Magufuli atafia ufisadi, mimi nitafia demokrasia - Zitto Kabwe

MWAKA 2015 tulikwenda kwenye uchaguzi kuchagua madiwani, wabunge na Rais. Baada ya Uchaguzi kumalizika serikali mpya iliundwa pamoja na serikali za mitaa kuundwa. Baada ya uchaguzi tumeona viongozi wapya wakichukua hatua mbalimbali nzuri na mbaya, zenye kujenga na kubomoa, zenye kuimarisha demokrasia na zinazobomoa demokrasia.

Tumeshuhudia maamuzi mengine ambayo yanatia hofu kwamba ingawa tunaona dhamira ya dhati ya kupambana na ufisadi, lakini pia tunaona mbinu za chini chini za kutokomeza demokrasia ya nchi yetu ambayo tumeijenga kwa jasho na damu.

Leo nitagusia baadhi ya maeneo ambayo nadhani ni vihatarishi vya ustawi wa wananchi wetu na ambavyo lazima tuanze kuvipinga mapema sana kabla havijaota mizizi.

Baadhi ya maeneo ninayotaka kuyazungumzia leo ni wabunge kusimamishwa kazi za Bunge, maamuzi ya serikali kuhusu Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), hali ya Zanzibar, mwelekeo wa Bajeti ya Kwanza ya Serikali ya Rais John Magufuli na tishio la nchi kuelekea kwenye utawala wa imla wa MTU mmoja.

Wabunge kusimamishwa kazi

Mei 30 mwaka huu, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Naibu Spika lilipitisha Azimio la Bunge la kuwasimamisha kazi wabunge saba kwa vipindi mbalimbali. Wabunge wawili, Esther Bulaya na Tundu Lissu walisimamishwa kuhudhuria mikutano miwili ya Bunge.
Wabunge wanne; Halima Mdee, Pauline Gekul, Godbless Lema na mimi tulisimamishwa kuhudhuria mkutano mmoja –ambao ni huu unaoendelea wa bajeti na mbunge mmoja, John Heche, amesimamishwa vikao 10 vya mkutano huu wa tatu unaoendelea.

Sababu iliyoelezwa na Bunge ni kwamba wabunge hawa walifanya fujo siku ya tarehe 27 Januari 2016, kutokana na hoja niliyoitoa bungeni ya kutaka mjadala kuhusu sababu za hovyo za uongo zilizotolewa na Serikali kuhusu uamuzi wa kuzuia Shirika la Utangazaji la Taifa ( TBC ) na televisheni binafsi nyengine kuonyesha moja kwa moja mikutano ya Bunge.

Mimi binafsi pamoja na wabunge wengine sita tuliosimamishwa kwa vipindi tofauti, hatukufanya fujo yeyote ndani ya Bunge. Kosa letu kubwa ni kutaka kuhoji maamuzi ya serikali ambayo kwa maoni yetu hayana msingi wowote.

Serikali inasema ninyi wananchi hamfanyi kazi kwa sababu Bunge linaonyeshwa wakati wa kazi. Hata hivyo, serikali hiyo hiyo inatuaambia kuwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita uchumi wa Tanzania ulikua kutoka shilingi 16 mwaka 2005 mpaka shilingi trilioni 99 mwaka 2015.
Kipindi chote hiki Bunge lilikuwa linaonyeshwa moja kwa moja na televisheni za TBC na StarTV. Kama mngekuwa hamfanyi kazi, uchumi usingekua kwa kiwango hicho cha asilimia 600 ndani ya muongo mmoja wa uongozi wa Rais Jakaya Kikwete.

Utawala wa Rais Magufuli unataka kutuaminisha kuwa ukiwa na Bunge ‘live’ watu hawafanyi kazi lakini uongozi uliopita umedhihirisha kwa ushahidi kuwa ukipanua demokrasia na kuwaonyesha wananchi kila kinachoendelea bungeni, uwezo wa kazi unaongezeka na uwezo wa wananchi kuwajibisha viongozi wao unaongezeka.

Hivyo Serikali kuamua kuficha Bunge ni mbinu za kuendesha serikali kwenye giza ili kufanya maamuzi ambayo baadaye ionekane serikali tu au Rais tu ndiye mfanya kazi. Ndio maana mikutano yote ya Rais anapohutubia huonyeshwa moja kwa moja lakini sio Bunge.

Wabunge wamesimamishwa kwa sababu ya kukataa Bunge kuendeshwa kwenye giza. Wabunge waliosimamishwa walisimama kidete kuhoji sababu za serikali kufikia maamuzi hayo.
Walitaka kujua kwanini Serikali imekuwa kigeugeu kwa kubadilisha badilisha sababu zake za kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya Bunge. Wakati mmoja serikali ilisema sababu ni gharama, kama ni hivyo ni kwanini walizuia StarTV na AzamTV kuonyesha moja kwa moja?

Ni dhahiri serikali inataka kuendesha mambo yake kwa uficho kwa sababu kuna maamuzi inataka kufanya na haitaki wananchi mjue mapema maamuzi hayo. Serikali inaturudisha nyuma badala ya kwenda mbele.

Wabunge waliosimamishwa ni wabunge wenye uwezo wa kujenga hoja. Kuna wengine wamebaki bungeni wenye uwezo mkubwa tu wa kujenga hoja, lakini hawa saba waliosimamishwa ni wabunge waliojidhihirisha kwa muda mfupi kwa baadhi yao kama Heche, wanaweza kusimamia hoja zao bila woga.

Swali la kujiuliza ni hili, tukio ambalo limetokea mwezi Januari ni kwanini adhabu yake itolewe mwezi Juni –tena wiki moja tu kabla ya Waziri wa Fedha kuwasilisha bungeni Bajeti ya Serikali?
Katika waliosimamishwa, Halima Mdee ni Waziri Kivuli wa Fedha, na mimi huko nyuma niliwahi kuwa na wadhifa kama huo. Kuna nini? Nitawaeleza katika hoja ya bajeti.

Kimsingi Utawala wa Rais Magufuli umepanga kupandisha kodi za wananchi masikini na uliona uwepo wetu bungeni utatibua mipango yao. Rais na wenzake ndani ya CCM hawapendi kusikia hoja zinazowapinga, hawana uvumilivu wa kukosolewa na hivyo walipanga kuhakikisha kuwa baadhi yetu hatutakuwepo kwenye mjadala wa bajeti ili kufanikisha malengo yao ya kufanya maamuzi yatakayowandamiza wananchi.

Nitaeleza vizuri hili zaidi baadaye kwenye makala hii. Nataka Watanzania wajue kuwa kusimamishwa kwetu ni ajenda maalumu ya serikali ya Rais Magufuli kufunika mjadala wa bajeti kwa sababu anajua kuwa tunajua wanachotaka kufanya dhidi ya “walalahoi” wa nchi yetu.
Sisi hatutakaa kimya, tutatumia wenzetu waliopo bungeni kuyasema haya na pia tutazungumza na wananchi kuwaeleza pia. Tutatumia mikutano yetu mbalimbali bila kujali itikadi za vyama vyetu kuhakikisha kuwa wananchi wanajua kila kinachoendelea na kuwataka kuunganisha nguvu kukataa udikteta unaonyemelea nchi yetu.

Wanafunzi 7800 kufukuzwa Chuo Kikuu Cha Dodoma

Mmesikia sakata la wanafunzi wa UDOM waliokuwa wanasomea programu maalumu ya ualimu wa Sayansi. Hawa ni watoto wa Watanzania masikini waliokubali kuacha kwenda ‘A level’ na kukubali kusomea diploma ya Ualimu ili wakawafundishe watoto wa masikini wenzao.

Wanafunzi hawa hawakuanzisha wao program hii. Ilianzishwa na serikali na kupitishwa na Baraza la Mawaziri ambalo Rais Magufuli alikuwa mjumbe na alishiriki kikao hicho kwa mujibu wa kumbukumbu za Baraza la Mawaziri.

Rais Magufuli hakupinga mpango huu na aliubariki kama wenzake walivyofanya na kuanza kutekelezwa. Lengo la program hii ni kuondoa tatizo la walimu wa masomo ya Sayansi. Tanzania ina uhaba wa walimu wa Sayansi 26,000 na tukienda kwa utaratibu wa kawaida tutahitaji miaka 20 kuziba pengo hilo.

Program hii ilianzishwa ili kuziba pengo hili kwa muda mfupi na vijana waliitikia wito huu wa kizalendo kuhakikisha wadogo zao hawakosi walimu siku za usoni.

Serikali ya Awamu ya Tano imewafukuza vijana hawa 7800 kutoka chuoni ndani ya masaa 24 kwa makosa ambayo si yao. Sisemi kuwa program haikuwa na kosoro. Zilikuwepo ikiwemo kudahili wanafunzi wengi zaidi ya ilivyotarajiwa.

Lakini aliyedahili si watoto hawa bali ni serikali yenyewe, kwanini waadhibiwe watoto? Bunge lilipotaka kujadili hoja hii au hata kuipeleka kwenye Kamati ya Bunge kuifanyia uchunguzi na kutoa mapendekezo, Naibu Spika, Tulia Ackson, alizuia hoja ya mbunge Joshua Nasari bila sababu za msingi.

Wabunge wote, bila kujali vyama vyao, walitaka hoja ijadiliwe ili kuweza kupata majawabu. Mbona wakati wa uongozi wa awamu ya nne tulijadili hoja ya mgomo wa madaktari na kisha kupelekwa kwenye kamati husika ya bunge kupata suluhisho la kudumu?

Kwanini utawala wa Rais Magufuli hautaki Bunge lifanye kazi yake? Mbona yeye Rais kaenda kujadili jambo hilo huko Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Mlimani)?

Rais Magufuli anafikia kuita watoto wetu vilaza? Rais huyu anayesema yeye ni Rais wa masikini anaita watoto wa masikini vilaza. Vijana hawa wazalendo waliojitoa muhanga kuacha kwenda kidato cha tano ili wasome kuwa walimu na kulea kizazi kijacho Rais wao anawaita vilaza.

Rais sifa zimempanda kichwani. Rais Magufuli hana budi kuwaomba radhi vijana hawa na wazazi wao. Rais ni mwalimu, anajua madhara ya kisaikolojia kufuatia maneno aliyoyasema. Ni sawa na Jenerali wa Jeshi anayetukana askari wake walio mstari wa mbele.

Hata Baba wa Taifa hakuthubutu kamwe kuita wanafunzi vilaza hata kama walimuudhi kiasi gani. Rais Magufuli anaongea mno na hii si sawa kwa kiongozi.

Rais ajue kuweka akiba ya maneno. Yeye ni kiongozi wa wote, wenye akili na vilaza. Yeye anapaswa kuwa wa mwisho kuongea ili watu waweze kukataa rufaa kwake. Yeye akishaongea wananchi walioonewa waende kwa nani? Waende kwa Mungu?

Tunamtaka Rais awarudishe wanafunziwa UDOM mara moja na wale wanafunzi ambao itaonekana hawakuingia kwenye program kihalali waondolewe badala ya kuadhibu watoto wote kwa makosa ya wachache ambao ni asilimia tano tu ya wote.

Makosa madogo ni mambo ya kawaida katika jamii. Yeye Rais ni mfano mzuri wa hili kwani naye mbona aliteua waziri mlevi na kurekebisha kwa kumfukuza peke yake, mbona hakufukuza baraza zima la mawaziri kwa ulevi wa waziri mmoja?

Zanzibar

Mnajua mara baada ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar kufutwa chama chetu cha ACT-Wazalendo kiliweka msimamo wa wazi kwamba kinatambua ushindi wa Maalim Seif Sharif Hamad kama Rais aliyechaguliwa na Wazanzibari na anayepaswa kula kiapo na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Tuliandika pia masuala 10 muhimu kwa Rais kuyafanyia kazi na moja ya jambo tulilomtaka Rais Magufuli kufanyia kazi ni suala la demokrasia ya Zanzibar. Rais hakusikia wito wetu na aliruhusu ufutwaji usio halali kisiasa wala kisheria wa uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 25, 2015.

Nasisitiza ACT Wazalendo hakiutambui uchaguzi wa marudio wa Zanzibar uliofanyika mwezi Machi mwaka 2016 na matokeo yake yote yaliyofanyika. Kwa maana hiyo hatutambui Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Baraza la Mapinduzi la Zanzibar na hata Rais wa Zanzibar.

Hivi karibuni kumekuwa na kuongezeka kwa sintofahamu huko Zanzibar kufuatia mgombea Urais aliyeshinda na kunyang’anywa ushindi wake kwenda kwa wananchi kuzungumza nao.
Hali hii imesababisha Jeshi la Polisi kumhoji Maalim Seif na siku mbili baadaye Dk. Ali Mohammed Shein kutamka kuwa hamwogopi Maalim Seif kwa sababu hana vifaru na mizinga.

Ninalaani kauli hii ya Dk. Shein ya kutisha kwa vifaru na mizinga. Kamwe huwezi kuzima haki za wananchi kwa vifaru na mizinga. Shein akumbuke kuwa Sultan alikuwa na jeshi, vifaru na mizinga na ulinzi wa dola kubwa kama Uingereza lakini aliangushwa na wananchi wa Zanzibar mwaka 1964.
Shein akumbuke kuwa nchi kadhaa duniani zilikuwa na madikteta wenye vifaru na mizinga lakini waliondoka. Ninamtaka Shein afute kauli yake hii na kuacha vitisho badala yake aanze mchakato wa kupata maridhiano ya jamii ya Zanzibar. Hatutaki kurithi damu, tunataka kurithi nchi yenye amani, haki na demokrasia.

Ninajua hali mbaya ya kisiasa iliyopo Zanzibar na mkwamo uliopo hivi sasa. Hata hivyo ni lazima tupate jawabu kupitia sanduku la kura.

Napendekeza kuwa vyama vikuu vya siasa Zanzibar vikubali ‘kufa kidogo’ yaani ‘to die a little’ kwa vyote kukubali kuwa chaguzi za mwaka 2015 na ule wa mwaka 2016 zilizofanyika visiwani humo zote zilikuwa batili, zifutwe na Uchaguzi Mkuu mpya uitishwe.

Uchaguzi huo utanguliwe na Serikali ya Mpito itakayohusisha vyama vyote vya siasa na baadhi ya wanajamii wanaoheshimika na Wazanzibari wote ili kujenga kuaminiana. Hii itatupa nusura ya Zanzibar.

Nawaomba Wazanzibari watumie mwezi mtukufu wa Ramadhani kutafakari maoni haya na wote kwa pamoja baada ya Ramadhani kuja na jawabu ya hali ya kisiasa.

Tunatamani Zanzibari irudi kwenye hali ya kawaida na ishamiri. Zanzibar ikiingia kwenye mtafuruku, Tanzania nzima itakuwa kwenye mtafaruku. Ni dhahiri kuwa Rais Magufuli ameshindwa kutoa uongozi kwenye suala hili na hivyo ni wajibu wa Wazanzibari wenyewe kukaa na kupata mwafaka wa kijamii na kusonga mbele.

Bajeti ya 2016/17

Kuanzia Juni 8, 2016 Bunge litakuwa kwenye mjadala wa bajeti ya kwanza ya Serikali ya Rais Magufuli. Rais ameleta mapendekezo ya bajeti ya shilingi trilioni 29.5.

Katika makadirio haya, vyanzo vya ndani ni shilingi trilioni 18.5 na misaada ni shilingi trilioni 3.6. Serikali inatarajiwa kukopa jumla ya shilingi trilioni 7.4.

Mwaka 2015/16, serikali ilitarajiwa kukusanya jumla ya shilingi trilioni 13.8, hivyo ndani ya mwaka mmoja wa fedha, utawala wa Rais Magufuli unataka kukusanya shilingi 4.7 trilioni zaidi –sawa na ongezeko la asilimia 25.

Kwa ufupi ni kwamba serikali haina budi kuongeza kodi kwa kiwango cha asilimia 25 ili kuweza kutimiza malengo yake ya makusanyo.

Mtakumbuka kuwa mara baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani, tulikuwa tunaelezwa kodi iliyokusanywa kila mwezi na tuliona wafanyabiashara wakikabwa koo kwa kukwepa kodi.

Hata hivyo, ongezeko la makusanyo lilikuwa kwa miezi miwili tu ya Novemba na Desemba kwani kuanzia mwezi Januari makusanyo yalianza kuendana na hali halisi ya uchumi wa nchi yetu na ndio maana mbwembwe za makusanyo hazisikiki tena hapa nchini.

Ukweli ni kwamba Rais alikuwa anakusanya fdha ambazo hazikuwa zimekusanywa na hapakuwa na hapajakuwa na mbinu mpya za kukusanya mapato ya serikali.

Maeneo muhimu yanayopoteza mapato kama vile makampuni ya nje kutumia mbinu za kihasibu kukwepa kodi hayajatazamwa kabisa na Rais na wasaidizi wake. Hivyo, serikali imeamua kurudi kwa wanyonge kuwaminya na kodi ikianzia kuchukua kodi zote majengo kutoka kwenye halmashauri zetu.

Kodi za majengo ndio chanzo kikuu cha mapato ya Halmashauri zetu za Miji. Manispaa na Majiji. Uamuzi wa serikali kuchukua chanzo hiki cha mapato utasababisha halmashauri zetu kushindwa kuzoa taka na hata kutoa huduma kwa wananchi.

Hata hivyo, uamuzi huu inaonekana umechukuliwa kwa sababu halmashauri nyingi za miji mikubwa zinaongozwa na vyama vya upinzani kama vile Manispaa ya Kigoma Ujiji, Manispaa ya Iringa, Arusha, Ilala, Kinondoni, Mbeya Jiji na kwingineko.

Utawala wa Magufuli unataka kuhakikisha kuwa manispaa zinaoongozwa na vyama vya upinzani zinashindwa kutoa huduma. Duniani kote kodi za majengo hukusanywa na Serikali za Mitaa. Katika Bajeti ya mwaka huu kodi hizi zitaongezwa maradufu.

Serikali inatarajia kupandisha ushuru kwenye soda, vilevi na sigara pia kwa mujibu wa vitabu vya bajeti vilivyogawiwa kwa wabunge. Hata kodi kwenye gharama za kupiga simu zitaongezwa kwa zaidi ya asilimia 10.

Eneo la ushuru peke yake serikali inataka kukusanya shilingi trilioni 1.2 kutoka shilingi bilioni 900 za mwaka uliopita. Hii ni nyongeza ya shilingi 300 bilioni zaidi kutoka bajeti ya mwaka 2015/16.
Maeneo haya mawili peke yake ( kodi za majengo na ushuru wa bidhaa ) yataongezewa kodi kiwango cha kuumiza sana wananchi wa kawaida. Hii ndio sababu serikali imefukuza baadhi ya wabunge mahiri bungeni ili kulainisha upitishwaji wao wa viwango hivi vya kodi.

Hata hivyo tutatumia wabunge wenzetu waliobakia bungeni kuhakikisha kuwa kodi kwa wananchi masikini haziongezwi kiholela. Sisi tunaamini kuwa bajeti ya shilingi 29.5 trilioni ya Utawala wa Magufuli si bajeti halisi kwani makadirio yao hayazingatii ukuaji wa uchumi na yana lengo la kuchukua fedha kutoka kwa wananchi kupeleka serikalini, jambo ambalo litadidimiza uchumi wa nchi yetu.

Tishio la Demokrasia

Jambo la mwisho ambalo ninataka kuwaeleza ni tishio lililopo mbele yetu dhidi ya demokrasia ya vyama vingi. Hatua mbalimbali ambazo utawala wa Magufuli unachukua ni ishara ya kutengeneza utawala wa imla.

Rais ndiye anayejua kila kitu na ndiye anayeamua kila kitu. Hii ni hatari sana kwa nchi yetu na ni lazima kuchukua hatua mahususi kumkatalia Rais mwanzoni kabisa ili asizoee.

Nilimwunga mkono toka mwanzo katika vita dhidi ya ufisadi kwani ni vita muhimu na lazima ipiganwe bila kujali itikadi za vyama. Hakuna namna unaweza kumlaumu Rais anapochukua hatua za kusafisha uvundo katika nchi. Pasipo shaka yoyote nitaendelea kumwunga mkono katika eneo hilo.
Hata hivyo, Rais anatia hofu mno katika ujenzi wa mfumo wa uwajibikaji. Tanzania ina vyombo vya kuimarisha uwajibikaji ikiwemo Bunge na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT).

Rais anataka kupigana dhidi ya ufisadi nje ya mfumo jambo ambalo ni la hatari sana kwa nchi kwani akitoka yeye tutaanza upya. Inawezekanaje kiongozi anayepambana na rushwa akavunja nguvu ya NAOT kwa kumpunguzia bajeti Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)?

Rais amediriki hata kuvunja Katiba na Sheria ya Ukaguzi kwani bajeti ya CAG haipangwi na serikali bali hupangwa na Kamati ya Bunge. Hata hivyo Rais ameenda kinyume na sheria na badala yake kapanga mwenyewe bajeti ya CAG? Tangu lini mkaguliwa akapanga bajeti ya anayemkagua? Kamati ya Bunge ilipanga bajeti ya shilingi bilioni 69 kwa CAG lakini serikali ( mkaguliwa ) imeipiga panga mpaka shilingi bilioni 32.

Hii ni moja ya mfano dhahiri kabisa wa serikali kuanza kuvunjavunja vyombo vya uwajibikaji. Hivi sasa kuna ukosefu wa sukari nchini. Rais alisimama kwenye majukwaa ya siasa na kutoa matamko makali kwamba kuna wafanyabiashara wameficha sukari na tukaonyeshwa sukari hiyo.

Hata hivyo baada ya siku chache vyombo kama PCCB na TRA vikasema sukari ile ni halali. 
Inakuwaje Rais alitamka maneno yale bila ya kushauriana na vyombo? Ni dhahiri Rais anaongea tu na kutaka kujenga utawala wa imla. Leo bado kuna shida ya sukari na sukari ambayo serikali inasema iliagiza haionekani. Ipo wapi?

Rais alikwenda BoT na kusema nusu ya wafanyakazi pale ni hewa. Mpaka leo hatujaona hao wafanyakazi hewa wa BoT wakielezwa. Rais alikwenda tu kwa kupata maneno yasiyo na ushahidi na kutoa matamko ambayo yanashusha hadhi ya Benki Kuu lakini anashindwa kutoka mbele kusema alikosea.

Leo nataka kumwambia Rais kuwa aongoze, asitawale. Rais awe na utu na wananchi wake. Rais awe anasikiliza kwanza na kuchambua mambo kabla ya kusema chochote mbele ya hadhara.

Rais awe wa mwisho kusema ili kama kuna rufaa watoe waseme kwake. Vinginevyo Rais anataka kujenga utawala wa imla na tutamkatalia wazi wazi.

Rais amesema kuwa yeye amejitoa muhanga kupambana na ufisadi. Sisi tunalazimika kujitoa muhanga kulinda demokrasia. Ni imani yetu kuwa ufisadi utapigwa vita kikamilifu si kwa kutegemea nia ya mtu mmoja bali kwa kuboresha na kutumia misingi ya demokrasia kwa kujenga taasisi madhubuti zitakazomaliza janga la ufisadi bila ya kutegemea nia ya Rais.

Naamini kuwa ni jukumu letu kusimama na kujitoa mhanga kuzuia maafa ya kitaifa yatakayoweza kutokea kutokana na makosa ya kukandamiza demokrasia na uhuru wa mawazo kwa kuhoji, kukosoa na kurekebisha makosa hayo sasa bila kuchelewa.

Mwandishi wa makala hii ni Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini kupitia chama cha ACT-Wazalendo

Mawasiliano ya mwandishi wa makala:

Zitto Kabwe, +255-756809535, www.zittokabwe.com

Zitto Kabwe ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).