Rais ndiye anaamua fedha zinazorudi zitumikeje - Waziri

FEDHA zinazobaki kutokana na kubana matumizi yanayofanywa na taasisi mbalimbali za umma na kisha kurudishwa serikalini, zitatumika kwa namna Rais John Magufuli atakavyoona inafaa, Bunge limeambiwa.

Kauli hiyo ilitolewa jana mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jaffo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Nsimbo, Richard Mbogo (CCM).

Alisema zitakuwa zinaelekezwa kwenye matatizo na kero zinazohitaji fedha kwa kuwa kero bado ni nyingi.

Mbunge huyo alikuwa ameomba kama inawezekana, fedha zinazorejeshwa serikalini baada ya kumalizika kwa bajeti ya sasa kutokana na taasisi za umma kubana matumizi zielekezwe katika ujenzi wa vituo vya afya ikiwa ni pamoja na vilivyo katika jimbo lake.

“Kwanza ninamshukuru sana Rais John Magufuli kwani uongozi wake ndio umesaidia hali hii ya taasisi kubana matumizi hadi fedha kurejeshwa serikalini. Lakini Rais ataangalia ni nini cha kuzifanyia pesa hizo kwa sababu matatizo yanayowakabili wananchi wetu ni mengi,” alisema. [HabariLeo]