Mealezo ya ACT-Wazalendo kuhusu kauli ya Rais Magufuli ya siasa za vyama wakati huu

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli amewaonya wanasiasa wanaomchelewesha kufanya kazi ya kuwatumikia Watanzania.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo baada ya kupokea ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kutoka kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Amesema haiwezekani uchaguzi umepita na mshindi amepatikana lakini wanasiasa hao wanaendeleza siasa ilhali wananchi wanataka watumikiwe wapate maendeleo.

Rais amesema hatawavumilia viongozi wa siasa wenye lengo baya na nchi na kuwataka waweke maslahi ya Taifa mbele badala ya vyama vyao.

Amewataka kufanya siasa baada ya miaka mitano ambapo wananchi watawapima kile walichokifanya kwa muda wote huo.

Awali Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu Damian Lubuva alisema suala la Kura ya Maoni halikusitishwa kama baadhi ya watu wanavyosema bali iliahirishwa kwa kuwa wakati kura hiyo ilipotakiwa kupigwa Aprili Mwaka jana, Tume ilikuwa na jukumu kubwa la kuandaa uchaguzi Mkuu.

Kutokana na hali hiyo, Jaji Lubuva alisema Tume haikuwa na uwezo wa kubeba mambo mawili makubwa kwa wakati mmoja. Jaji Lubuva amesema kutokana na zoezi la Uchaguzi Mkuu kumalizika rasmi, Tume iko tayari kuanza mchakato wa kura ya maoni.

Kuhusu suala hilo la Kura ya Maoni, Rais Dk Magufuli amemhakikishia Jaji Lubuva kuwa serikali italiamualia mara baada ya Tume kulifikisha serikalini.


Kauli ya Rais ya Kuzuia Vyama vya Siasa Kufanya Shughuli za Siasa kwa Miaka Mitano ni Tangazo la Vita dhidi ya Demokrasia na Mfumo wa Vyama vingi Nchini.


Kauli ya Rais ya Kuzuia Vyama vya Siasa Kufanya Shughuli za Siasa kwa Miaka Mitano ni Tangazo la Vita dhidi ya Demokrasia na Mfumo wa Vyama vingi Nchini

Tumepokea kwa MSHTUKO na masikitiko makubwa kauli ya Rais kwamba vyama vya siasa havipaswi kufanya siasa isipokuwa wakati wa Kampeni na kupitia bungeni. Kimsingi kauli ya Rais ni kauli yenye nia ya kuvunja Sheria ya Vyama vya siasa inayolinda uwepo wa mfumo wa vyama vingi na kuhimiza vya vya siasa kufanya shughuli za siasa katika msimu wote ili kuthibitisha uhai wao.

Tunaichukulia kauli ya Rais kama tangazo la vita dhidi ya demokrasia na uhai wa vyama vingi nchini. Chama chetu kitaitisha vikao vya dharura kujadili hali ya siasa nchini na namna ya kukabiliana na mashambulizi yanayoendelea dhidi ya demokrasia nchini mwetu.

Tunatoa wito kwa vyama vyote vya siasa vinavyoamini katika misingi ya demokrasia nchini kukutana haraka na kujadili namna ya kuunganisha nguvu pamoja katika kupigana vita mpya ya kulinda demokrasia nchini mwetu.

Aidha, tunatoa wito kwa wananchi wote na taasisi za kiraia kusimama imara katika kulinda demokrasia. Tunasisitiza kuwa ushahidi wa kisayansi duniani kote unaonyesha kuwa huwezi kuua demokrasia bila kuua juhudi za maendeleo. Tusiruhusu mtu yeyote mwenye mamlaka kuua demokrasia nchini mwetu.Hatua zozote za kuua demokrasia ni kuua Umoja, Amani na Mshikamano wa wananchi na Taifa, ambayo ndiyo misingi ya maendeleo ya nchi yetu kijamii, kisiasa na kiuchumi. Tunatoa wito kwa wananchi wote kushikamana na kusimama imara katika kipindi hiki kigumu ili kulinda demokrasia.

Zitto Kabwe, MB
Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo
Alhamisi, 23 Juni 2016.