Taarifa ya TRA: Kampuni 4 zilizoiibia serikali sh29.2 bilioni za mapato kwa mashine ya EFDUkwepaji kodi kwa kutumia risiti bandia

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) wamebaini kuwepo na baadhi ya Makampuni na watu binafsi ambao wamekuwa wakijihusisha na ukwepaji Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na Kodi ya Mapato kwa kutumia Mashine za Kielektroniki (EFDs) ambazo hazijasajiliwa na TRA na kutoa risiti bandia.

Makampuni hayo yamekuwa yakinunua risiti za manunuzi bandia kutoka kwa watu wanaomiliki mashine za kielektroniki (EFDs) ambazo hazijasajiliwa na kuzitumia risiti hizo kudai marejesho ya VAT bila kuwepo na bidhaa au huduma halisi iliyouzwa au kutolewa na muhusika, kitendo ambacho kinainyima Serikali mapato stahiki kwa mujibu wa sheria.

TRA kwa kushirikiana na TAKUKURU inaendelea na uchunguzi ili kubaini makampuni yote yanayojihusisha na udanganyifu huu, ambapo hadi sasa jumla ya makampuni manne (4) yamebainika kujihusisha na ukwepaji kodi kwa mtindo huu kuanzia mwaka 2010 hadi 2014; na jumla ya shilingi 29,216,900,301.7 imebainika kutokulipwa Serikalini na makampuni hayo kwa kipindi hicho.

Makampuni hayo manne ni pamoja na Skol Building Material Ltd ambayo tangu mwaka 2012 hadi 2013 haikulipa jumla ya VAT ya shilingi 5,464,915,963 na Kodi ya Mapato yenye thamani ya shilingi 10,960,787,861 ambayo jumla ya kodi inayodaiwa ni shilingi 16,425,703,824 kwa kipindi hicho.

Kampuni nyingine ni Farm Plant (T) Limited, tangu mwaka 2010 hadi 2014 haikulipa jumla ya VAT ya shilingi 5,930,170,573 na Kodi ya Mapato yenye thamani ya shilingi 4,948,393,516 ambayo jumla ya kodi inayodaiwa ni shilingi 10,878,564,089.

Kwa upande wa A.M. Steel & Iron Mills Limited kuanzia mwaka 2013 hadi 2014 haikulipa jumla ya VAT ya shilingi 79,016,112 na Kodi ya Mapato yenye thamani ya shilingi 131,693,518 ambayo jumla ya kodi inayodaiwa ni shilingi 210,709,630.

Kampuni nyingine ni A.M. Trailer Manufacturers Limited ambayo tangu mwaka 2013 hadi 2014 haikulipa jumla ya VAT ya shilingi 638,221,034.80 na Kodi ya Mapato yenye thamani ya shilingi 1,063,701,724.00 ambayo jumla ya kodi inayodaiwa ni shilingi 1,701,922,758.80

Baada ya kubaini ukwepaji kodi wa makampuni hayo, TRA kwa kushirikiana na TAKUKURU inaendelea na uchunguzi wa tuhuma hizi na mara baada ya uchunguzi kukamilika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kukwepa kodi.
“Ni wito wangu kwa wafanyabiashara wote kutojihusisha na kununua risiti za bandia na kudai marejesho ya (VAT) yasiyostahili kwa kuwa Mamlaka imejidhatiti kuendelea na zoezi hili la kuwabaini wafanyabiashara wanaokwepa kodi na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria kwa hatua stahiki”. 
Alisema Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Alphayo Kidata.


Imetolewa na:


Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) kwa pamoja.

----
Chanzo cha taarifa: www.tra.go.tz