Loading...
Saturday

Wanafunzi UDom wawashangaa waanzilishi wa programu; Wamwomba Rais Magufuli awakabili wadahili

null


Mtandao wa wanafunzi nchini Tanzania Unamuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dakta John Pombe Magufuli kuwachukulia hatua wale wote waliodahili wanafunzi wasio na sifa katika programa maalum iliyoanzishwa katika chuo kikuu cha Dodoma na sio kuwaadhibu wanafunzi wote ambapo wengine hawakuwa na hatia.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa mtandao huo Bw Alphonce Lusako alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari hii leo jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa Rais amesema baadhi ya wanafunzi walidahiliwa wakiwa hawana sifa za kujiunga na programu hiyo mtandao unaona kosa hilo ni la wadahili na siyo la wanafunzi, hivyo wanafunzi wenye sifa wangeachwa waendelee na masomo yao kama kawaida.

Bw Lusako amebainisha kuwa kutokana na sakata hilo, wanafunzi wengi wameathirika kisaikolojia na kukata tamaa wasijue nini cha kufanya huku wengine wakijilaumu kujiunga na programu hiyo ambayo kama sivyo, wangeendelea na Kidato cha Tano na wangekuwa wanahitimua Kidato cha Sita hivi sasa.

Aidha kwa upande wake, mwanafunzi ambaye ni mhanga wa sakata hilo, Ibrahim Abdalah amesema kuwa wanasikitika kuona hata walioanzisha program hiyo wanashindwa kujitokeza kuwatetea kwani hawakwenda kujiunga na programu hiyo kwa ridhaa zao bali ni serikali iliyoamua kuianzisha ili kukabiliana na upungufu wa walimu wa sayansi nchini.

Akisoma taarifa rasmi ya wanafunzi waliosimamishwa UDOM, Gibson Johnson alisema, wanaiomba serikali kuangalia uwezekano wa wao kuendelea na masomo yao.

“Tunaiomba na kuililia serikali iangalie wale wenye division I, II na III ituache tumalizie masomo yetu, lakini watakaokuwa na ufaulu wa chini kuanzia division IV itafute namna ya kuwasaidia,” alisema Johnson.

Wamemuomba Rais Magufuli na Waziri wa Elimu, Sayansi,Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako kuona haja ya kuwarudisha chuoni ili kumaliza masomo yao kama ilivyopangwa, kama jambo hilo likishindikana serikali ifanye mkakati wa kuwatafutia vyuo stahiki ili wamalize masomo yao.
 
Toggle Footer
TOP