“Hayo ni matokeo ya awali ya watafiti wa wizara yangu hivyo basi nasubiri matokeo ya vipimo vya damu na haja ndogo vilivyopelekwa kwa uchunguzi zaidi katika Maabara ya CDC, Atlanta iliyopo nchini Marekani na matarajio yetu ni kupata majibu hayo katika kipindi kisichozidi wiki moja” aliongeza Bi Mwalimu.Aidha Bi. Mwalimu amesema kwamba mpaka kufikia tarehe 24 Juni 2016, idadi ya wagonjwa imefikia 32, na idadi ya vifo imebakia 7. Hii ni baada ya kuongezeka kwa wagonjwa 11 katika kipindi cha wiki moja.
“Hadi jana kulikuwa na jumla ya wagonjwa 9 ambao wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa ya Dodoma, na 14 wako katika Hospitali ya Wilaya ya Kondoa. Wagonjwa watatu waliolazwa Hospitali ya Mkoa Dodoma, na wawili waliolazwa Kondoa, bado hali zao ni tete” aliongeza Bi. Mwalimu.Pamoja na hayo Bi. Mwalimu alisema kwamba Serikali itaendelea kuimarisha mikakati ya kitaifa ya kupunguza uchafuzi wa sumukuvu katika vyakula, ikiwa ni pamoja na kujenga uwezo wa kupima vimelea hivyo katika damu na mkojo miongoni mwa taasisi za ndani ya nchi.
“Tutaendelea kutoa matibabu kwa wananchi walioathirika na Ugonjwa huo, kwenye Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na Hospitali ya Wilaya ya Kondoa ili kudhibiti na kurudisha afya za wananchi katika kiwango kinachohitajika,” aliongeza Bi. Mwalimu.Aidha Bi. Mwalimu ametoa rai kwa wananchi na wakazi wa Dodoma kuchambua nafaka zilizoharibika (zilizooza, kuvunjika, zilizobadilika rangi), kukoboa mahindi kabla ya kuyasaga au kuacha kutumia nafaka zitakazoonekana kuharibika sana ili kuepukana na kiasi kilichozidi sumukuvu kwenye nafaka.