Diallo amwomba radhi Dk Mwakyembe na kupiga marufuku gazeti la DIRA kusomwa StarTv

Wakati Mhariri wa Gazeti la Dira na mwenzake wako mahakamani kujibu mashitaka ya tuhuma za kuandika na kusambaza taarifa za uongo kwa lengo la kusababisha hofu nchini, uongozi wa StarTV umepiga marufuku gazeti hilo kusomwa asubuhi na kumwomba radhi Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe kwa usumbufu aliopata kwa kituo hicho cha runinga kulisoma gazeti hilo tata siku ya Jumatatu tarehe 20 Juni, 2016.

Taarifa kutoka ndani ya Sahara Media Group Ltd, wamiliki wa StarTv, zimesema msimamo huo ulichuliwa na kiongozi wao mkuu Anthony Diallo jana na taarifa hizo zimethibitishwa leo kwa njia ya simu na Dk. Mwakyembe.
"Ni kweli nimeongea na Diallo, nimeelewa changamoto za kuongoza watu wengi na nimepokea apology yao, jambo ambalo ni uungwana.
"Nimefarijika kuwa nao wametambua kuwa gazeti hilo halina viwango, hivyo hawatalisoma tena asubuhi", alisema Dk. Mwakyembe.
Wakati huohuo, Waziri huyo mwandamizi katika Serikali ya Awamu ya Tano amesema maandalizi ya kufungua kesi ya kashifa dhidi ya mmiliki, mhariri, mchapishaji na wasambazaji wa taarifa za uongo za gazeti hilo yanaendelea vizuri.