Loading...
Wednesday

Zitto apata dhamana baada ya kuhojiwa Polisi

Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe jana tarehe 7/6/2016 aliitwa Polisi na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es salaam ACP Camilius Wambura.

Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa chama hicho Ado Shaibu alisema ACP Wambura alimwita Zitto Kabwe kuhojiwa ikiwa ni siku moja imepita tangu azindue operesheni "Linda Demokrasia" ambayo inatarajiwa kuzunguka nchi nzima kupinga ukandamizwaji wa demokrasia nchini

Amesema licha ya Zitto kuitwa na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Wambura aliomba Zitto asiende jana kwa kuwa ni karibu na muda wa kufuturu na kumtaka aende leo saa tatu asubuhi ambapo aliitikia wito na kuripoti.

Shaibu alisema ACT-Wazalendo iliwasiliana na wanasheria wao ili kupata tafsiri ya kimahakama ya uhalali wa jeshi la polisi kuzuia mikutano ya vyama vya siasa ambayo inatambuliwa na kulindwa na katiba.

Akizungumza na wanahabari kituoni hapo mara baada ya kutoka, mwanasheria wake, Stephan Mwakibola, alisema kuwa kiongozi huyo amehojiwa kuhusiana na maudhui ya hotuba ambayo aliitoa Jumapili iliyopita katika mkutano uliofanyika katika Viwanja vya Mbagala-Zakhem jijini Dar.

Naye Zitto alisema kuwa anasikitika kuona siku hizi kiongozi wa chama cha siasa anapokwenda kwenye mikutano analazimika afikirie kutafuta maneno ya kuzungumza.

Mwakibola alieleza kuwa polisi wamemruhusu Zitto kuendelea na shughuli zake za kila siku baada ya kupewa dhamana, na Jumatano ijayo ametakiwa kuripoti tena polisi. Hata hivyo, wakili huyo hakuwa tayari kuweka bayana sehemu ya hotuba ambayo ililileta utata kwa sababu suala hilo bado liko chini ya upelelezi.


 
Toggle Footer
TOP