkoa wa Kigoma, alifuatwa na askari wa polisi na kutiwa mbaroni nyumbani kwao Ubungo Kibangu jijini Dar e Salaam.
Tukio hilo la aina yake lilitokea mchana wa juzi na kuibua hisia miongoni mwa majirani ambao waliliambia gazeti hili kuwa, askari hao walifika nyumbani kwao na mtumishi huyo na kumfunga pingu mikono na miguuni na kuondoka naye.
Kutokana na hekaheka hiyo ya watumishi hewa, taarifa kutoka wilayani Nyasa mkoani Ruvuma, zililieleza gazeti hili kuwa walimu watano wastaafu nao walikamatwa na polisi kwa madai ya kupokea mishara hewa.
Mbali na walimu hao pia alikuwepo muuguzi mmoja.
Akizungumzia na MTANZANIA kuhusu tukio hilo la kamatakamata mmoja wa waliokumbwa na hali hiyo, Marco Nyimbi ambaye ni mwalimu mstaafu wa Shule ya Msingi Muungano wilayani Nyasa mkoani Ruvuma alisema hatua ya kukamatwa kwake ilimfanya apigwe na butwaa na kushangazwa na hatua ya kukamatwa yeye na wenzake watano kwa kudaiwa kuwa ni watumishi hewa.
Hivi karibuni akizungumza Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki, alisema Serikali imewaondoa jumla ya watumishi 12,246 kwenye mfumo wa malipo ya mishahara kwa sababu mbalimbali, ikiwemo umri wa kustaafu kwa lazima, kufukuzwa kazi, vifo na kumalizika kwa mikataba.
Waziri Kairuki alisema kuondolewa kwa watumishi hao kumeokoa Sh bilioni 25 ambazo zingelipwa kwa watumishi hao.
Alisema kuwa fedha hizo zingepotea endapo watumishi wasingeondolewa kwenye mfumo, ikilinganishwa na watumishi 10, 295 walioondolewa kwenye mfumo kuanzia Machi 15 hadi Aprili 30 mwaka huu.
Alisema pia kuwa watumishi hewa 1,951 wameongezeka ikiwa ni pamoja na Sh bilioni 1.8.
Alifafanua kuwa ofisi hiyo ilitoa maelekezo kwa Makatibu Wakuu, Wakuu wa taasisi za umma na Mamlaka za Serikali za Mitaa, kuwasilisha taarifa ya watumishi hewa ifikapo Juni 10, mwaka huu.