Hii aibu ifutwe! Kutoka kuongoza kielimu hadi kuongoza kugida mataptap, Kilimanjaro, Dar; Kulikoni?

ASILIMIA 87 ya watanzania wanakunywa pombe za kienyeji huku Mikoa wa Dar es salaam na Moshi ikiongoza kwa kuwa na wanywaji wengi wa pombe.

Sambamba na hilo, kwa sasa vijana wengi wanatumia pombe kupita kiasi kuanzia shule ya msingi hadi Vyuo Vikuu hali inayosababisha kukumbwa na magonjwa ya akili na kujiingiza kwenye vitendo vya uhalifu.

Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Katibu Mkuu wa Chama cha Wataalam wa Afya ya Akili Tanzania (MEHATA), Dk. Kissah Mwambene, alipokuwa akitoa mada kwa wabunge juu ya athari za matumizi ya pombe iliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), mjini hapa.

Alisema takwimu hizo zinatokana na utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2010 nchini ambapo kumekuwepo na ongezeko la unywaji pombe kupita kiasi na kusababisha uwepo na ukatili wa kijinsia kwa jamii.

Mwambene alisema utafiti huo ulifanywa kwa watu wenye umri wa kuanzia miaka 15 na unywaji pombe kwa ujumla ikiwemo za kienyeji na za kiwandani asilimia wanaume ni 40.6 na wanawake ni asilimia 23.3.

Alibainisha ukatili wa mwanaume kwa wanawake ni mkubwa sana na kuwepo na magovi katika jamii, mauaji ya kikatili na wengine kupata madhara mengi ya kijamii na kiuchumi.

Hata hivyo, alisema hali hiyo pia inasababisha urahisi wa kupata magonjwa ya akili huku akiwatahadharisha kina mama mjamzito wanaotumia pombe kuwa wanaweza kuzaa watoto wenye sura ya tofauti na wenye mtindio wa ubongo.
“Pombe inasababisha matatizo ya kujiua yanaongezeka na Tanzania kwa utafiti wa mwaka juzi imekuwa ni nchi ya nane kwa kuongoza na vitendo vya watu kujiua,” alisema Mtaalamu huyo
Kwa upande wake, Mtaalamu wa Tafiti za Afya (TPHA), Dk.Shaibu Mashombo, alisema matumizi ya pombe kupita kiasi yanafanya wanaume kushindwa kupata watoto na uwezo wa kufanya kazi na taraka kuongezeka.

Akifungua semina hiyo, Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangalla, alisema ni ulevi ni tatizo kubwa katika jamii huku akitaja kwa maeneo ya Dar es Salaam ikiwemo Kinondoni, Salanga na Makumbusho yanaongoza. 

Aidha alisema asilimia 30 ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 15 wameanza ulevi na asilimia 80 ya wasomi ni watu wanaotumia pombe huku asilimia 63 wanaoishi jirani na vilabu vya pombe ni wanatumia kilevi.

Naye Mratibu wa semina hiyo kutoka TAMWA, Gladness Munuo alisema kuna haja ya kuweka sera na sheria nzuri za kuzuia ulevi.

Kwa upande wao wabunge wakichangia walishauri kupigwa marufuku uuzwaji wa pombe za viroba kwa kuwa vinaathiri vijana wengi.