UKAWA vs CCM: Tumekubaliana wenye mahusiano ya kimapenzi na wabunge wa CCM yasitishwe kwa muda


WABUNGE wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), wameazimia kutoshirikiana na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika michezo ya aina yoyote.

Maazimio hayo yalifikiwa jana baada ya wabunge hao kutoka ndani ya Ukumbi wa Bunge huku wakiwa wameziba midomo yao kwa plasta na karatasi nyeupe, ikiwa ni ishara kupinga kunyimwa haki za kuzungumza ndani na nje ya Bunge.

Akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Bunge jana, Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (CHADEMA), alisema wamefikia uamuzi huo ili kuionyesha dunia kwamba wanapinga hatua ya Serikali kuwanyima uhuru wa kuzungumza kinyume na Katiba ya nchi.
“Leo tumekubaliana hatutashiriki katika michezo na wabunge wa CCM, hilo tumeanza leo asubuhi kwenye mazoezi katika viwanja mbalimbali, hivi sasa tunatafakari hata kutafuta uwanja wetu.
“Tukikutana katika uwanja mmoja, sisi tutatumia upande mmoja na wao watatumia upande mwingine, hatuchanganyani, hata salamu leo kuna mmoja kanisalimia nimekwepesha mkono wangu,” alisema Kubenea.
Kubenea alisema hata katika mechi zinazoandaliwa kwa ajili ya timu ya wabunge UKAWA hawatashiriki katika kipindi hiki cha wiki mbili zilizobakia za bajeti.
“Si katika michezo tu, hata katika mahusiano, tumekubaliana kama kuna wabunge wana mahusiano ya kimapenzi na wabunge wa CCM yasitishwe kwa muda wa wiki mbili mpaka tutakavyoamua vinginevyo,” alisema Kubenea.

Jana asubuhi, mbunge wa CCM Kangi Lugola alisema kuwa alisikitishwa baada ya kudai kuwa Mbunge wa Chadema (Viti Maalumu), Lucy Magereli hakumjibu salamu yake wakati akiingia bungeni licha ya kumsalimia mara tatu na kuwa katika umbali mfupi wa kusikika.

“Kusalimia ni jambo la utamaduni wetu. Nilikuwa namsalimia mbunge wa kike wa Ukawa, lakini hakujibu. Lakini, nikajua ni sababu ya wao kufunga mdomo na plasta, nikamtania au kwa sababu ya plasta hujibu ili isije kudondoka hakuitikia,” alisema Lugola.

Alisema ameshtushwa na hali ilipofikia na hajui sababu za msingi za wabunge wa Ukawa kufanya vitendo hivyo, kinyume na udugu na utamaduni wa Watanzania.

Mbunge huyo machachari, alisema Kubenea alimziba mdomo Msigwa kwa mkono ili asizungumze chochote.

Naye mbunge wa Sumve (CCM ) Richard Ndassa alisema jambo wanalolifanya wabunge wa Ukawa siyo jema na halina tija kufanywa na wawakilishi hao wa wananchi.

“Sisi ni wabunge, hivi inapofikia kususa kuongea na wabunge wenzako, hatima yake nini?” alisema.

“Mimi nilienda kuwasalimia kama kawaida ambavyo huwa tunafanya kwa wabunge awe CUF, CCM au Chadema, sasa unavyosusa una maanisha nini,” alilalamika Ndassa.

Alisema kitendo cha kutosalimia ni cha juu sana na kwamba iwapo Ukawa wanashauriwa na mtu basi inawapasa kuchuja mambo mengine, likiwamo hilo la kuwasusa wabunge wenzao.

Juzi Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia wakati anawaongoza wabunge wa Ukawa kutoka bungeni aliwatuhumu wabunge wenzao wa CCM kuwa wanawabagua.