Aliyefanyikwa ukatili na kukatwa matiti ajifungua; Anaomba msaada

Moshi. Msichana Maria Aloyce (23), ambaye Januari mwaka huu alikatwa matiti yake yote na mwanamume mmoja, amejifungua mtoto wa kike huku changamoto ikiwa ni jinsi ya kumnyonyesha.

Msichana huyo, mkazi wa Kijiji cha Ghona, Kata ya Kahe Mashariki, alifanyiwa unyama huo Januari 7 na polisi kuchukua zaidi ya miezi mitano kumtia mbaroni mtuhumiwa. Wakati akikatwa matiti hayo, alikuwa na ujauzito wa miezi mitano.

Mmoja wa majirani anayemuuguza msichana huyo, Fadhilai Mrisha amesema kuwa Maria amejifungia salama katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC. 
“Amejifungua mtoto wa kike mwenye uzito wa kilo 3.1 lakini changamoto kubwa ni kwamba hana matiti yote na mtoto anahitaji maziwa. Kwa kweli huu ni mtihani,” amesema Mrisha.
Msichana huyo aliwaomba wasamaria wema kumsaidia maziwa kwa ajili ya mtoto wake pamoja na kugharimia matibabu katika kipindi chote alicholazwa kwa vile hana uwezo.
“Ninaomba wanisaidie nipate maziwa ya mtoto. Kama unavyoniona sina matiti, yote yamekatwa kabisa nimebaki na makovu tu. Kuna gharama za matibabu. Nisaidieni,” amesema.
Chanzo cha taarifa: Daniel Mjema, [email protected]MWANANCHI