Makala kutoka Raia Mwema: Usalama siri za serikali shakani - Rais apelekewa faili

RAIS John Magufuli amepelekewa faili lenye kurasa 28 kuhusu tuhuma mbalimbali dhidi ya Idara ya Mpigachapa Mkuu wa Serikali, ambazo ni pamoja na bosi wa idara hiyo kuvujisha nyaraka za siri za serikali kwa viongozi wa juu wa moja ya vyama vikubwa vya upinzani nchini.

Katikati ya tuhuma hizo ni Mpigachapa Mkuu wa Serikali, Cassian Chibogoyo, ambaye ameshikilia wadhifa huo kwa takribani miaka 22 sasa.

Tuhuma hizo zimeandikwa na watumishi wazalendo wa Idara hiyo; katika barua yao ya Mei 05, 2016 iliyopelekwa katika Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi (Ikulu).
“Mpigachapa Mkuu wa Serikali ana uhusiano wa karibu sana na viongozi wa (kinatajwa chama cha siasa cha upinzani). Kuna siri za serikali alikuwa akizitoa kwa chama hicho. Kuna wakati tulikuwa tunashuhudia viongozi (wa chama hicho) wakija idarani kwa siri nyakati za usiku ambapo baada ya kufuatilia tuligundua kuna baadhi ya nyaraka ambazo ni top secrets za serikali Cassian Chibogoyo alikuwa akiwapatia viongozi hao,”
inaeleza sehemu ya maelezo ya barua hiyo iliyowasilishwa Ikulu dhidi Chibogoyo ambaye hata hivyo amekanusha taarifa hizo, akisema hana uhusiano na viongozi hao wa kisiasa na kwamba yeye ni mwanifu kwa serikali.

Pamoja na hayo, Chibogoyo anadaiwa kufanya ununuzi bila ya kufuata sheria za ununuzi, kuchapa siri za serikali katika kampuni binafsi na kuwa na uhusiano wenye utata na baadhi ya kampuni binafsi, hasa za uchapaji.

Katika faili hilo ambalo Raia Mwema limefanikiwa kuona nakala yake, watumishi hao wamedai kwamba, mwaka 2011, idara ilinunua mashine iliyowahi kutumika kutoka nchini Ujerumani; kinyume cha sheria ya ununuzi ya mwaka 2011 na kanuni zake za mwaka 2013.
“Mashine ilinunuliwa kama ‘used machine’ (iliyokwishakutumika) kutoka Ujerumani bila hata kufuata taratibu na sheria ya ununuzi. Ukweli ni kwamba mashine hii ilinunuliwa kama used machine kutoka nchini Ujerumani, ikiwa haina baadhi ya sehemu zake muhimu kama vile “Cutter” na “Camera”.
“Aidha, wakati mashine hii inanunuliwa, serikali ilidanganywa na Mpigachapa Mkuu wa Serikali kuwa mashine ni mpya na iko kamili, kumbe ni uongo mtupu kwani baada ya kufungwa kiwandani mashine ilishindwa kufanya kazi hadi ilipoongezwa,” ilisema sehemu ya waraka huo kwa Magufuli.
Kwa mujibu wa wafanyakazi hao, mashine hiyo hadi sasa haina risiti za manunuzi yake; japo ilinunuliwa kwa gharama za jumla ya shilingi bilioni mbili.

Kutokana na ubovu huo wa mashine hiyo, wafanyakazi hao wamedai, serikali iliingia hasara kubwa ya kuchapisha karatasi za kura katika kampuni binafsi ya YUKOS kwa vile mashine iliyotakiwa na kufanya kazi hiyo kwenye Idara ya Mpigachapa Mkuu wa Serikali ilikuwa mbovu.

Madai mengine dhidi ya Chibogoyo ambaye amebakiza miaka miwili kabla ya kustaafu kazi kwa mujibu wa sheria yanahusu suala la usiri wa siri za serikali.

Wafanyakazi walioandika kwa Magufuli wanadai kwamba nyaraka muhimu kama kiapo cha urais alichoapa Rais pamoja na mawaziri wapya, Katiba Pendekezwa na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) vyote vilichapwa nje ya idara; jambo ambalo limehatarisha siri za nchi.
“Kazi hizi nyeti zinazochapwa nje ya kiwanda cha serikali, kwa kawaida huletwa kiwandani na kufanyiwa maandalizi yote hadi kufikia hatua ya kuingizwa mitamboni.
“Lakini kwa sababu ni mibovu hupelekwa nje ya kiwanda cha serikali na kuchapwa huko kwa siri huku Katibu Mkuu akiwa amedanganywa na mpigachapa mkuu wa serikali kwamba kazi zimechapwa kiwandani,” ilisema barua hiyo.
Wafanyakazi hao pia wamemtuhumu Chibogoyo kuhusiana na kupotea kwa leseni 104 za umiliki silaha katika kitengo cha “bindery” mnamo mwaka 2011.
“ Leseni 140 zilizokuwa zimekamilika kabisa zilihifadhiwa katika “Strong Room” ya kitengo hicho zilipotea katikamazingira yenye utata bila kuvunjwa mlango au hiyo strong room.
“ Ifahamike kwamba ufunguo mmojawapo wa strong room unatunzwa na Mtunza Funguo na ufunguo mwingine unatunzwa na Mpigachapa Mkuu wa Serikali, bwana Cassian Chibogoyo,” ilisema barua hiyo.
Waraka huo unaeleza kuwa katika tukio hilo la upotevu lililotokea pasipo kuvunjwa kwa mlango, leseni 140 zilizopotea zilikuwa za katikati ingawa zilizokuwa juu na chini hazikupotea.
Mara baada ya kupata tuhuma hizi, Raia Mwema lilimtafuta na kumpata Chibogoyo ambaye alikubali kuzungumza na kueleza upande wake.
Alisema tuhuma zote zinazoelekezwa kwake zimepangwa na watu walioamua kuchafua heshima yake ya utumishi wa serikali aliyoifanyia kazi kwa zaidi ya miaka 30.
“ Wanasema mimi nimenunua mashine iliyotumika, huo ni uongo. Mimi siwezi kuamua kununua mashine kama hiyo. Kuna mchakato ni lazima ufuatwe ili idara inunue mashine.
“ Wanaohusika na kununua mashine ni Bodi ya Zabuni na kadiri ninavyofahamu zabuni ile ilitangazwa kimataifa na kampuni iliyoshinda ilitimiza vigezo na masharti yote ikiwamo hiyo sheria ya manunuzi.
“ Kimsingi mashine ile ilikuwa mpya. Brand new kabisa na hivi ninavyozungumza nawe inafanya kazi na tayari imerudisha hadi gharama za ununuzi wake. Hakuna lililokuwa na ukweli… . Hakuna utafiti.. Sheria inakataza.
“ Ni kweli kuna wakati ilipata matatizo na mtaalamu kutoka Ujerumani alipokuja, alisema tatizo lilikuwa ni fluctuation of electricity (matatizo ya umeme). Kuna wakati umeme unakuwa mkubwa na wakati mwingine mdogo. Ilitengenezwa na ikapona,” alisema.
Kuhusu kuchapisha siri za serikali nje ya idara yake, Chibogoyo alikiri kwamba zipo kazi za serikali anazozichapa nje lakini ni kwenye mazingira ya usiri mkubwa na kutokana na sababu maalumu.
“ Serikali inaweza kuniletea kazi hapa. Lakini wakasema inazihitaji hizo kazi haraka. Labda wakati huo mimi nina kazi nyingine au labda mitambo imekorofisha. Mimi siwezi kukubali kuona mambo yanaiharibikia serikali wakati nipo.
“ Ninachofanya ni kuandaa kila kitu hapa. Maandalizi yote. Nikimaliza naenda kwenye kiwanda husika na kuchapa hizo karatasi kwa ulinzi mkali. Navijua viwanda vyote vya kuchapa na uwezo wao.
“ Kuna mambo manne ya kuzingatia kabla sijakipa kiwanda kazi ya kuchapa nyaraka za siri. Kuna uwezo wake wa kufanya kazi, ubora wa kazi zake, uwezo wa kuzitunza nyaraka hizo kwa maana ya kutoziharibu na usiri uliopo. Nikijiridhisha na mambo hayo, naruhusu kuchapa.
“ Tatizo nadhani kuna watu wanataka kupewa kazi za serikali na mimi wananiona ni kikwazo. Unajua sisi tulioanza kazi enzi za Mwalimu Nyerere tunaonekana ni kikwazo kwa wengi wasiopenda watu wanaofuata taratibu. Mimi ni mkali.
“ Hapa sasa natamani nistaafu tu nikapumzike na wajukuu. Maana hii kazi ina presha nyingi. Kama ningekuwa situnzi siri, ningedumu kwenye hii ofisi kwa miaka 22? Ninaowapa kazi wanakidhi vigezo,” alisema.
Idara ya Mpigachapa Mkuu wa Serikali ni miongoni mwa idara konge za serikali, ikiwa imeanzishwa na serikali ya kikoloni mwaka 1905 na makao makuu yake ya kwanza yakiwa mkoani Tanga.