Hospitali ya Taifa Muhimbili yafuta utaratibu wa ndugu kupelekea wagonjwa chakula


Hospitali ya taifa Muhimbili imeboresha huduma zake kwa wagonjwa kwa kuingia ubia na mzabuni ili kutoa huduma ya chakula kwa wagonjwa wote waliolazwa hospitalini hapo.

Utaratibu huo kuanza kutumika kuanzia julai mosi mwaka huu.

Uboreshwaji wa huduma hii unalenga kuitaka hospitali kujikita katika majukumu yake ya msingi ya kushauri, kutafiti na kutibu.

Pia, inalenga kuondokana na msongamano wa watu ndani ya hospitali kutwa nzima, kwani huingiliana na utoaji huduma hasa kwa saa za mchana.

Baadhi ya ndugu wa wagonjwa wameliunga mkono suala hilo, baadhi yao wakisema kuwa huduma hiyo itawaondolea gharama kubwa hususani za usafiri wa kuja hospitalini mara tatu kwa siku kwani baadhi ya ndugu wamekuwa wakishindwa kuwapelekea chakula jamaa zao hasa wale wanaotoka nje ya mkoa na wasio na ndugu Dar es Salaam. Hata hivyo, hospitali hiyo imekuwa ikitoa chakula kwa wagonjwa wasio na ndugu, jamaa au marafiki wa kuwasaidia.Mkurugenzi wa Uuguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Agness Mtawa akifafanua jambo. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma, Aminiel Aligaesha.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Bw. Aminiel Aligaesha akizungumza.

  • Yawaondolea usumbufu ndugu wa wagonjwa kupeleka chakula mara tatu kwa siku
  • ·Ndugu watapata muda wa kuendelea na shughuli za uzalishaji
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeboresha huduma za chakula kwa wagonjwa wote watakaolazwa kuanzia Julai Mosi, mwaka huu ili kuwaondolea ndugu wa wagonjwa usumbufu na gharama za usafiri wakati wa wanapokwenda kuwaona ndugu zao waliolazwa mara tatu kwa siku katika hospitali hiyo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma, Hospitali ya Taifa Muhimbili Bw. Aminiel Aligaesha amesema hospitali imeingia ubia na mzabuni ili kutoa huduma hiyo kwa wagonjwa wote wanaolazwa.

Bw. Aligaesha amesema Hospitali inataka kujikita katika majukumu yake ya msingi ambayo ni kushauri, kuchunguza na kutibu.

“Aidha Hospitali inataka kuwaondelea adha ndugu wa wagonjwa ambao wamekuwa wakiingia gharama kubwa hususani usafiri wa kuja Hospitalini mara tatu kwa siku, ambapo kwa kukadiria gharama ya usafiri wa ndugu mmoja wa mgonjwa ni kati ya shilingi 6,000/= na 10,000/= kwa siku, kulingana na mahali anapotokea bila kujumuisha gharama za kuandaa chakula cha mgonjwa ambacho mara nyingi ni chakula maalumu. Na kama mgonjwa akilazwa zaidi ya siku tano hadi 10 ndugu mmoja wa mgonjwa gharama atalipia fedha nyingi kwenye usafiri” amesema Bw. Aligaesha
Ameongeza kuwa adha ya pili wanayopata ndugu ni usumbufu ambapo inabidi kuacha shughuli nyingine za uzalishaji ili kuja kuleta chakula mara tatu kwa siku, hivyo kuingiliana na shughuli zao za kiuchumi na kimandeleo na kushindwa kuzalisha. Hivyo jukumu hili linachukuliwa na Hospitali kuwaondolea adha hii.
“Pia kuna baadhi ya ndugu wamekuwa wakishindwa kuwaletea chakula wagonjwa wao hivyo hospitali ililazimika kuwapatia chakula ambacho kilikuwa kwa ajili ya wagonjwa wanaotoka mikoani wasio na ndugu hapa Dar Es Salaam” amesisitiza Bw. Aligaesha.
Amesema kumekuwepo na ongezeko la msongamano wa watu ndani ya Hospitali toka asubuhi saa 12 mpaka saa 12 jioni, suala linaloingiliana na utoaji huduma hasa saa za mchana kwani muda wa saa 6.00 hadi saa 8.00 mchana ulikuwa unaingiliana na majukumu ya kiutendaji ambapo majopo mbalimbali ya watalaamu yamekuwa yakiendelea na raundi za wagonjwa waliolazwa. Hii wakati mwingine imesababisha mgonjwa kutokupata huduma stahiki kutokana na muingiliano huu.
“Vile vile msongamano huu ni changamoto kwa ajili ya masuala ya kiusalama ambapo kati ya watu wanaoingia Hospitali kwa kigezo cha kuja kuona wagonjwa kuna wanaoingia kwa lengo la kufanya uhalifu ikiwemo wizi wa mali za Hospitali, magari pamoja na vifaa vya magari” alisisitiza.
Amesema kwa kufanya hivyo, Hospitali itapunguza baadhi ya gharama za uagizaji wa vyakula kwa wazabuni, kulinda upotevu na baadhi ya vyakula kuharibika wakati mwingine kwani utunzaji wa vyakula una mahitaji makubwa.

Bw. Aligaesha amesema Hospitali inakusudia kutoa chakula chenye ubora na viwango vinavyotakiwa kwa wagonjwa ikiwemo kutoa chakula maalumu (special diet) kwa wagonjwa wenye uhitaji huo.

Kuhusu utaratibu huo Bw. Aligaesha amesema Mzabuni ndiye atakayepika chakula kwa wagonjwa wote waliolazwa na atatayarisha, atakipeleka na kukikabidhi katika wodi husika ambapo jukumu la kumpa mgonjwa kifungua kinywa, chakula cha mchana na jioni linabaki wa Hospitali.

Amesema wagonjwa watapatiwa milo mitatu kwa siku yaani asubuhi, mchana na jioni kazi itakayofanywa na muuguzi wa zamu ambaye atahakikisha wagonjwa wote wamepata chakula kufuatana na mahitaji (diet list) iliyowasilishwa jikoni kutokana na mahitaji yao ya kiafya.

Kutokana na uamuzi huu, utaratibu wa ndugu kuleta chakula kwa wagonjwa waliolazwa wakati wa mchana umefutwa na hivyo mchana hatutakuwa na nafasi ya ndugu kuja kutembelea wagonjwa. Muda wa kutembelea wagonjwa utakuwa asubuhi saa 12 hadi saa moja kamili na saa 10:00 jioni hadi saa 12:00 jioni ndipo ndugu wataruhusiwa kuingia ndani kuwaona ndugu zao waliolazwa. Katika muda huo ndugu ataruhusiwa kuja na chakula chochote anachofikiri atamuongezea mgonjwa wake kama matunda n.k

Bw. Aligaesha amesema mgonjwa aliyelazwa atachangia kiasi cha shilingi 50,000 atakapolazwa ambapo kati ya hizo, shilingi elfu 10,000 itakuwa ni gharama ya kumuona daktari (Consultation), shilingi elfu 10,000 ikiwa ni gharama ya kulazwa na bei ya chakula itakuwa shilingi elfu 30,000 sawa na shilingi elfu 6,000 kwa siku. Wastani wa mgonjwa kukaa wodini ni siku tano. Gharama hizo zinahusika kwa muda wote atakaokuwa amelazwa.

Kwa sasa Hospitali inatoa chakula kwa wagonjwa 650 ambao wamepata rufaa kutoka hospitali za nje ya mkoa wa Dar es Salaam kwa gharama wastani wa shilingi 1.8 bilioni kwa mwaka, sawa na shilingi 150 milioni kwa mwezi kwa vyakula pamoja na gharama nyingine kama vile za nishati. Takribani wagonjwa kati ya 600 na 700 ambao rufaa zao ni kutoka Hospitali za Dar es Salaam walikuwa hawapati chakula kutoka Hospitalini, na ilibidi ndugu zao wawaletee chakula. Hata hivyo, Hospitali ilikuwa inawapatia chakula tu kama ndugu zao wakishindwa kufanya hivyo.
“Uongozi wa Hospitali unaamini kwamba mabadiliko haya hayatamuongezea mgonjwa gharama, bali yatampunguzia gharama pamoja na ile adha kama ilivyoainishwa hapo juu. Aidha, uongozi unaamini kwamba uamuzi huu unaendana na azma nzima ya kuboresha utoaji huduma katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuboresha mazingira ya Hospitali. Tunaomba ushirikiano wenu katika kutekeleza jukumu hili ili kusudi wagonjwa waweze kuhudumiwa vizuri zaidi” amesisitiza Bw. Aligaesha.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma wa MNH, Aligaesha akifafanua jambo kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI KUINGIA UBIA NA MZABUNI ILI KUTOA HUDUMA YA CHAKULA KWA WAGONJWA WOTE WALIOLAZWA


Utangulizi:

Hospitali ya Taifa Muhimbili imeingia ubia na mzabuni ili kutoa huduma ya chakula kwa wagonjwa wote waliolazwa kuanzia tarehe 1 Julai, 2016.

Kwa nini Hospitali imechukua hatua hii;

Hospitali inataka kujikita katika majukumu yake ya msingi ambayo ni kushauri, kuchunguza na kutibu.

b. Aidha Hospitali inataka kuwaondelea adha ndugu wa wagonjwa ambao wamekuwa wakiingia gharama kubwa hususani usafiri wa kuja Hospitalini mara tatu kwa siku, ambapo kwa kukadiria gharama ya usafiri wa ndugu mmoja wa mgonjwa anaweza kutumia kati ya shilingi 6,000/= na 10,000/= kwa siku, kulingana na mahali anapotokea bila kujumuisha gharama za kuandaa chakula cha mgonjwa ambacho mara nyingi ni chakula maalumu. Na kama mgonjwa akilazwa zaidi ya siku tano hadi 10 ndugu mmoja wa mgonjwa gharama atalipia fedha nyingi kwenye usafiri.

c. Adha ya pili wanayopata ndugu ni usumbufu ambapo inabidi kuacha shughuli nyingine za uzalishaji ili kuja kuleta chakula mara tatu kwa siku, hivyo kuingiliana na shughuli zao za kiuchumi na kimandeleo na kushindwa kufanya uzalishaji. Hivyo jukumu hili linachukuliwa na Hospitali kuwaondolea adha hii.

d. Pia kuna baadhi ya ndugu wamekuwa wakishindwa kuwaletea chakula wagonjwa wao hivyo hospitali ililazimika kuwapatia chakula ambacho kilikuwa kwa ajili ya wagonjwa wanaotoka mikoani wasio na ndugu hapa Dar Es Salaam.

e. Kumekuwepo na ongezeko la msongamano wa watu ndani ya Hospitali toka asubuhi saa 12 mpaka saa 12 jioni, suala linaloingiliana na utoaji huduma hasa saa za mchana kwani muda wa saa 6.00 hadi saa 8.00 mchana ulikuwa unaingiliana na majukumu ya kiutendaji ambapo majopo mbalimbali ya watalaamu yamekuwa yakiendelea na raundi za wagonjwa waliolazwa. Hii wakati mwingine imesababisha mgonjwa kutokupata huduma stahiki kutokana na muingiliano huu.

Vile vile msongamano huu ni changamoto kwa ajili ya masuala ya kiusalama ambapo kati ya watu wanaoingia Hospitali kwa kigezo cha kuja kuona wagonjwa kuna wanaoingia kwa lengo la kufanya uhalifu ikiwemo wizi wa mali za Hospitali, magari pamoja na vifaa vya magari.

g. Kupunguza baadhi ya gharama za uagizaji wa vyakula kwa wazabuni, kulinda upotevu na baadhi ya vyakula kuharibika wakati mwingine kwani utunzaji wa vyakula una mahitaji makubwa.

h. Aidha Hospitali inakusudia kutoa chakula chenye ubora na viwango vinavyotakiwa kwa wagonjwa ikiwemo kutoa chakula maalumu (special diet) kwa wagonjwa wenye uhitaji huo.

Utaratibu wa chakula cha mzabuni kwa wagonjwa

a. Mzabuni ndiye atakayepika chakula kwa wagonjwa wote waliolazwa na atatayarisha, atakipeleka na kukikabidhi katika wodi husika.

b. Jukumu la kumpa mgonjwa kifungua kinywa, chakula cha mchana na jioni linabaki wa Hospitali.

c. Wagonjwa watapatiwa milo mitatu kwa siku yaani asubuhi, mchana na jioni

d. Wagonjwa watagawiwa chakula na muuguzi wa zamu ambaye atahakikisha wagonjwa wote wamepata chakula kufuatana na mahitaji (diet list) iliyowasilishwa jikoni kutokana na mahitaji yao ya kiafya.

Hata hivyo ndugu wataruhusiwa kuja na matunda pale watakapoweza hususani wakati wa jioni.

Muda wa kuona wagonjwa

Kutokana na uamuzi huu, utaratibu wa ndugu kuleta chakula kwa wagonjwa waliolazwa wakati wa mchana umefutwa na hivyo mchana hatutakuwa na nafasi ya ndugu kuja kutembelea wagonjwaMuda wa kutembelea wagonjwa utakuwa asubuhi saa 12 hadi saa moja kamili na saa 10:00 jioni hadi saa 12:00jioni ndipo ndugu wataruhusiwa kuingia ndani kuwaona ndugu zao waliolazwa.

c. Katika muda huo ndugu ataruhusiwa kuja na chakula chochote anachofikiri atamuongezea mgonjwa wake kama matunda n.k

Uchangiaji huduma ya chakula

Kutokana na sababu nilizozieleza hapo juu, mgonjwa aliyelazwa atachangia kiasi cha shilingi 50,000 atakapolazwa ambapo kati ya hizo, shilingi elfu 10,000 itakuwa ni gharama ya kumuona daktari(Consultation), shilingi elfu 10,000 ikiwa ni gharama ya kulazwa na bei ya chakula itakuwa shilingi elfu 30,000 sawa na shilingi elfu 6,000 kwa siku. Wastani wa mgonjwa kukaa wodini ni siku tano. Gharama hizo zinahusika kwa muda wote atakaokuwa amelazwa.

Kwa sasa Hospitali inatoa chakula kwa wagonjwa ambao wamepata rufaa kutoka hospitali za nje ya mkoa wa Dar es Salaam, ambapo kwa wastani, idadi ya wagonjwa 650 hupatiwa chakula kwa siku. Gharama ya kuwalisha wagonjwa hawa ni wastani wa shilingi 1.8 bilioni kwa mwaka, sawa na shilingi 150 milioni kwa mwezi kwa vyakula pamoja na gharama nyingine kama vile za nishati n.k.

Hii ina maana kwamba takribani wagonjwa kati ya 600 na 700 ambao rufaa zao ni kutoka Hospitali za Dar es Salaam walikuwa hawapati chakula kutoka Hospitalini, na ilibidi ndugu zao wawaletee chakula. Hata hivyo, Hospitali ilikuwa inawapatia chakula tu kama ndugu zao wakishindwa kuwaletea.

Hitimisho;

Uongozi wa Hospitali unaamini kwamba mabadiliko haya hayatamuongezea mgonjwa gharama, bali yatampunguzia gharama pamoja na ile adha kama ilivyoainishwa hapo juu. Aidha, uongozi unaamini kwamba uamuzi huu unaendana na azma nzima ya kuboresha utoaji huduma katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuboresha mazingira ya Hospitali. Tunaomba ushirikiano wenu katika kutekeleza jukumu hili ili kusudi wagonjwa waweze kuhudumiwa vizuri zaidi.

Imetolewa na;


Aminiel Aligaesha,
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano,
Hospitali ya Taifa Muhimbili,

Juni 21, 2016