Loading...
Thursday

Taarifa ya Wakala ya Serikali Mtandao kuhusu Miradi ya TEHAMA Serikalini

Taasisi za umma zinashauriwa kushirikiana na Wakala ya Serikali Mtandao (eGA) katika kupanga na kutekeleza Miradi ya TEHAMA Serikalini ili kurahisisha mpango wa kubaini na kuondoa urudufu na kuipunguzia Serikali gharama za usakinishaji na uendeshaji mifumo inayofanana ndani ya Serikali.

Hayo yamesemwa na Meneja Habari, Elimu na Mawasiliano wa Wakala Bi. Suzan Mshakangoto kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi ya Wakala Juni 2, 2016.

“Taasisi yoyote ya umma inayotaka kuanzisha mradi wa TEHAMA inatakiwa kuwasilisha mradi wake ukiwa unaendana na vigezo vilivyowekwa katika orodha hakiki ya miradi ya TEHAMA Serikalini,inayopatikana katika tovuti ya Wakala www.ega.go.tz, kwa Wakala ili uweze kuhakikiwa na kuthibitishwa”, alisema Bi. Mshakangoto.

Amesema baadhi ya vigezo vya mradi ni kuonesha jinsi gani utaboresha utendaji kazi wa taasisi husika, utoaji wa huduma kwa umma ikilinganishwa na utaratibu wa zamani na iwapo unatimiza malengo ya Dira ya Taifa ya Mandeleo 2025 na unazingatia Sera, Viwango, Miongozo na Taratibu za Serikali.

Ameongeza kuwa, taasisi za umma zinatakiwa kuweka taaarifa za miradi ya TEHAMA inayoendelea katika mfumo wa Usimamizi wa Miradi ya TEHAMA Serikalini (Government ICT Project Portfolio) unaopatikana kwa anuani ya https://gip.ega.go.tz ambao unapokea na kutunza taarifa za miradi ya TEHAMA iliyopo na inayotarajiwa kuanzishwa Serikalini.

Ameeleza kuwa, taasisi za umma zimekuwa na miradi ya TEHAMA ambayo inafanana na hivyo kuiongezea Serikali gharama ya kuiendesha miradi hiyo jambo ambalo limekuwa na changamoto kubwa kwa Serikali.

“Ipo miradi au mifumo ambayo imekuwa haibadilishani taarifa suala ambalo limepelekea kuwa na taarifa zisizolingana. Pia miradi au mifumo mingine imekuwa ikishindwa kujiendesha na hivyo kushindwa kufanya kazi kama ilivyokusudiwa, kwa kweli hii imekuwa ni changamoto kubwa”, alifafanua Bi. Mshakangoto.

Vilevile amesema, Wakala itahakikisha taasisi za umma zinakuwa na mifumo inayoongea, inayobadilishana taarifa na inayozingatia teknolojia iliyopo ili kuweza kukidhi mahitaji ya Serikali na kuboresha utoaji huduma kwa umma.

“Wakala inawashauri wafanyabiashara wanaojihusha na miradi au utengenezaji wa mifumo ya TEHAMA Serikalini kufuata orodha hakiki iliwekwa ili kujua mahitaji halisi ya Serikali na kuweza kujenga mifumo ya TEHAMA endelevu na inayoleta tija kwa umma”, alisisitiza Bi. Mshakangoto.

Wakala ya Serikali Mtandao (eGA), iliyoanzishwa 2012, ni taasisi ya Serikali yenye majukumu na mamlaka ya kuratibu, kusimamia na kukuza jitihada za Serikali Mtandao nchini Tanzania. Pia Wakala hii inasimamia udhibiti wa viwango vya Serikali Mtandao kwa kutumia Miongozo mbalimbali na Viwango vilivyowekwa ili kuwa na mifumo bora ya TEHAMA Serikalini.


0 comments :

Post a Comment

 
Toggle Footer
TOP