Zoezi la kupunguza wafanyakazi kwenye balozi za Tanzania ng'ambo


Imeelezwa kuwa zoezi linaendelea la kuwapunguza wafanyakazi katika ofisi za mabalozi wa Tanzania katika nchi mbalimbali duniani, kwa kwalengo la kutekeleza agizo la Rais John Magufuli la kubana matumizi yasiyo ya lazima, ili kuwezesha fedha zinazookolewa zielekezwe katika miradi ya maendeleo inayowagusa moja kwa moja wananchi wa kawaida.

Gazeti linalochapishwa na IPP Media Tanzania, NIPASHE linasema hadi sasa, tayari vigogo kadhaa wa ofisi hizo za balozi za Tanzania kwenye nchi mbalimbali duniani wameshakumbwa na hatua hiyo inayotekelezwa na Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa.

Hivi karibuni, Wizara hiyo ilitoa taarifa iliyothibitisha kuwapo kwa mpango wa kuwapunguza maafisa na watumishi wengine mbalimbali kwenye ofisi za ubalozi baada ya kubainika kuwapo kwa idadi kubwa ya watumishi isiyoendana na mahitaji halisi ya kazi zilizopo.

Akizungumza na NINAPSHE hivi karibuni, waziri katika wizara hiyo, Balozi Augustine Mahiga, alisema baadhi ya maafisa hao tayari wamesharejea nchini wakitokea kwenye vituo vya kazi walivyokuwapo nje ya Tanzania.

Akizungumza bila kutaja takwimu, Mahiga alisema maafisa na watumishi wengine mbalimbali wako pia katika mchakato wa kurejea nchini, baadhi wakiwa njiani na wengine wanasubiri fedha za kuwasafirisha kutoka walipo.
“Tayari kazi hiyo inaendelea. Tunavyozungumza tayari kuna wengine wengi wako hapa nchini na wengine wako njiani,” alisema Mahiga.
Akieleza zaidi, Mahiga alisema zipo baadhi ya ofisi za balozi ambazo zilikuwa na mrundikano mkubwa wa maafisa na watumishi wengine pasi na sababu za msingi.
“Kuna balozi zetu ambazo hadi sasa watumishi ni wengi sana kulinganisha na majukumu yaliyopo. Sasa tumeona ni vyema tuwapunguze na tunaendelea kutekeleza hilo kadri tunavyopata fedha za kuwasafirisha,” aliongeza Mahiga.
Ili kupata takwimu za watumishi waliopunguzwa, Nipashe ilimtafuta Msemaji wa Wizara hiyo, Mindi Kasiga, lakini kila alipopigiwa alikuwa akipokea simu yake lakini hakukuwa na majibu kutoka kwake.