[update] Gazeti laomba radhi; "Utabiri" wa NIPASHE kuhusu Wakuu wa Wilaya na kilichotokea leo

Gazeti la leo, Jumatatu, Juni 27, 2016 limemuomba radhi Mku wa Mkoa wa Dar es Salaam...


Makonda aliandika ujumbe huu kuhusu habari iliyochapishwa na gazeti hilo jana...


Jana gazeti hilo lilichapisha habari ifuatayo....


Mchana wa leo, imetangazwa rasmi orodha ya safu ya uongozi wa wateuzi wa Rais katika ngazi ya Wilaya. Gazeti la NIPASHE Jumapili lililotoka asubuhi ya leo, lilichapisha habari ifuatayo...

Sifa za Makonda kuwaponza Ma-DC kibao


SIFA ambazo Rais John Magufuli amekuwa akimpa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuhusiana na utendaji wake wa kuvutia huenda zikasababisha kung’olewa kwa Wakuu wa Wilaya wengi ambao umri wao unaelekea kuwatupa mkono zaidi.

Chanzo kimoja kimeiambia Nipashe kuwa Magufuli alishaonyesha kuvutiwa na utendaji wa Makonda na pia vijana wengine kadhaa aliowaamini katika kipindi chake cha kuwapo madarakani tangu alipoapishwa Novemba 5, mwaka jana, hivyo kuna kila dalili kuwa uteuzi wake wa wakuu wa wilaya unaotarajiwa kufanyika wakati wowote kuanzia Julai mwezi ujao huenda ukwaponza wakongwe wengi na kuwanufaisha vijana.
“Kama alivyosema kwamba tatizo la madawati linaweza kutumika kama kigezo cha nani abaki na nani aendelee na kazi... lakini ni wazi pia kuna vigezo vingine atavitumia kuwachuja watu wa kuwabakiza katika nafasi hizo kama ile ya kushindwa kutatua migogoro ya ardhi na namna ya kukabiliana na njaa. Utendaji wa Makonda na vijana wenzake unaweza pia kuwa chanzo cha wengi kupoteza nafasi zao, hasa wale ambao umri umekwenda sana,” chanzo kiliiambia Nipashe mwishoni mwa wiki.
Rais Magufuli alitoa muda hadi kufika mwishoni mwa mwezi huu kuona kuwa wakuu wote wa wilaya na mikoa wahakikishe hakuna tatizo la madawati kwenye maeneo yao ya kazi na kwamba vinginevyo, kila atakayeshindwa atakwenda na maji.

Chanzo kingine kilisema kuwa tangu Rais Magufuli alipoteua Wakuu wa Mikoa wapya na kuwaacha 12 wa zamani, wakuu wengi wa wilaya wamejawa na hofu kuhusiana na hatma yao kutokana na kutokuwa na uhakika kuwa watabaki kwenye nafasi zao ama la.

Aidha, ilielezwa kuwa dalili za kuwapo na hofu kubwa kwa baadhi ya wakuu wa wilaya waliopo sasa ni wengi wao kuonekana wakicharuka na kuwasimamisha watendaji wanaoona kuwa hawaendani na kasi ya sasa ya serikali ya awamu ya tano, lengo likiwa ni kuongeza ufanisi wa kazi na pia kumthibitishia Rais kuwa wanatosha katika nafasi hizo na hivyo asiwaache wakati wa uteuzi wake mpya.

Ilielezwa kuwa baadhi ya wakuu hao wa wilaya wamekuwa wakifanya kazi ya ziada ili kuhalalisha uwapo wao, ikiwa ni pamoja na kupiga picha za matukio mbalimbali ya kijamii na kuzisambaza kwenye vyombo vya habari na pia mitandao ya kijamii.
“Kuna kila dalili kwamba ma-DC wengi wazee watapoteza kazi… hata wakati akifungua mkutano wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi Mei 27 (2016), Rais Magufuli alisema hataona shida kuwajaza vijana wengi kwa sababu wale aliokwishawaweka tayari wameonyesha uwezo mkubwa wa kiuongozi,” chanzo kingine kiliiambia Nipashe.
Katika hotuba yake hiyo ya Mei, ingawa Rais Magufuli hakumtaja kwa jina, lakini ilifahamika wazi kuwa aliyemvutia zaidi ni Makonda ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kabla ya kupandishwa na kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Kadhalika, katika nyakati tofauti, Rais Magufuli amekuwa akimsifu Makonda na kumtambulisha kama ‘kijana mchapakazi.’

Kwenye mkutano wake na wazee wa mkoa wa Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema anajua watu wanauliza ni lini atateua wakuu wa Mikoa na Wilaya hivyo alitaka wanaouliza hivyo wajibiwe kwamba bado anawachambua.
“Watakaowauliza waambieni bado naendelea na uchambuzi ili kuona nani anatosha na nani hatoshi, lakini angalau Mheshimiwa Makonda wewe umeshajihakikishia utakuwamo… lakini usiende kulala, kaendelee na juhudi zako,” alisema Rais Magufuli kabla hajatimiza ahadi yake kwa kumteua Makonda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Machi 13 mwaka huu wakati alipowateua wakuu wa mikoa 26, kati yao 13 wakiwa wapya.
HOFU ZAIDI

Kwenye mkutano huo wa Bodi ya Makandarasi, Rais Magufuli alisema kuanzia sasa wateule wake wengi serikalini watakuwa ni vijana kwakuwa amegundua wengi wao hawapendi rushwa na tena ni wachapakazi wazuri.

Alisema ingawa anafahamu kuwa vijana hawapendwi, lakini amegundua kuwa ndiyo wachapakazi hodari na ambao watasaidia kulipeleka taifa katika maendeleo anayoyatamani kwakuwa aliowaweka tayari ameshaanza kuona matunda ya kazi zao.

Magufuli alienda mbali zaidi kwa kusema kuwa baadhi ya wazee walioaminiwa na kupewa nafasi serikalini wamekosa uzalendo na ndiyo walioifikisha nchi mahala pabaya.

Wakati huo huo, akihutubia kwenye sherehe za kuzaliwa CCM mkoani Singida, Februari 6 mwaka huu, Rais Magufuli alisema hatawavumilia viongozi wa mikoa na wilaya ambao watakuwa wakikaa kwenye ofisi nzuri, viti vizuri na kupigwa na hewa safi ya viyoyozi huku wanafunzi katika maeneo yao wakiketi chini.

Zikiwa zimebaki siku nne kuanzia leo kufikia siku ya mwisho aliyotoa Rais Magufuli kwa ajili ya kukamilisha upatikanaji wa madawati nchini kote, wakuu mbalimbali wa wilaya na mikoa wanaendelea kufanya jitihada za kila namna kutimiza azma hiyo.