Lissu, gazeti la MAWIO waitwa mahakamani kujibu mashtaka ya njama na uchochezi Zanzibar

(picha: Mtanzania)
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, yatoa hati ya wito kwa Mbunge Singida Mashariki, Tundu Lissu (48) na mwenzake, wa kwenda kujibu mashtaka ya kula njama na kutoa lugha ya uchochezi kwa watu wa Zanzibar.

Mbali na Lissu mshtakiwa mwingine aliyepewa wito huo ni Mhariri wa Gazeti la Mawio, Jabir Idrissa (52) huku Mhariri wa habari Simon Mkina (44) na Mchapishaji Ismail Mehboob (24) wakisomewa mashtaka hayo mapema jana.Washtakiwa hao walisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Wakili wa Serikali Paul Kadushi alidai kuwa kati ya Januari 12 na 14, mwaka huu mahali pasipofahamika jijini Dar es Salaam, washtakiwa walikula njama ya kusambaza taarifa ya uchochezi kupitia gazeti la Mawio lililokuwa na kichwa cha habari cha “Machafuko yaja Zanzibar”.

Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa Januari 14, mwaka huu, jijini Dar es Salaam,washtakiwa wote kwa lengo la kushawishi uchochezi kwa Watanzania Visiwani dhidi ya mamlaka za kisheria za serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Ilidaiwa kuwa walichapisha kwenye gazeti la Mawio toleo namba 182 la Januari 14 hadi 20, 2016 ikiwa na habari ya uchochezi yenye kichwa cha habari kisemacho ‘Machafuko yaja Zanzibar”.

Kadushi alidai katika shtaka la tatu, Januari 13, mwaka huu Jengo la Jamana lililopo Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa Mehboob, kwa lengo la kushawishi Watanzania wa Visiwani, dhidi ya mamlaka za kisheria za serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Upande wa huo wa Jamhuri ulidai katika shtaka la nne, Januari 13, mwaka huu katika Jengo la Jamana mshtakiwa Mehboob alichapisha gazeti la Mawio toleo namba 182 bila kuwa na kiapo kutoka kwa msajili wa magazeti.

Shtaka la tano, Januari 14, mwaka huu jijini Dar es Salaam, kwa makusudi na bila kuwa na mamlaka ya kisheria waliwatishia watanzania wa Visiwani, wasijitokeze kwenye Uchaguzi Mkuu wa marudio uliofanyika Machi 20, mwaka huu.

Ilidaiwa kuwa washtakiwa waliwatishia kwamba uchaguzi huo utasababisha kutokea kwa vita na machafuko utakaosababisha umwagaji wa damu kupitia makala iliyochapishwa na gazeti la Mawio yenye kichwa cha habari “Machafuko yaja Zanzibar”.

Hakimu Simba aliwataka washtakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaotoka katika taasisi zinazotambulika watakaosaini hati ya dhamana yenye thamani ya Sh. Milioni 10 kila mmoja walitimiza masharti hayo.

Wakili wa utetezi, Peter Kibatala alidai kuwa mashtaka yaliyofunguliwa dhidi ya washtakiwa hayana mashiko ya kisheria mahakama iyafute na kuwaachia huru.Alidai kuwa sheria za magazeti za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bara haziingiliani na Tanzania Visiwani hivyo kesi hiyo haina mashiko ya kisheria.

Wakili Kadushi aliomba muda wa siku saba kwa ajili ya kujibu hoja za utetezi.Hakimu alisema kesi hiyo itasikilizwa majibu ya hoja za Jamhuri Juni 28, mwaka huu na washtakiwa Lissu na Idrissa wafike mahakamani kusikilizwa mashtaka yao.
  • Mwene Said via Michuzi blog.