Yule askari FFU wa Arusha aliyembaka mwanafunzi wa Korogwe Girls School atupwa jela miaka 30 na viboko 12

MAHAKAMA ya Wilaya ya Arusha imemhukumu kwenda jela miaka 30, kuchapwa viboko 12 na kulipa fidia ya Sh. milioni 15, askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Raphael Makongojo (25), baada ya mahakama hiyo kumkuta na hatia ya kumbaka mwanafunzi.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kusomwa kwa hukumu hiyo, hakimu aliyesikiliza kesi hiyo aliyeomba jina lake lisitajwe, alisema mbali na adhabu hiyo pia mahakama imemwamuru askari huyo kufanya kazi ngumu.

Mama mzazi wa binti huyo (jina limehifadhiwa) akizungumza nje ya mahakama hiyo, alipongeza kutolewa hukumu hiyo, lakini akaongeza ingefaa adhabu ingekuwa ya kifungo cha maisha kwa sababu baada ya miaka 30 anaweza kutoka na kuendeleza vitendo kama hivyo.

Mshtakiwa alifikishwa mahakamani hapo Februari, mwaka huu akidaiwa kumbaka mwanafunzi huyo Januari 16, mwaka huu eneo la kwa Morombo, kwenye uwanja wa mpira wa FFU jijini hapa.

Ilidaiwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 130 (1 na 2 a) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, sura ya 16.

Awali mshitakiwa alikana kutenda kosa hilo, lakini baada ya hukumu hiyo kutolewa ndugu wa mshitakiwa walionyesha nia ya kukata rufaa. [NIPASHE]