Nasaha Islam: Mwezi wa Ramadhan
Kila inapofika mwezi wa Tisa kwenye karenda ya Kiislam (hijria), Waislam ulimwengu mzima uingia kwenye mfungo wa Ramadhani.

Huu ni mwezi ambao, tumefaradhishiwa Swaum na MwenyeziMungu kama tunavyosoma kwenye aya hii:

"Enyi mlioamini mmelazimishwa kufunga (swaumu) kama walivyolazimishwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu".
(Qur'an Surat Baqara [2]:183).

Wengi wetu tunaposoma Ayat (Maneno Matukufu) kutoka kwenye Qur'an, tunakuwa si wenye kuzitafakari kwa kina, kwa mfano ayah niliyoinukuu hapo tunaweza kuigawa kwenye mafungu matatu.

Kwanza kabisa, kufunga ni amri wala si jambo la hiari. Pili, kufunga Ramadhani kunatupatia faida kadhaa za kiafya na Kiiman. Tatu, kwa kuitekeleza amri hii, tutakuwa tumefikia lengo la kuumbwa kwentu nalo si lingine ila ni lile lengo lililotajwa kwenye surat Adh-Dhaariyaat aya ya 56:

"Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi"
(Qur'an Surat Adh-Dhaariyaat [51]:56)

Je MwenyeziMungu (s.w.t) anatutaka tumuabudu katika mwezi wa Ramadhani tu? Je, hii ina maana kuwa katika miezi mingine ya mwaka hatutakiwi kumuabudu/kumtii MwenyeziMungu (swt) Kikamilifu?

Swali ili ukimuuliza Muislamu yoyote atakujibu kuwa lah, miezi yote tunatakiwa kumuabudu MwenyeziMungu (swt) sawa kama ulivyo mwezi huu.

Ni kweli kabisa tunatakiwa kumuabudu/kumacha MwenyeziMungu (swt) kwa masaa yote 24 ya kila siku na katika kila kipengele cha maisha yetu kwa mwaka mzima. Pili tunatakiwa kumcha MwenyeziMungu kwa juhudi zetu zote hata mauti yatukute tukiwa Waislamu wa kweli.

Lakini ajabu ya Waislam sisi, tunakwenda kinyume na maneno ya MwenyeziMungu (swt), nasema hivyo kwa sababu wengi wetu katika mwezi huu wa Ramadhani, tunakuwa ni Waislamu wa kweli na wenye kupenda kheri nyingi.

Ndio utaona wenye kupenda masi kama vile kunywa pombe, Uasherati na maasi mengine mwezi huu, wanapumzika, nasema wanapumzika na si kuacha kwa sababu mwezi unapoisha tu wanarejea kule kule kwenye maasi.

Wanasahau kuwa MwenyeziMungu anatutaka tuwe wachamungu mpaka mwisho wa uhai wetu, kama tunavyosoma kwenye ayah hii kutoka Surat Al I'Mran.

"Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu kama ipasavyo kumcha; wala msife ila nanyi ni Waislamu."
(Qur'an Surat Al I'Mran [3]:102)

Na katika kumtii MwenyeziMungu tunatakiwa tusichague baadhi ya mambo na kuacha mengineyo, bali, ni kufuata amri zote au kwa maneno mengine ni kutii kila kipengele kilichopo katika maisha yetu.

"Enyi mlioamini! Ingieni katika hukumu za Uislamu zote, wala msifuate nyayo za shetani; kwa hakika yeye kwenu ni adui dhahiri"
(Qur'an Surat Baqara [2]:208)

Kama utaratibu wa kumuabudu MwenyeziMungu (swt) ndio huu, inakuwaje Allah (swt) atuamrishe kufunga Ramadhani ili tupate kuwa wachamungu? Kuna hekima gani katika mwezi wa Ramadhani tofauti na miezi mingine?

Jawabu ni kuwa, katika mwezi wa Ramadhani tunapewa/kutunukiwa nafasi ya pekee. Nafasi ambayo kama tutaitumia ipasavyo itatusaidia kulifikia lengo la kuumbwa kwetu kwa urahisi zaidi. Kuhusu kheri zinazopatikana ndani ya mwezi wa Ramadhani, Nabii Muhammad (s.a.w.) anasema:

"Mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa MwenyeziMungu (swt) ambao ameujaza Rehma, Baraka na Msamaha".

Na pia ni ukweli usio na shaka kuwa, kwa kutokuzingatia taratibu za mwezi wa Ramadhani tutakuwa ni wenye kuipoteza tunu hii, hivyo, kwa wenye hasara kubwa duniani na akhera.

Mwezi wa Ramadhani unatupa nafasi ya kuanza maisha mapya na kujiwekea malengo bora zaidi kwa mwaka ujao. Endapo utakuwa umebahatika kuifahamu tunu hii na kuitekeleza ni kheri kwako. Endelea na ongeza juhudi. Na endapo utakuwa huifahamu tunu hii, basi hujachelewa bado, wakati ni huu; utumie na usiupoteze.

Tujiwekee malengo la kutekeleza ibada za ziada (sunnah) zilizotushinda mwaka uliopita, pia tujiwekee malengo ya kutekeleza majukumu muhimu maishani kwa mwaka unaofuata.

Tujiwekee nia ya kutorudia tena kwenye maasi. Mtume wa Allah (swt) amesema:

"Yeyote anayedhamiria kufanya jambo jema lakini hakufanikiwa kulifanya, anaandikiwa malipo (kama aliyefanya).
(Bukhari na Muslim).

Lakini hii haina maana kuwa kazi yetu ni kuweka niya bila kutekeleza ahadi na nia, la jitahada zinatakiwa na pale tutakapokwama kutekeleza kile tulicho dhamilia ndipo tutakapo lipwa kama vile tumefanya na si kinyume chake.

Kama vile tunavyoishi na kukaa nao vema Ndugu, Marafiki, Jamaa na majirani kwenye mwezi huu wa Ramadhani basi hata mwezi huu utakapoisha, tunapaswa kuishi vilevile kama tulivyoishi nao kwa wema kwenye miezi mingine kumi na moja na si kinyume chake.

Pamoja na swala, kufunga Ramadhani Uislamu unahusika na jukumu la kuiendesha jamii kisiasa, kiuchumi kwa kuchunga mipaka ya MwenyeziMungu (swt) na kila nyanja ya maisha.

Kwa kifupi maisha haya tunayoishi mwezi huu wa Ramadhani ndio hivi tunavyopaswa kuishi hata miezi Mingine kwa kutekeleza yale yote yanayomfurahisha MwenyeziMungu (swt); na tujiepushe kabisa na yote yasiyompendeza Allah (swt).