Aliyekuwa Katibu wa Dayosisi KKKT ahukumiwa miaka 30 jela kwa kubaka

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kusini Kati, Edward Ahazi Masevela (54) amehukumiwa kwenda jela miaka 30 baada ya kupatikana na hatia ya kubaka na udhalilishaji.

Alifikishwa katika mahakama ya wilaya ya Makete Mei, mwaka huu akituhumiwa kumbaka na kumdhalilisha mtoto mwenye umri wa miaka 12 ambaye ni mwanafunzi katika moja ya shule za msingi wilayani humo.

Na katika kosa lingine alituhumiwa kumfanyia shambulio la aibu la mtoto mwingine wa kike ambaye pia ni mwanafunzi katika moja ya shule za wilaya hiyo kwa kumuingiza vidole sehemu za siri.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Njombe, Cosmas Joseph Hemela alisema mahakama hiyo imejiridhisha pasipo shaka na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka dhidi ya tuhuma hizo.

Alisema kwa kuzingatia ushahidi huo, mahakama imemkuta mtuhumiwa na makosa mawili, moja ni la ubakaji na lingine ni la shambulio la aibu.

Alisema Masevela alitenda makosa hayo kati ya mwezi Julai 2015 na April 2016 kabla hajafikishwa mahakamani hapo Mei, mwaka huu.

Kwa kuzingatia kifungu cha sheria namba 130(1) na kifungu cha 131 (1) kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2002, mtuhumiwa amekutwa na hatia ya Kubaka na kufungwa jela miaka 30.

Na kwa kuzingatia kifungu cha sheria namba 138(1)(a)(2b) kilichofaniwa marekebisho mwaka 2002, mtuhumiwa amekutwa na hatia ya kufanya shambulio la aibu kwa kumwingiza vidole sehemu za siri mtoto mdogo na kukutwa na hatia inayompeleka jela miaka miwili.

Alipopewa nafasi ya kujitetea kabla ya kuhukumiwa vifungo hivyo atakavyovitumikia kwa pamoja, aliiomba mahakama imemuone huruma akisisitiza kwamba hakutenda makosa hayo aliyosema ushahidi wake ulikuwa wa kutengeneza.

Baada ya kutoa hukumu hiyo, hakimu huyo alisema rufaa dhidi ya hukumu hiyo ipo wazi ndani ya siku 30. [Frank Leonard blog]