Loading...
Friday

M/Kiti, Katibu Afya, Mhasibu, Mratibu Chanjo, Mganga Mkuu, Mhazini wasimamishwa wakituhumiwa kuihujumu CHF

BARAZA la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, mkoani Tabora limewasimamisha kazi watumishi watano kwa tuhuma za ubadhirifu wa zaidi ya Sh milioni 190, ambazo ni fedha za Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) pamoja na fedha za chanjo.

Watumishi hao wanatuhumiwa kughushi nyaraka, kukosekana kwa baadhi ya nyaraka za fedha, kuidhinisha malipo hewa pamoja na kukiuka taratibu na kanuni za utumishi wa umma na kukiuka matumizi ya fedha za umma.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Kiwelle Bundala. Kiwelle aliwataja watumishi waliosimamishwa kazi kupisha uchunguzi kuwa ni Katibu wa Afya Wilaya, Kisasu Sikalwanda, Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya, Denins Gombeye, Mratibu wa Chanjo wa Wilaya, Joel Mjondela, Mganga Mkuu Hospitali ya Wilaya, Emmanuel Mihayo na Mweka Hazina, Stanslaus Kalokola.

Alisema uchunguzi utakapofanyika na kubaini watumishi hao hawana hatia wataendelea na kazi na ikiwa tofauti hatua nyingine za kinidhamu zitachukuliwa.

Mwanri alilipongeza baraza hilo kwa kuchukua maamuzi magumu ya kulinda maslahi ya wananchi na kuongeza kuwa ataendelea kusimamia sheria na taratibu za utumishi wa umma. Aliwataka watumishi wa Serikali kuhakikisha wanasimama katika nafasi zao za kufanya kazi kwa uandilifu na kuepuka ubadhirifu ambao hauna faida ndani yake.

Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mkoa wa Tabora, Mohamed Msangi alisema sababu za watumishi hao kusimamishwa kazi ni kughushi nyaraka za malipo, kukosekana kwa baadhi ya nyaraka pamoja na kufanya malipo hewa.

Alisema taarifa ya CAG inaonesha kukiuka taratibu nyingi za matumizi ya fedha za umma.
 
Toggle Footer
TOP