Wizara yaandaa nyaraka za kuwaburuza mahakamani wabadhirifu wa KNCU


WIZARA ya Kilimo,Mifugo na Uvuvi kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika imeanza kuandaa utaratibu za kuwachukulia hatua wahusika wa ubadhirifu uliosababisha chama kikuu cha ushirika cha KNCU Ltd kushindwa kulipa deni lake la sh bilioni 3.4 ilililokopa benki ya CRDB.

Akijibu swali lililoulizwa na mbunge wa Siha, Godwin Mollel (Chadema) kwanini serikali isiwajibishwe viongozi wa KNCU aliosababisha hasara kwa kuchukua mkopo huo walioshindwa kulipa Naibu waziri Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Tate William Ole-Nasha (pichani)alisema serikali inawachukulia hatua wahusika wote kwa mujibu wa kifungu 15 (33) cha sheria ya ushirika.

Ole Nasha alisema Chama kikuu cha Ushirika cha KNCU Limited kilishindwa kulipa deni la shilingi bilini 3.4 kutoka CRDB lililokopwa 2008/2009 na 2010/2011 kutokana na mdodoro wa kiuchumi na ubadhirifu au uongozi mbovu.

Alisema baada ya serikali kubainisha hayo kufuatia ukaguzi uliofanyika, Tume ya Maendeleo ya ushirika iliisimamisha Bodi iliyokuwa madarakani na kuiweka mpya kama hatua za awali kabla ya kuchukua hatua za sasa za kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wahusika.

Katika swali hilo lililoulizwa kwa niaba na mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega (CCM) ambapo pia alitaka mpango wa serikali kurudisha mashamba ya ushirika yanayotumika kwa maslahi ya wachache.

Mollel ambaye swali lake lilijipambanua kwenye uuzawaji wa shamba la Gararagua uliofanywa na KNCU Ltd mwaka 2015 ili kulipa deni la CRDB alitaka kujua mipango ya serikali kuwajibisha watendaji na pia kurejesha umiliki wa mashamba kwa halmashauri kwa yale ambayo ushirika umeshindwa.

Ole-Nasha alisema kwamba Tume ya ushirika kwa kushirikiana na Mkurabita, Tamisemi na vyama vikuu vya ushirika nchini inakamilisha maandalizi ya mpango wa matumizi bora ya ardhi.

Alisema mpango huo ambao utajadiliwa katika mkutano wa vyama vyote vya ushirika unaoketi mkoani Dodoma kuanzia jana kw asiku mbili utakubaliana mkakati wa kuyaendeleza mashamba kw amanufaa ya wanachama na halmashauri kwa ujumla.

Kwa mujibu wa takwimu ambazo Tume ya maendeleo ya Ushirika inazo, yapo mashamba 96 ya vyama vya ushirika nchini yakiwemo 41 mkoa wa Kilimanjaro.Kati ya mashamba hayo, mashamba 7 yapo wilaya ya Siha, ambapo matatu yanamilikiwa na KNCU na mengine manne yanamilikiwa na vyama vya msingi.

mengi ya mashamba hayo yamekuwa yakitumika kwa kilimo, ufugaji na ujenzi wa nyumba za makazi ya wanachama na kukodishwa. [Lukwangule blog]