Hatimaye wananchi waliowahi kuwa wafanyakazi wa kiwanda cha nguo MWATEX cha jijini Mwanza wameshinda kesi ya kudai stahiki zao.
Kesi hiyo ya mwaka 1995, ilifunguliwa na wafanyakazi hao baada ya kiwanda hicho kudaiwa kufilisika na kuwaondoa wafanyakazi hao pasipo kuwapa barua za kuachishwa kazi.
Baadhi ya waliowahi kuwa wafanyakazi wa kiwanda hicho wamesema licha ya kuwa wameshinda kesi, hukumu hiyo haijaeleza wazi juu ya stahiki zao za kwamba ni kiwango gani wanatakiwa kulipwa kwa kukaa bila malipo kwa zaidi ya mika kumi na tano.
Kesi hiyo imetolewa hukumu tarehe 14 mwezi huu na wanachosubiri ni kuona nini makubaliano na uongozi wa MWATEX kujua kiasi gani kinahitajika.
Rozaria Lymo ni mmoja kati ya wafanyakazi waathirika wa kiwanda hicho waliozungumza nasi, akisema amekuwa mfanyakazi wa kiwanda hicho tangu mwaka 1972, akitaja kuwa bado hawajajua nini mstakabali wa malipo yao, kwani kuna fununu zinazodai kuwa watalipwa kwa viwango vya mishahara ya zamami, hali kadiri miaka inavyosonga mbele viwango vya fedha, hata vile vya kima cha chini cha mshahara, vimekuwa vikibadilika.
Baadhi ya wafanyakazi wametoa ushuhuda kuwa kuna baadhi ya watendakazi wenzao wamepoteza maisha kutokana na mfadhaiko na msongo wa mawazo; Familia zimeharibika kwa watoto kushindwa kwenda shule; Ndoa zimevunjika kwa kukosa kipato huku wengine wakipata maradhi ya msongo wa mawazo.
- via GSengo blog