M/Kiti CHADEMA (T), viongozi BAVICHA wakamatwa; ACT-Wazalendo yazungumzia kusakwa Zitto, mkutano kufutwa

Polisi imemshikilia kwa saa mbili Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe mkoani Mwanza.

Jeshi hilo lilizuia mkutano wa hadhara wa CHADEMA uliokuwa ufanyike wiki iliyopita mjini Kahama ambako lilitumia mabomu ya machozi kuwatawanya wanachama na wafuasi wa chama hicho, katika kile kilichoelezwa kulikuwa na dalili za uvunjifu wa amani.

Jeshi hilo pia lilizuia msafara wa viongozi wa chama hicho kuingia katika ofisi zake za Shinyanga walipokuwa wakielekea Mwanza.

Taarifa iliyotolewa jana na msemaji wa chama hicho, Tumaini Makene ilieleza kuwa mbali na Mbowe, jeshi hilo pia lilikuwa linawashikilia Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHAa), Patrobas Katambi na Katibu Mkuu wa BAVICHA, Julius Mwita.

Wengine ni Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka na viongozi wengine na wanachama wa chama hicho waliokuwa wanashikiliwa katika kituo cha Polisi Nyakato, jijini Mwanza.

Makene alisema tangu asubuhi ya jana, Mbowe na viongozi wenzake walikuwa wakizunguka katika maeneo kadhaa ya jijini Mwanza kuwasalimia wananchi katika ‘vijiwe’ mbalimbali kabla hawajakamatwa.

Alisema, “Hadi sasa (saa 11 jioni) hakuna maelezo ya kushikiliwa kwao.”

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alithibitisha kukamatwa kwa viongozi hao na kubainisha kuwa waliachiwa bila kufunguliwa kesi yoyote.

“Walikutwa Igoma Sokoni wakizungumza na wananchi. Mikutano ya namna hii imezuiwa. Wamefungua kesi mahakamani, hivyo hakuna haja ya kufanya tofauti mpaka itakapohukumiwa,” alisema Msangi.

Alifafanua kuwa jeshi hilo halina uhasama wowote na CHADEMA au chama kingine chochote na“hatuwezi kukiingilia kinapofanya mikutano yake ya ndani au hotelini. Kilichozuiwa ni mikutano ya hadhara.”

Wakati Msangi akisema hayo, kongamano la ACT Wazalendo ambalo lilitakiwa lifanyike jana kuanzia saa 7:00 mchana kwenye Ukumbi wa Jengo la LAPF; Millennium Towers, Kijitonyama lilizuiwa na polisi.

Tangu mapema asubuhi, askari polisi walitanda katika eneo la ukumbi huo kuzuia kongomano hilo.

Ukumbini hapo, waandaaji walisema hakuna anayeruhusiwa kuingia kwani wamepewa maelezo ya kuufunga baada ya tukio lililoandaliwa kuahirishwa.

Zaidi ya viti 210 vilikuwa vimepangwa kwa ajili ya kongamano hilo na mmoja wa viongozi wa ukumbi huo alionekana akiondoa mabango yaliyokuwa yanautambulisha mkutano huo wa ACT.

Viongozi watatu wa ukumbi huo walikataa kueleza kinagaubaga juu ya sakata hilo, lakini taarifa za jumla zilisema mkutano umezuiwa.

Mmoja wa watumishi wa ukumbi huo, alisema: “Tuliandaa kila kitu, ila shughuli imeahirishwa. Ukumbi unatakiwa kufungwa. Hautatumika kwa leo.”

Ilipofika saa 5:00 asubuhi, Msemaji wa ACT-Wazalendo, Abdallah Khamis alisema chama kinafanya mkutano wa dharura kwenye ofisi zake za makao makuu na baadaye kingezungumza na waandishi wa habari.

Saa 8:00 mchana, Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Anna Mghwira akiwa na viongozi wenzake, isipokuwa Kiongozi wa Chama, Zitto Kabwe alikuwa mbele ya kamera za wanahabari akifafanua kilichotokea kwa wanachama, wafuasi wa chama hicho na Watanzania kwa ujumla.

Alisema ilipotimu saa 4:00 asubuhi walipewa taarifa na mwenye ukumbi kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni limemjulisha kuwa chama hicho hakina kibali cha kuendesha kongamano hilo na kwamba kisiruhusiwe kufanya hivyo.

“Huku ni kufifisha demokrasia. Wapigania haki za kiraia wasimame imara na vyama vya upinzani katika kuilinda,” alisema Mghwira.

Wakati kongamano hilo likizuiwa, kuna taarifa za kukanganya juu ya alipo Zitto baada ya kudaiwa alikuwa anasakwa na polisi tangu juzi.

Taarifa hizo zinakuja siku chache baada ya kiongozi huyo kuitwa Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam na kuhojiwa juu ya kauli alizozitoa kwenye mkutano wa hadhara zinazokosoa utendaji wa Serikali na kupinga matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar.

Baadaye jioni, Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Msafiri Mtemelwa alitoa taarifa kuwa Zitto ametoweka na hajulikani alipo. Hiyo ilikuwa ni baada ya askari kanzu kumtafuta kwa muda kwa saa kadhaa.

“Zitto amekuwa akitafutwa kwa muda mrefu. Askari wanalinda nyumbani kwake tangu jana (juzi) usiku. Hivi sasa ametoweka, hatujui alipo. Lolote litakalompata, Jeshi la Polisi litajibu,” alisema Mtemelwa.

Awali, Mghwira alipoulizwa imekuwaje kuhusu Zitto alijibu kuwa mkutano ulikuwa wa dharura ndiyo maana viongozi wote hawakuwapo.
****************

WAKATI Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, akikamatwa na kuhojiwa na polisi, Kiongozi Mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amejikuta akikwama kujadili bajeti katika kongamano lililoandaliwa na chama hicho jijini Dar es Salaam, baada ya ukumbi kuzingirwa na polisi.

Viongozi hao wakuu wa vyama vya upinzani, walijikuta katika hali hiyo mahali na kwa nyakati tofauti jana.

Mbowe alikamatwa na polisi jijini Mwanza, akiwa na baadhi ya viongozi wa Kanda ya Ziwa na wanachama wakati akizungumza katika ‘vijiwe’ vya chama hicho huku Zitto, akipigwa `stop' kujadili bajeti kwenye kongamano lililoandaliwa na chama chake jijini Dar es Salaam.

Mbowe akizungumza na Nipashe jana, alisema kukamatwa kwake kunaonyesha polisi wanavyoleta utawala wa kutisha wananchi ili wawe na hofu.

“Polisi wasilete utawala wa kutisha wananchi. Viongozi ni wajibu wao kuzungumza na wananchi ili kufahamu matatizo yao pamoja na kuimarisha chama,” alisema Mbowe.

Alisema baada ya kutembelea ‘vijiwe’ vya chama hicho vilivyoko Nyegezi, Mkuyuni Sokoni, Butimba, Sahara na Igoma ili kuzungumza na viongozi wa matawi katika mkutano wa ndani, alishangazwa kuona polisi wanamganda kama luba.

Mbowe alisema baada ya kukamatwa maeneo ya Igoma, alifikishwa katika Kituo kidogo cha Polisi Igoma na kuchukuliwa maelezo akiwa na viongozi wengine wa chama hicho, kisha kuachiwa huku akitakiwa kutoa taarifa mahali popote anapotaka kwenda.

“Hata nikitaka kwenda kununua machungwa, wanataka niwape taarifa. Huu utawala gani wa kuwatisha wananchi…mimi ni kiongozi ambaye ni haki yangu kuzungumza na wanachama wangu kwenye matawi yao,” alisema Mbowe kwa uchungu.

Naye Ofisa Opereseheni wa chama hicho Kanda ya Ziwa, Njugu Tungaraza, alisema jana saa 10:00 jioni wakiwa ‘kijiwe’ cha Igoma, walikamatwa na polisi baada ya kufuatiliwa kuanzia Butimba Kambarage kisha Sahara.

Tungaraza alisema baada ya kukamatwa, walihojiwa na polisi wakiongozwa na Ofisa Upelelezi wa makosa ya Jinai (RCO) wa mkoa huo.

Viongozi wengine waliokamatwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Patrobass Katambi, Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka, Peter Makele (Mwenyekiti Kanda ya Ziwa), mwanasheria wa chama hicho, John Mallya na viongozi wengine na walinzi wa chama hicho, Red Brigade

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alipopigiwa simu mara mbili na Nipashe, iliita bila kupokewa. Hata alipoandikiwa ujumbe mfupi wa maandishi juu ya kuwapo kwa tukio hilo, hakujibu chochote.

Kwa upande wa Zitto, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam lilimzuia kujadili hotuba ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2016/17 kama ilivyowasilishwa bungeni mjini Dodoma Jumatano iliyopita na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango.

ACT-Wazalendo, iliandaa kongamano kwa lengo la kuichambua bajeti hiyo baada ya Zitto pamoja ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini, kuondolewa bungeni.

Wiki iliyopita, Zitto alihojiwa na Jeshi la Polisi kwa zaidi ya saa tatu kwa kile kilichodaiwa hotuba aliyoitoa katika viwanja vya Mbagala Zakhem wilayani Temeke Juni 5, mwaka huu.

Jana, chama hicho kilitarajia kufanya kongamano lake katika moja ya ukumbi wa jijini Dar es Salaam, lakini hakikufanya hivyo baada ya polisi kutanda nje ya ukumbi huo tangu asubuhi kwa kile kilichotafsiriwa ni kuzuia kufanyika kwa kongamano hilo.

Nipashe lilifika katika ukumbi huo na kuwaona askari wawili wakiwa nje wakifanya doria, huku vijana wawili waliovalia nguo za kiraia, wakiwaambia waalikwa waliokuwa wanakwenda katika kongamano hilo kuwa halipo.

“Mnakwenda wapi? Kama mnakwenda kwenye kongamano, halipo,” alieleza mmoja wa vijana aliyekuwa akienda kwa ajili ya kongamano hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Anna Mghwira, alisema walipewa taarifa na mwenye ukumbi waliopanga kufanyia kongamano hilo kwamba Polisi walikuwa wametanda katika eneo hilo tangu saa 12:00 asubuhi.

Mghwira alisema ilipofika saa 4:00 asubuhi, mmiliki wa ukumbi huo, aliwataarifu rasmi kuwa walipewa taarifa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni kuwa ACT hawana kibali cha kufanya kongamano hilo.

“Tulipewa taarifa na mwenye ukumbi kuwa Jeshi la Polisi limezuia kufanyika kwa kongamano hilo, na Polisi walimwambia mmliki wa ukumbi huo kuwa endapo ataturuhusu tufanye kongamano hilo, watawafungia kufanya biashara,” alisema Mghwira.

Hata hivyo, Mghwira alisema kitendo hicho wanakitafsiri ni mwendelezo wa hatua za uhakika kwa Jeshi la Polisi kufifisha demokrasia nchini.

Mghwira alitoa wito kwa wananchi na wapigania haki za kiraia, kusimama imara sambamba na vyama vya upinzani katika kulinda demokrasia.

“Juhudi za kupambana na ufisadi nchini haziwezi kufanikiwa bila kulinda msingi ya demokrasia. Demokrasia ndiyo msingi imara wa mapambano dhidi ya ufisadi,” alisema Mghwira.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge na Serikali ya mtaa wa ACT-Wazalendo, Yeremia Maganja, alisema waliwasiliana na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro, ambaye aliwajibu kuwa hakuwa na taarifa ya kongamano hilo.

Alisema waliwasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Christopher Fuime, ambaye aliwajibu kuwa hawezi kulizungumzia suala hilo na wamtafute Kamanda Sirro.

ALICHOTAKA KUZUNGUMZA ZITTO 

Katika nakala ambazo ACT waliwapatia waandishi zikimnukuu Kiongozi wa ACT, Zitto alisema bajeti ya mwaka 2016/17 haitatatua kero ya ajira nchini na badala yake itasababisha Watanzania wengi zaidi kukosa ajira kwa waajiri kupunguza wafanyakazi ili kubana matumizi.

Alisema hali itakuwa mbaya zaidi kwa wenye mahoteli na miji kama Arusha itaumia zaidi kwa kuwa inategemea mno biashara ya utalii.

Kuhusu Viwanda, Zitto alisema ni jambo la kupongeza kwa sababu bajeti imelenga kuondoa changamoto ya miundombinu.

Hata hivyo, alisema inawezekana uwekezaji kwenye viwanda ukakumbwa na changamoto ya soko kutoka na serikali kubana matumizi na hivyo wananchi hawatakuwa na fedha za kutumia kununua bidhaaa na huduma.

Zitto alisema serikali imepandisha kodi kwenye bidhaa kutoka nje na ushuru, hali aliyoielezea kuwa itasababisha bei ya bidhaa na huduma kupanda na kusababisha mfumuko wa bei.
  • via NIPASHE