M/Kiti CHADEMA amtaja Afisa Usalama akimtuhumu kuteka na kumpiga

AFISA Usalama wa Taifa wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Peter Tewele anadaiwa kumteka, Mwenyekiti wa CHADEMA Kata ya Sola wilayani humo Natalis Mataba(62) kisha kumpiga, kumtesa na kumtelekeza porini katika wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.

Tukio hilo linadaiwa kutokea juzi majira ya saa 2:30 asubuhi katika ofisi za Usalama wa Taifa wilayani humo zilizoko katika kata hiyo, ambapo chanzo kinaelezwa kuwa mwenyekiti huyo amekuwa akiwatukana.

Akizungumza na Waandishi wa habari akiwa hospitali ya wilaya akipatiwa matibabu, Mataba alisema kuwa Afisa huyo alifika nyumbani kwake majira ya saa 2:30 asubuhi akiwa ameambatana na mlinzi wa ofisi hiyo na kumtaka waongozane naye ofisini.

“Nilipofika ndani ya Ofisi hiyo Ofisa Usalama huyo wa wilaya alinieleza ya kuwa hii ni ofisi ya Usalama na siyo ya CHADEMA na kisha wakanipeleka kwenye moja ya vyumba vilivyoko ndani ya ofisi hiyo ambacho kina giza na kisha kuniamuru nilale kifudifudi na ndipo walipoanza kunipiga ngumi na mateke”alisema.


Alisema kuwa baada ya kipigo hicho walimfunga kamba miguu na mikono huku kichwani wakimvalisha mfuko wa sandalusi ambapo walimtoa nje na kumuingiza katika gari dogo na kuondoka naye kwa kasi huku kukiwa na vijana wawili ndani ya gari hilo wakiwa wamemkandamiza kichwa chini.

“…walinipiga sana huku nikiwa nimefungwa kamba mikono hadi nikapoteza fahamu na baada ya kuona nimepoteza fahamu walinivua mfuko wa plastiki waliokuwa wamevalisha usoni kisha kunitupa katika moja ya pori ambalo sikulitambua na baadaye waliondoka,” alisema Mataba

Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ambaye pia ni Mkuu wa wilaya Rosemary Kirigini alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo alikiri kupokea taarifa za Kiongozi huyo kutekwa na mfanyakazi wa serikali.

Kirigini alieleza kuwa hatua mbalimbali zikiwemo za uchunguzi zinaendelea, huku akibainisha kuwa ameshangazwa kusikia Afisa huyo akifanya jambo hilo wakati anafahamu taratibu za kisheria kwa mtu aliyekosea.