Maoni ya viongozi CUF kuhusu ombi la Prof. Lipumba la kurejea katika uongozi wa chama

Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui amesema aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba hawezi kuwa na nia njema ya kukijenga chama hicho endapo atarudishwa kwenye nafasi aliyoikataa.

“Anataka kuja kukiharibu chama,” alisema Mazrui. Alifafanua kuwa tayari chama hicho kimefanya mambo mengi bila Lipumba ambaye alikuwa anaona kila kinachoendelea, hivyo alichokisema hakina mashiko kwani CUF ilisharidhia kuitisha mkutano wa uchaguzi kujaza hiyo.

Akieleza sababu alizozitoa mwenyekiti huyo, Mazrui alisema haoni chochote cha maana. “Sababu zilizomuondoa zingalipo. Kinachomrudisha ni nini?” alihoji naibu katibu mkuu huyo.

Alisisitiza kuwa Wazanzibari wanaendelea na mchakato wa kuidai haki yao iliyoporwa Oktoba 25 na hawana nafasi ya kushughulika na masuala yasiyokuwa na tija kwao, hivyo haoni kama kuna sababu ya kumjadili Lipumba na nafasi yake badala ya kuendelea pale walipo.

“CCM wanaona kinachoendelea, hivyo wameona wamtumie Lipumba kuja kuharibu mipango yetu. Hatuna muda wa kumjadili.Tunataka haki iliyoporwa,” alisisitiza.

Msimamo wa Mazrui haukutofautiana sana na ule wa Kaimu Mwenyekiti wa chama hicho, Twaha Taslima aliyebainisha kuwa amesikia taarifa za kurudi kwa Profesa Lipumba, lakini haoni uwezekano huo.

“Katiba hairuhusu hilo.Hakuna kifungu kinachotoa nafasi kwa kiongozi aliyejiuzulu kurudi kwenye nafasi yake pindi atakapotaka kufanya hivyo,” alisema Taslima.

Aliielezea Ibara ya 117 (2) iliyotumiwa na Profesa huyo kuandika barua ya kutengua uamuzi wake, kuwa inatoa tafsiri zaidi ya moja hivyo kuwapo haja ya viongozi kukutana na kujadili suala hilo kabla ya kutoa maamuzi.

Kwa kuwa hakuwapo kwenye mkutano huo, Taslima alisema: “Tunahitaji kukutana haraka na kujadili. Tutafanya mkutano wetu na tutavijulisha vyombo vya habari ndani ya wiki hii.”

Taslima alisema kipindi alichoongoza kilikuwa na changamoto nyingi ambazo ni tofauti na sasa, hivyo haoni haja ya mtu mwingine kuja wakati mambo yametulia. Chama hicho kilipanga kufanya uchaguzi wa kuziba nafasi hiyo Agosti mwaka huu.

Baada ya kung’atuka kwa Lipumba, Taslima alichukua mikoba yake na kukivusha chama hicho kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana, pamoja na ule wa Zanzibar ambao uliahirishwa na chama hicho kususia marudio yake Machi 20 mwaka huu.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa chama hicho, Abdul Kambaya alisema upo uwezekano wa Lipumba kurudi kwenye nafasi yake kwasababu mpaka sasa haijazibwa.

“Mwenyekiti huchaguliwa au kutenguliwa na halmashauri kuu. Haikupitisha kujizulu. Barua ya kujiuzulu itaenda pamoja na hii ya kutengua uamuzi wa awali,” alisema Kambaya.

Kauli za viongozi hao, zimekuja muda mfupi baada ya Profesa Lipumba kutangaza nia hiyo jana kwenye ofisi za makao makuu ya chama hicho, Buguruni huku akibainisha kuwa amefanya hivyo baada ya kuombwa na viongozi wa dini, wa chama na wanachama wa CUF.

Jana, wakati anatangaza kufanya mabadiliko ya kile alichokiamua miezi 10 iliyopita, hakuruhusu maswali, ila alifafanua kile kitakachofuata baada ya kuwasilisha ombi hilo, kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho: “Katibu Mkuu anashauriana na wanasheria kabla suala langu halijapelekwa kwenye halmashauri kuu kama katiba inavyosema,” alisema Profesa Lipumba.
  • via GPL