Aliyeongoza Form Six: Amelelewa na Bibil; Alisoma shule ya Kata; AlidharauliwaDk. Msonde alimtaja mhitimu aliyeongoza kitaifa kwa upande wa masomo ya Sayansi kuwa ni Hassan Bakari Gwaay wa mchepuo wa Fizikia, Kemia na Hisabati (PCM) kutoka Shule ya Sekondari Tabora Boys ya Tabora.
“Ndoto yangu ni kujiunga katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ili ikibidi nikasomee masuala ya mafuta na petrol… hilo ndiyo chaguo langu,” mwanafunzi kinara katika masomo ya Sayansi, Hassan Gwaay aliiambia Nipashe katika mahojiano yake maalum akiwa kwao Mirerani, mkoani Manyara jana. 
[Imenukuliwa kutoka kwenye gazeti la NIPASHE]

Mwanafunzi aliyeongoza katika matokeo ya kidato cha sita yaliyotangazwa jana na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Hassan Gwaay ameonesha moja kati ya tunda bora lililodhihirisha faida ya kuanzishwa kwa shule za kata na Serikali ya awamu ya nne iliyoongozwa na Dk. Jakaya Kikwete.

Gwaay mwenye umri wa miaka 19 ameeleza kuwa alisoma katika shule ya kata ya Mirerani Benjamin W. Mkapa mkoani Manyara alipopata elimu ya kidato cha nne na kupata ufaulu mzuri uliomuwezesha kuchaguliwa kujiunga na shule ya wavulana ya Tabora (Tabora Boys) kuendelea na elimu yake ya kidato cha tano.

Amesema kuwa alipokuwa akisoma katika shule hiyo ya kata, wanafunzi waliokuwa wanasoma katika shule za watu binafsi zenye mazingira bora zaidi ya walikuwa wakimuonesha dharau lakini alitaka kuwadhihirishia kuwa hata katika shule hiyo anaweza kufanya vizuri zaidi yao.
“Sikujali kelele na dharau za watoto waliosoma kwenye shule za kulipia, ambao mara kwa mara walikuwa wakiibeza shule yetu. Nilipomaliza kidato cha nne, nilipata daraja la kwanza alama 10 (Division 1 ya point 10). Ndipo nilipowadhihirishia kuwa hata kwenye shule za kata watu wanafaulu,” Gwaay anakaririwa na gazeti la Jambo Leo.
Mwanafunzi huyo ambaye amelelewa na bibi yake kwa muda mrefu baada ya mama yake kufariki huku akiishi mbali na baba yake (anamsaidia), alisema kuwa baada ya kujiunga na shule ya wavulana ya Tabora kusoma masomo ya Fizikia, Kemia na Hesabu (PCM), aliweka bidii zaidi hasa baada ya kugundua kuwa wanafunzi aliokutana nao hapo wote walikuwa na akili sana.

Alisema kuwa alipofanya mtihani wa ‘Mock’ alipata Fizikia (A), Kemia (A) na Hesabu (B) na kwamba aliumia sana kuona amepata B. Aliongeza bidii hadi kuibuka na alama A kwenye mitihani yote katika Mtihani wa Taifa na kutangazwa kuwa mwanafunzi aliyeongoza.

Changamoto ya upungufu wa walimu hususan wa Sayansi katika shule nyingi za umma nchini lilimkumba pia Gwaay katika shule ya wavulana ya Tabora, lakini aliipanda ngazi hiyo ndefu kwa nguvu ya ziada bila kukata tamaa.
“Hakuwa na Mwalimu wa Fizikia pale. Tangu najiunga sikuwahi kumwona zaidi ya wakuazimwa ambaye alikuwa akija jioni na mwisho mwa wiki tu na alikuwa akija mara chache. Muda mwingi tulitumia kujisome wenyewe lakini hatukukata tamaa,” alisema.
Shule ya wavulana ya Tabora mwaka huu imerudi kwenye nafasi yake ya ubora ulioaminika miaka mingi iliyopita. Imeshika nafasi ya 5 kati ya shule zote.

------------------------

MWANAFUNZI Hassan Gwaay wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora aliyeshika nafasi ya kwanza katika watahiniwa kumi bora waliofanya vizuri kitaifa kwenye masomo ya sayansi katika matokeo ya mtihani wa kidato cha sita yaliyotangazwa jana, amesema matokeo aliyoyapata hakuyategemea.

Hassan alitangazwa kushika nafasi hiyo na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani nchini (NECTA), Dk. Charles Msonde, wakati alipokuwa akitangaza matokeo hayo.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kutoka nyumbani kwao mkoani Manyara, Hassan ambaye ni mtoto wa kwanza kuzaliwa katika familia yao, alisema anamshukuru Mungu kumwezesha kuongoza nafasi hiyo.

Hassan alisema alipata nafasi hiyo kupitia mchepuo wa PCM ambapo alikuwa akisoma masomo ya Fizikia, Kemia na Hesabu na katika matokeo ya jumla amepata daraja la 1.3
“Matokeo yamenishangaza…sikutegemea kama ningeweza kuwa mwanafunzi bora katika masomo ya sayansi kwa mwaka huu, namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kupata ufaulu wa kiwango cha juu, nimefurahi sana,” alisema Hasaan.
Alisema anaamini matokeo hayo ni mwanzo mzuri wa kumwonesha njia ya kutimiza ndoto yake ya kuwa mhandisi mkubwa nchini.
“Tangu nikiwa mdogo nilikuwa napenda sana masomo ya sayansi, lengo langu ni kuwa mmoja kati ya engineers (wahandisi) wakubwa nchini,” alisema Hassan.
Alisema pamoja na kufaulu vizuri lakini hana ndoto za kusoma katika vyuo vya nje ya nchi kwa kuwa anaamini uwezo wa elimu inayotolewa na vyuo vya hapa nchini.

Akizungumzia historia yake ya elimu, alisema alijiunga na kidato cha tano katika Shule ya Sekondari Tabora baada ya kufaulu vizuri katika Shule ya Sekondari Benjamini William Mkapa iliyopo Mererani Manyara ambako alisoma kidato cha kwanza hadi cha nne.

“Shule hiyo ni ya kata, kidato cha nne nikapata ufaulu wa divisheni 1.10, ndipo nikachaguliwa kujiunga na Tabora Boys, nikiwa shuleni Tabora mara nyingi darasani nilikuwa nashika nafasi ya nne ama ya tano,” alisema Hassan.

Alisema alipofika kidato cha sita katika mitihani ya maandalizi (mock) alipata divisheni 4.3 huku akitaja sababu kubwa ya mafanikio yake ni kujali muda na kupanga vizuri ratiba za kujisomea.
“Mimi nilikuwa nina ratiba mbili, ratiba ya kwanza iliyokuwa ikiniongoza ilikuwa ni ya shule ambayo tulikuwa tukiingia darasa kuanzia saa moja hadi saa tano na baadaye tunarudi tena hadi saa kumi jioni,” alisema Hassan.
Alisema ratiba ya pili ilikuwa ikiongozwa na yeye mwenyewe ambapo baada ya muda wa kutoka darasani saa kumi alikuwa akijisomea hadi saa 12 na kupumzika kidogo baadaye anarudi kujisomea hadi saa mbili usiku. [via gazeti la MTANZANIA]