Loading...
Thursday

Niwatake wafuasi wa CUF wasisite na waendelee na kasi hiyo hiyo ya mgomo baridi - Maalim Seif


MVUTANO mkubwa wa kisiasa uliyoikumba Zanzibar kuhu majemedari wawili wakuu wa vyama vyenye ushindani mkubwa wa kisiasa visiwani hapa, kutoka Chama cha Wananchi (CUF) na Chama Cha Mapinduzi (CCM)

Kila mmoja kwa nafasi yake kujigamba na kuwahakikishia wananchi kuwa ndie rais wa Zanzibar, kunaviweka visiwa hivi njiapanda.

Njiapanda kwenye uchumi, kwenye amani, umoja na mshikamano; japo kutaja kwa uchache.

Mvutano huo umeibuka tangu Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kufuta uchaguzi wa Oktoba 25, 2015 kutokana na sababu mbalimbali walizozieleza na kufanyika kwa uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20, mwaka huu ambao CUF waliususia na wamesisitiza kutoutambua.

Majemedari hao ni Dk. Ali Mohamed Shein aliyetangazwa na ZEC kuwa ndie mshindi kwa kupata asilimia 91 ya kura katika Uchaguzi wa Machi 20 na Maalim Seif Sharif Hamad ambaye anaamini kuwa alishinda kwenye uchaguzi wa Oktoba 25, uliofutwa.

MAALIM SEIF

Maalim Seif Sharif Hamad, anaendelea kusisitiza kwamba yeye ndiye rais halali wa Zanzibar kwa mujibu wa uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana.

Msimamo huo wa Maalim Seif umemfikisha kwenye vyombo vya dola na hivi karibuni alivyohojiwa na Jeshi la Polisi Maalim Seif, aliliambia jeshi hilo, kwamba yeye na chama chake hawaitambui Serikali iliyoko madarakani ambayo inaongozwa na Dk. Shein.

Katika mahojiano hayo yaliyochukua saa tatu kati yake na Jeshi hilo, Maalim Seif, aliulizwa na jopo la maofisa 12 wa polisi, sababu za kutomtambua Rais Dk. Shein na badala yake kujitangaza kwa umma yeye ndiye rais wa Zanzibar; lakini yeye alishikilia msimamo kuwa hamtambui.

Maalim Seif alishikilia msimamo wake huo na kwamba hakemei kitendo cha wafuasi wa CUF kumtambua kuwa yeye ndiye rais, akisema huo ndio ukweli na kwamba wananchi wanatambua hivyo.

“Uchaguzi tunaoutambua ulikuwa huru na wa haki ni ule wa Oktoba 25, mwaka jana na si vyinginevyo na kwamba hadi matokeo yake yalipofutwa, mimi ndio niliyokuwa nikiongoza kwa kura nyingi,”alisema Maalim Seif katika mahojiano hayo.

Msimamo huo umekuwa jinai kiasi cha sasa Maalim Seif kushtakiwa kwa makosa ya uchochezi ikiwamo kujiita rais wa Zanzibar chini ya kifungu cha 45 sheria ya jinai ya Zanzibar.

Pamoja na kuonekana mchochezi, Maalim Seif amelihakikishia jeshi la polisi kuwa yeye na chama chake hawana dhamira ya kumdhuru Dk. Shein bali wanatumia ulingo wa siasa kufikia malengo yao ya kushika dola ili achie madaraka.

Katibu Mkuu huyo ambaye pia ni Makamu wa kwanza Mstaafu wa Zanzibar, alisema kuwa njia pekee ya kumwondoa Dk. Ali Mohamed Shein, madarakani ni kuendelea na mgomo baridi.

Anasema mataifa ya nje hayawezi kumuondoa Dk. Shein madarani, lakini wananchi na wafuasi wa CUF wakiungana kwa pamoja kufanya mgomo baridi haifiki miaka mitano Dk. Shein ataachia madarakara

Maalim Seif anaamini kuwa mgomo baridi ndio silaha imara ya kumuondoa madarakani na matumaini yake kwa kuwa wafuasi wa CUF ni wengi wakiendeleza mgomo baridi watafanikiwa.

Mgomo baridi unaoendelea kisiwani Pemba ambao unatekelezwa na wafuasi wa CUF, tayari Dk. Shein na viongozi wezake wa CCM hawana raha kutokana na mgomo huo.

“Niwatake wafuasi wa CUF wasisite na waendelee na kasi hiyo hiyo ya mgomo baridi mpaka haki mliyoporwa Oktoba 25, mwaka jana irejee,” huu ndio msimamo wa Maalim Seif.

“Hawa sasa hivi wapo taabani leo unaambiwa nchi nzima mazungumzo ni Seif baraza la wawakilishi wameacha shughuli zao wanamjadili Seif.”

DK SHEIN

Dk. Shein ambaye ndiye mshindi kwa asilimia 91 ya kura kwenye uchaguzi wa Machi 20, amesisitiza kuwa ndie rais halali wa Zanzibar huku akiwataka wananchi kuyapuuza maneno ya yanayotolewa na wapinzani hasa CUF kwamba Serikali yake haitofika mwaka 2020.

Dk. Shein anasema maneneo yanayosemwa na wapinzani anaona ni utani na dhihaka wanayowambia wananchi kuwa uchaguzi mkuu wa Zanzibar utarejewa tana kabla ya mwaka 2020.

Msimamo wa Dk. Shein kuhusu matamko ya Maalim Seif ni kwamba hakuna hata taifa ama nchi inayoweza kuishurutisha Zanzibar kufanya uchaguzi mwingine kabla ya mwaka 2020.

Amekuwa akisisitiza kuwa Zanzibar inaongozwa kwa Katiba na Sheria za nchi, hivyo hakuna wa kuiongoza na kuleta matakwa yake ili yafuatwe na Zanzibar ili uchaguzi urejewe tena.

Dk. Shein amesisitiza kuwa amewekwa na wananchi kwa mujibu wa Sheria na Katiba ya nchi, hivyo maneno ya dhihaka na utani yanayosemwa na wapinzani kuwa uchaguzi utarejewa ni kasumba za kisiasa.

“Wataumwa hadi kuvimba matumbo, lakini mimi ndie Rais halali wa Zanzibar na nitaendelea kuiongoza Zanzibar hadi mwaka 2020 utakapoitishwa uchaguzi mwingine,” hii ni kauli ya Dk. Shein.

Dk. Shein ambae pia ni makamu mwenyekiti wa CCM, alisisitiza kuwa Serikali haipatikani kwa hujuma, vitimbi ama kufukiza udi, uvumba na ubani bali serikali hupatikana kwa kufuata misingi ya demokrasia na sheria za nchi kama ilivyofanya CCM na hatimaye kushika dola.

Aliwataka wananchi kutokuwa na hasira kwani chama chao cha CCM kimeshinda na ndicho kinachoongoza Serikali na yeyote mwenye nia ya kuvuruga amani na utulivu nguvu za dola zipo na zitapambana naye.

“Mimi nimewekwa kwa ridhaa za wananchi kwa mujibu wa sheria na Katiba na hata Mwenyezi Mungu anajua kuwa mimi ndie Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,” alisisitiza Dk. Shein.

Pamoja na hayo, Dk. Shein aliwataka wananchi na wanaCCM kuendelea na kazi zao kama kawaida na kushirkiana na serikali kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo kwa kuamini kuwa Serikali yao ipo na itaendelea kushirikiana nao.

Kufuatia vitendo vya hujuma vinavyotokea kisiwani Pemba ambavyo vinahusishwa na itikadi za kisiasa, Dk Shein, amevunja ukimya na kutaka sheria ichukue mkondo wake.

Alilitaka jeshi la polisi na ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka kuhakikisha watu wote waliohusika na vitendo vya kunyanyasa wananchi na kuharibu mali wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya dola.
  • via NIPASHE

PEMBA:  CUF, CCM HAWAZIKANI


Makovu ya kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu uliopita yanakitafuna kisiwa cha Pemba baada ya kuibuka ubaguzi baina ya wafuasi wa vyama vikuu vya kisiasa vya CCM na CUF na kuzorotesha shughuli za kijamii na kiuchumi.

Uchaguzi huo ulifutwa Oktoba 25 na mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salim Jecha kwa maelezo kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa sheria na kanuni za uchaguzi, jambo ambalo CUF walilipinga wakisema si mwenyekiti huyo au ZEC mwenye mamlaka ya kufuta uchaguzi, ikidai kuwa chama hicho kikuu cha upinzani kiliibuka mshindi.

Jecha alifuta uchaguzi huo siku ambayo alitakiwa atangaze mshindi wa mbio za urais, huku matokeo ya majimbo 31 yakiwa yameshatangazwa na matokeo ya majimbo mengine tisa yakiwa yameshahakikiwa na washindi kupewa vyeti vyao.

ZEC ilitangaza uchaguzi mpya ambao ulisusiwa na CUF ambayo ilitangaza kutoutambua.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwenye kisiwa hicho kidogo chenye watu takribani 400,000 umebaini kuwa wananchi hao wanabaguana katika misiba, sherehe, vyombo vya usafiri na biashara, jambo ambalo limethibitishwa na polisi, viongozi wa mikoa ya Kusini na Kaskazini Pemba pamoja na wa vyama hivyo viwili.

Matukio ya watu kuvamiwa na kupigwa, wananchi kususa kununua bidhaa za wafuasi wa chama kimoja, mabasi kukosa abiria au abiria kushushwa kwa sababu ya tofauti za kiitikadi, kususia kushiriki katika maziko na harusi yametawala kwenye kisiwa hicho ambacho ni moja ya visiwa vikubwa viwili vinavyounda Zanzibar.

“Wakati baba anafikwa na mauti alikuwa naibu sheha wa shehia ya Bopwe Wete. Lakini wakati wa shughuli za mazishi yake, watu waliokuja msibani walikuwa wachache kwa sababu tu alikuwa mwanaCCM. Tunawajua watu wa CUF pale kijijini na hawakuja msibani,’’ alisema Said Abrahaman mkazi wa wilaya ya Wete akizungumzia mazishi yaliyofanyika mwanzoni mwa Mei.

Abdallah Vuai Ali, dereva wa daladala linalofanya safari zake kati ya Chakechake na Ndagoni, alisema wiki mbili zilizopita alilazimika kupakia abiria mmoja kutoka Ndagoni hadi Chakechake kutokana na watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa CUF kuteremka katika gari hilo baada ya kupanda kada wa CCM.

“Yule mama naye aligoma kushuka katika gari, hivyo nililazimika kumpeleka kituo cha tatu kutoka hapa Ndagoni kisha nikawarudia wale abiria walioshuka,” alisema Ali.

Mwanachi lilifika Wilaya ya Mkoani ambako ilielezwa na baadhi ya wakazi wa eneo la bandari wanavaa sare za vyama ili waweze kutambulika itikadi zao kwa wateja wanaonunua bidhaa mbalimbali.

Omar Ali Faki, aliyedai kuwa ni kada wa CUF, alisema kabla ya wafanyabiashara kuondolewa eneo hilo kutokana na kuibuka kwa ubaguzi huo, biashara zake hazinunuliwi na wafuasi wa CCM.

Gazeti hili lilishuhudia wafanyabishara hao wakiwa wamezuiwa kuendelea na shughuli zao kutokana na uhasama huo wa kisiasa, huku mkuu wa kituo cha Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo (KMKM) katika bandari hiyo, Bakari Kombo Khamis akisema waliwaondoa wafanyabiashara hao kwa kisingizo cha mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu.

“Ilikuwa si ajabu kuona watu wamevaa sare za vyama sokoni na wateja walikuwa wananunua bidhaa kwa kutazama alichovaa muuzaji,” alisema Khamis.

“Kamati ya ulinzi ya wilaya tulikutana kujadili suala hili na kuamua kuwaondoa wafanyabiashara hao ili kupunguza hali hiyo ya kubaguana lakini bado wanafanya biashara kwa kujificha.”

Alidai baadhi ya wananchi wamesusa kupanda meli ya Mv Maendeleo na Mv Mapinduzi kwa maelezo kuwa ni za Serikali iliyopo madarakani na badala yake wanapanda meli ya Sealink ya kampuni ya Azam pamoja na Serengeti.

Viongozi waliozungumza na gazeti hili walisema mvutano na uhasama wa kisiasa upo kwa kiasi kikubwa katika wilaya ya Wete na Micheweni zilizopo Mkoa wa Kaskazini, huku viongozi wa CCM na CUF wakibainisha hatua wanazochukua kuwalinda wanachama wao.

Katibu wa CUF wilaya ya Micheweni, Khatib Hamad Sheikh na katibu wa chama hicho wilaya ya Wete, Riziki Omar Juma wanasema wafuasi wao wataendelea kutoshirikiana na CCM kwa sababu Serikali ikiwabagua kwa muda mrefu.

“Wanachama wetu wanapigwa na polisi bila sababu na tukipeleka taarifa vituoni, hakuna hatua zinazochukuliwa. Vijana wa CUF wananyimwa ajira, wananyimwa vitambulisho vya ukaazi na hati za kusafiria. Haya yote ni mateso ambayo tumeyavumilia na sasa yamefika mwisho,” alisema Riziki.

Katibu wa CCM wa Wilaya ya Kaskazini Pemba, Hadija Nassor Abdi alisema uhasama baina ya wanachama wa CUF na CCM ni mkubwa kiasi cha kutoshirikiana katika shughuli za kijamii.

“Wanachama wetu wakishiriki katika shughuli za watu wa CUF wanafukuzwa, wanawashusha katika daladala na hawawauzii bidhaa ya aina yoyote wanapokwenda dukani,” alisema.

“Mashamba kuvamiwa na mazao kuharibiwa kwa sasa si jambo la ajabu. Nyumba kadhaa zimebomolewa na wiki mbili zilizopita walichoma moto nyumba ya mwanaCCM iliyopo kijiji cha Shumba.”

Itaendelea kesho (via MWANANCHI)

0 comments :

Post a Comment

 
Toggle Footer
TOP