Wagonjwa, wauguzi MOI wataabika kwa kukosa lift; Uongozi wakana; Fundi akiri kukata huduma


Ukosefu wa "lift" katika jengo la wagonjwa la taasisi ya mifupa ya MOI katika Hospitali kuu ya Taifa Muhimbili Dar es Salaam umeelezwa kuwa moja ya changamoto kubwa inayowakabili wagonjwa wanaofika katika kitengo hicho kwa ajili ya kupata matibabu.

Mmoja wa wauguzi wa jengo hilo ambaye tunahifadhi jina lake ameieleza ITV madhila wanayoyapata kuwapandisha wagonjwa kutoka ghorofa ya kwanza hadi ya tano kwa kutumia ngazi.

Huku tukipiga picha kwa usiri, tulizungumza na mmoja wa mafundi wa kampuni ya "Premider Elevator" ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake ambapo amesema wameamua kusitisha utoaji huduma wa "lift" kutokana deni kubwa wanaloidai taasisi hiyo, na kwamba watafanya hivyo mpaka pale deni lao litakapolipwa.

Lakini uongozi wa taasisi hiyo ya mifupa ya MOI umesisitiza hakuna tatizo la "lift" katika jengo hilo, huku wagonjwa wakisema "lift" ni changamoto kuu kwa wiki sita sasa.