Loading...
Thursday

KUB yawasilisha kwa Katibu wa Bunge hoja ya kutokuwa na imani na Naibu Spika Tulia Ackson

Wabunge wa upinzani wamewasilisha kwa Spika wa Bunge hoja ya kumwondoa madarakani Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kwa kutokuwa na imani naye.

Hatua hiyo imefikiwa na wabunge hao kufuatia kutoridhishwa na mwenendo wa uongozi wa Dk Tulia anapokalia kiti cha Spika.

Tangu Jumanne wiki hii, wabunge hao wamekuwa wakisusa vikao vinavyoongozwa na kiongozi huyo kwa madai anaminya demokrasia.

Walifikia uamuzi huo baada ya Dk Tulia kuzuia kujadiliwa hoja ya kufukuzwa kwa wanafunzi zaidi ya 7,000 wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDom) iliyowasilishwa na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari na kukatisha mjadala wa bajeti ya maji.

Kitendo hicho kiliwafanya wabunge wote wa upinzani kupingana na maamuzi ya Dk Tulia, jambo lililosababisha watolewe bungeni.

Kutokana na hali hiyo wabunge hao kupitia Mbunge wa Simanjiro, James Ole Millya akisindikizwa na Mbunge wa Kibamba, John Myika wa CHADEMA na Mbunge wa Konde wa CUF, Khatibu Said Haji waliwasilisha hoja hiyo kwa Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah baada ya Spika, Job Ndugai kutokuwapo bungeni.

Hoja hiyo iliwasilishwa kwa mujibu wa Kanuni ya 138(1) ambayo inaeleza utaratibu wa jinsi ya kumwondoa Naibu Spika.

Kanuni hiyo inasema, “Utaratibu wa kumwondoa Naibu Spika madarakani chini ya Ibara ya 85(4)(c) ya Katiba utakuwa kama ule wa kumwondoa Spika, isipokuwa tu taarifa ya kusudio la kumwondoa Naibu Spika madarakani inayoeleza sababu kamili za kuleta hoja hiyo, itapelekwa kwa Spika ambaye ataiwasilisha kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa ajili ya kuijadili.”

Fasiri ya pili ya Kanuni hiyo inasema: “Endapo Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge itaridhika kuwa zipo tuhuma mahususi dhidi ya Naibu Spika zinazohusu uvunjaji wa Katiba, Sheria au Kanuni zinazoongoza Shughuli za Bunge, basi Kamati hiyo itaidhinisha kuwa hoja hiyo ipelekwe bungeni ili iamuliwe.”

Kwa mujibu wa Ibara ya 85(4)(c), Naibu Spika atakoma kuwa Naibu Spika na ataacha kiti cha Naibu Spika endapo ataondolewa kwenye madaraka ya Naibu Spika kwa azimio la Bunge.
  1. Akizungumza na waandishi wa habari jana kwa niaba ya wabunge hao, Mbunge wa Simanjiro, James Millya alizitaja sababu hizo kuwa ni kwanza Dk Tulia ameweka maslahi ya chama chake cha siasa mbele kuliko maslahi ya Bunge, kinyume na Kanuni ya 8(b) ya Bunge.

  2. “Pili, Mei 6 alitumia vibaya madaraka ya kiti cha Spika kwa kutoa uamuzi wa mwongozo ambao ulikuwa unakiuka Ibara ya 12(2) ya Katiba. Muongozo huo uliokuwa unapinga udhalilishaji wa wabunge wanawake,” alisema.

  3. Ya tatu ni kitendo cha Dk Tulia kuvunja Kanuni ya 64(1) (f) na (g) zinazokataza mbunge kutumia lugha ya matusi kwa mbunge mwingine ambapo alinukuliwa akisema “Mheshimiwa Bwege, usionyeshe ubwege wako humu ndani.”

  4. Alisema ya nne ni Mei 30 kiongozi huyo aliamua kwa makusudi kuvunja Ibara ya 63(2) ya Katiba na kutumia vibaya Kanuni ya 69(2) na 47(4) ya Kanuni za Bunge kumzuia Joshua Nassari kwa upande mmoja na Bunge zima kwa upande wa pili kutimiza majukumu yake ya kikatiba ya kusimamia na kuishauri Serikali.

  5. “Sababu ya tano ni kuwa Mei 26, mwaka huu Dk Ackson akiongoza kikao cha Bunge bila ridhaa ya upinzani alishiriki kufuta sehemu ya hotuba ya msemaji wa upinzani kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kinyume cha kanuni ya 99(9) ya Bunge bila kushirikisha kamati yoyote ya Bunge,” alisema.

  6. Sababu ya sita, Millya alisema kuwa ni kitendo cha Dk Ackson kukataa taarifa ya maoni tofauti, iliyowasilishwa na wabunge wanne wa upinzani.
Dk Tulia aliwataka wabunge wenye malalamiko juu ya utaratibu wa uendeshaji wa shughuli za Bunge kukata rufaa kwa kufuata Kanuni za Bunge.

Alisema kanuni ndogo ya 5(2) inasema Spika atawajibika kutilia nguvu kanuni zote za Bunge na 5(3) inasema Spika anaweza kumtaka mbunge yeyote anayekiuka kanuni hizi kujirekebisha mara moja.

Alisema kwa hiyo mbunge yoyote asiyeridhika, kanuni za Bunge zinamruhusu kukata rufaa na zinamweleza nini cha kufanya.
 
Toggle Footer
TOP