Aonya 'vimemo' vinavyopelekwa kuwaombea msamaha watumishi wazembe

NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jaffo, amewataka wabunge kuacha kuwapelekea viongozi ‘vimemo’ vya kuwaombea msamaha watumishi wasio na maadili wa hospitali mbalimbali nchini watakapokuwa wanatumbuliwa.

Alitoa angalizo hilo jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Masasi Mjini (CCM), Rashid Chuachua, aliyetaka kujua hatua zilizochukuliwa dhidi ya watendaji wa Hospitali ya Wilaya ya Masasi ya Mkomaindo kutokana na ubadhirifu wa dawa uliofanywa mwaka 2014.

Alisema wizara yake iko katika uchunguzi wa kina kuhusu madudu mbalimbali yaliyofanywa katika maeneo mbalimbali nchini yanayohusiana na wizara hiyo zikiwemo hospitali na muda si mrefu wahusika wataanza kuchukuliwa hatua.
“Watendaji wasiofaa tutawashughulikia na ninawaomba wabunge msituletee vimemo kwamba huyu ni ndugu yangu au hivi wakati tutakapoanza kuchukua hatua,” alisema Naibu Waziri huyo.
Kuhusu kupandisha zahanati kuwa vituo vya afya, Jaffo aliishauri Halmashauri ya Masasi kuanzisha mchakato huo kupitia vikao na kuwasilisha mapendekezo hayo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ili kupata kibali.