Maendeleo ya kesi inayowakabili Lissu na gazeti la MAWIO

MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam akikabiliwa na mashtaka ya kuchapisha taarifa za uchochezi.

Lissu alisomewa mashtaka hayo jana na kuunganishwa na wenzake, Mwandishi wa gazeti la Mawio, Jabir Idrissa, Mhariri wa gazeti hilo, Simon Mkina na mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob ambao walisomewa mashtaka yao awali.

Baada ya Lissu kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Mkazi Mkuu ,Thomas Simba, alifuta mashtaka mawili ya uchochezi kati ya matano yanayowakabili washtakiwa hao. Hakimu Simba alifuta mashtaka hayo baada ya upande wa Jamhuri kuyaondoa katika hati ya mashtaka kwa kuwa hayana kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Awali, Wakili wa Serikali, Paul Kadushi alimsomea Lissu mashtaka yake kwa kudai kuwa kati Januari 12 hadi 14, 2016 katika Jiji la Dar es Salaam, Lissu aliandika taarifa za uchochezi yenye kichwa cha habari kisemacho’ Machafuko yaja Zanzibar’.

Katika shtaka la pili linalowakabili washtakiwa wote, inadaiwa Januari 14, 2016 katika Jiji la Dar es Salaam, kwa nia ya kusababisha chuki kati ya wananchi wa Zanzibar na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, walichapisha gazeti la Mawio likiwa na habari hiyo ya uchochezi.

Aidha, inadaiwa Januari 14, 2016, Dar es Salaam, Lissu na wenzake bila ya kuwa na mamlaka yoyote, walisababisha hofu kwa wananchi wa Zanzibar kwa kuwaambia wasikubali kurudiwa kwa uchaguzi mkuu mwaka huu, kwa sababu utasababisha machafuko.

Baada ya kusomewa mashtaka, Lissu alikana kutenda kosa hilo na kuachiwa kwa dhamana. Kesi ilipotajwa kwa mara ya kwanza, Wakili wa utetezi, Peter Kibatala aliwasilisha pingamizi la awali akiiomba Mahakama iyafute mashtaka yote kwa kuwa yana mapungufu kisheria, lakini upande wa Jamhuri uliomba upewe muda kwa ajili ya kutolea ufafanuzi.

Jana Hakimu Simba alifuta mashtaka mawili baada ya wakili Kadushi, kudai kuwa wameondoa shtaka la kwanza (kula njama) na la tano (kuchapisha taarifa za uchochezi), kwa kuwa hayakuwa na kibali cha DPP.

Hata hivyo, Wakili Kibatala aliendelea kuiomba mahakama ifute mashtaka yote, yaliyobaki kwa sababu hati ya mashtaka imekosewa “hakuna sehemu iliyooneshwa kwamba makosa hayo yametendeka wapi”.

Aidha, katika Sheria ya Magazeti kuna baadhi ya vitu vimeruhusiwa na vingine havijaruhusiwa, lakini katika hati ya mashtaka hayajaorodheshwa hayo.

Alitoa mfano “katika sheria hiyo, hakuna sehemu inayokataza kuelimisha, kukosoa au kurebisha jambo endapo serikali ikikosea”.

Wakili Kibatala alidai kutokana na hati hiyo kutoeleza mambo hayo muhimu, Mahakama iyatupilie mbali mashtaka yaliyobakia kwa kuwa sheria ya magazeti haipo kwenye muungano wa Tanzania Bara na Visiwani.

Baada ya mabishano hayo, Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 11, mwaka huu atakapotoa uamuzi. [HabariLeo]

Tundu Lissu (katikati) na Mhariri wa Mawio, Simon Mkina (mwenye miwani) na mchapishaji wao Ismail Mahboob (wa tatu kutoka kushoto, mbele).
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam leo imewafutia mashitaka mawili Siomon Mkina, Mhariri wa Mawio na Jabir Idrisa, mwandishi wa gazeti hilo na Tundu Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki, anaandika Faki Sosi.

Ni katika kesi ya uchochezi iliyofunguliwa na serikali dhidi ya watu hao pamoja na mchapishaji wa gazeti la Mawio, Ismail Mahboob wa Kampuni ya Flint Graphics.

Mashitaka yaliyofutwa ni shtaka namba moja na shtaka namba tano ambapo pande zote mbili (utetezi na mashtaka) zimeridhia kufutwa kwa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Thomas Simba.

Mashtaka hayo ni kupanga njama za kufanya chapisho la uchochezi na kosa la pili ni kuwatisha wananchi wa Zanzibar kwamba, machafuko yanawaweza kutokea Zanzibar.

Awali, Poul Kadushi, Wakili wa Serikali aliiomba mahakama hiyo kuondoa shtaka namba moja na tano kutokana na kukosekana kwa idhini ya Mamlaka ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).

Peter Kibatala, Wakili wa Upande wa Washitakiwa amesema kuwa, Wakili wa Serikali amefanya busara kukubaliana na upande huo kuwa, mashtaka hayo yalikuwa na upungufu kisheria.

Hakimu Simba amefuta mashtaka hayo baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili na kwamba, watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashitaka matatu pekee.

Shitaka la pili la kuchapisha chapisho la uchochezi linawakabili Idrisa mshitakiwa namba moja, Mkina ambaye ni mshitakiwa namba mbili na Lissu, mshitakiwa namba nne.

Shitaka la tatu la kuchapisha magazeti bila ya kuwa na hati ya kiapo kutoka kwa msajili wa magazeti linamuhusu Mahboob, mshitakiwa namba tatu.

Shtaka namba nne la kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar ya kutopiga kura kwa kuhofia umwagikaji wa damu.

Hata hivyo, Kadushi amejibu hoja zilizowasilishwa mahakamani hapo na upende wa utetezi kuwa, zina kasoro.

Kadushi amedai kuwa mashitaka yote yaliyobaki katika shauri hilo yameanishwa kwa kila kosa na kifungu chake na maelezo ya kosa hilo.

Amedai kuwa, kifungu namba 32 (a), (b), na (c) cha makosa ya jinai kimeanisha kuwa, na nia ya kutenda kosa ni kosa na kutenda kosa ni kosa.

Peter Kibatala amedai kuwa, bado hoja za Kadushi hazina mashiko na kwamba, mashtaka hayo ya matatu yaliyobaki hayana mashiko kutokana na kwamba, Sheria ya magazeti haifanyi kazi Zanzibar na kuwa chapisho hilo lingeleta athari Zanzibar na sio Tanzania Bara ambapo yupo waziri husika.

Kibatara amewasilisha hoja ya kufutwa kwa mashtaka yaliyobaki kwa madai kuwa, hayana mashiko kwa mujibu wa kifungu 31(a)(b) na (c) cha sheria ya magazeti ambayo inampa haki raia kuikosoa serikali.

Kesi hiyo itatajwa tena 11 Julai mwaka huu ambapo hakimu atatoa maamuzi ya kufutwa ama kutofutwa kwa shauri hilo. [MwanaHALISI Online]

*************


MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), jana amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na kusomewa mashtaka matano, likiwamo la kuandika na kuchapisha habari za uchochezi katika gazeti la Mawio.

Akisoma mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Thomas Simba, Wakili wa Serikali, Paul Kadushi, aliwataja washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mhariri wa gazeti hilo, Simon Mkina, mchapishaji Kampuni ya Jamana na Ismail Mehboob.

Kadushi alidai mahakamani hapo kuwa Lissu na wenzake wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Januari 14 hadi 20, mwaka huu katika Jiji la Dar es Salaam, ambayo ni kinyume na sheria ya magazeti.

Alidai Lissu na wenzake wanadaiwa kuandika na kuchapisha katika gazeti hilo taarifa‎ za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho ‘Machafuko yaja Zanzibar’.

Wanadaiwa mnamo Januari 14, 2016 katika Jiji la Dar es Salaam, walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Shtaka la tatu katika kesi hiyo linamkabili mshtakiwa wa tatu, Mehboob, ambaye anadaiwa Januari 13, mwaka huu katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala, alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi.

Mshtakiwa huyo pia anadaiwa kuwa alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya kisheria ya kiapo kwa msajili wa magazeti.

“Mshtakiwa huyo na wenzake, kwa pamoja Januari 14, 2016‎, jijini Dar es Salaam, bila ya kuwa na mamlaka yoyote yale, aliwatisha na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar ili wasiweze kuingia kwenye marudio ya uchaguzi mkuu,” alidai Wakili Kadushi.

Wakili huyo, aliiomba mahakama kuondoa shtaka la kwanza na la tano kwa sababu halijaendana na sharti la kisheria baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kushindwa kutoa idhini kwa mashtaka hayo.

Kadushi pia aliiomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa kesi hiyo, kwa sababu washtakiwa wanne walikuwapo mahakamani hapo na upelelezi ulikwisha kamilika.

Katika kesi hiyo, Lissu anawakilishwa na Wakili Peter Kibatala ambaye aliunga mkono uamuzi wa upande wa Jamhuri kuondoa mashtaka hayo mawili.

Lissu alikana mashtaka hayo na Hakimu Simba alikubaliana na hoja ya upande wa Jamhuri ya kuondoa mashtaka hayo na kubakisha matatu yanayowakabili washtakiwa wote.

Hakimu Simba aliwataka washtakiwa hao kuwa na wadhamini wawili kila mmoja watakaosaini bondi ya Sh milioni 10. Walikidhi masharti hayo na kutolewa nje kwa dhamana.

Kesi hiyo imehairisha hadi Julai 11, mwaka huu itakapoendelea kusikilizwa.

NJE YA MAHAKAMA

Akizungumza nje ya mahakama jana, Lissu alisema kuwa Serikali ilimfikisha mahakamani baada ya kusema ukweli kuhusu hali halisi ya uchaguzi wa marudio Zanzibar.

Alisema kitendo hicho kimesababisha kuandikiwa mashtaka ya uchochezi ili waweze kuzibwa midomo na kushindwa kutetea haki za wanyonge ambao ni Watanzania wengi.

“Kauli yangu haikuwa ya kichochezi, bali nilikuwa naangalia mustakabali wa uchaguzi wa marudio Zanzibar, kwa sababu ilionekana kabisa haki ya wanyonge inaporwa na watu wachache, hatuwezi kuvumilia vitendo vya ukandamizaji unaoendelea kuonekana nchini, lazima tuseme,” alisema.

Alisema kumekuwa na matendo ya hovyo hovyo yanayojitokeza na kwamba wakiwa wanasema ukweli, wanafikishwa mahakamani ili washindwe kuzungumza.

“Hatutakubali, tutapambana na Serikali ndani ya mahakama na nje ya mahakama na tunaamini tutashinda,” alisema.

MBOWE NA DEMOKRASIA

Akizungumzia hali ya kisiasa nchini Dar es Salaam juzi, Mwenyekiti wa Chadema ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alisema demokrasia ipo majaribuni kutokana na uamuzi wa watawala.

Alisema kutokana na hali hiyo, taifa linapitia wakati mgumu, ikiwemo watu, vyama vya siasa kufungwa midomo pamoja na Bunge.

Mbowe aliyasema hayo katika futari iliyoandaliwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Edward Lowassa, ambayo iliwakutanisha masheikh mbalimbali wa Mkoa wa Dar es Salaam.

“Hivi sasa nchi inapita katika kipindi kigumu, Bunge, mahakama na hata Serikali vipo ‘under attack’ (chini) ya mtu mmoja ambaye akiamua kufanya lolote linakuwa. Pamoja na hali hiyo, tunajua tutapambana hivyo hivyo.

“Hata kilio cha masheikh kilichotolewa hapa kuhusu sheria kandamizi kwa kile kilichoelezwa eti ugaidi kila mtu anajua, lakini pamoja na hali hiyo, tunayachukua haya na tutayafanyia kazi, kikubwa tunawaomba Watanzania waendelee kutuunga mkono ndani na nje ya Bunge,” alisema.

Mbowe alisema kupitia umoja wa vyama vinavyounda Ukawa, hivi sasa wanajitahidi kuimba wimbo mmoja wa kuhakikisha demokrasia ya kweli inakuwepo nchini.

Alisema pamoja na misukosuko iliyopo, Ukawa wataendelea kudai demokrasia, licha ya kile alichodai hila za watawala kutaka kuwafumba midomo.

SHEIKH BUNGO

Akizungumza katika hafla hiyo kwa niaba ya masheikh wenzake, Sheikh Kondo Bungo ambaye ni mwanaharakati wa Kiislamu, alimtaka Mbowe kuhakikisha anawaunganisha wabunge na kupinga sheria kandamizi dhidi ya Waislamu.

Alisema hivi karibuni, Bunge limepitisha sheria ya ugaidi, ambayo huenda ikageuka kitanzi kwa Watanzania wengi.

Sheikh Bungo alisema kwa sasa sheria hiyo ya ugaidi inaeleza kuwa hata kama utahisiwa wewe ni gaidi utaishia gerezani bila hatia kama ilivyo kwa masheikh waliopo magerezani.

“Ninasema hata sisi wengine tuna vinyongo, hadi sasa magereza mengi yamejaa masheikh, tena wale ambao wanaonekana hawakubaliani na matakwa ya mabwana wakubwa. Wapo masheikh wetu wa Zanzibar ambao sasa ni mwaka wa tatu hakuna dhamana na haijulikani hatima ya kesi yao.

“Tupo kwenye mtanziko mkubwa, na ndugu yetu Lowassa tunakuambia hata masheikh waliokuja hapa kwa mwaliko wako, ni wale ambao hawakubalini na hali ya mambo,” alisema Sheikh Bungo. [MTANZANIA]