Aliyewahi kuwa mtangazaji BBC na Mbunge Burundi, Bi. Hafsa Mossi auawa


Hafsa Mossi
Hafsa Mossi

Na GRACE MACHA, ARUSHA

MBUNGE wa Bunge la Afrika Mashariki, (EALA) wa Burundi, Hafsa Mossi, ameuawa kwa kupigwa risasi kifuani na watu wasiofahamika maeneo ya Mutanga karibu na nyumbani kwake kwenye mji mkuu wa Bujumbura, Burundi.

Mossi ambaye aliwahi kuwa mwandishi wa habari wa Shirika la Habari la Kimataifa la BBC, Idhaa ya Kiswahili alipigwa risasi leo saa nne asubuhi na kuwahishwa katika hospitali ya jeshi na kubainika kuwa amefariki dunia.

Msemaji wa Polisi wa Burundi, Pierre Nkurikiye, amenukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari akithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Taarifa zinasema kuwa mbunge huyo alipigwa risasi baada ya kusimamisha gari lake llilokwanguliwa na gari lingine na kisha watu hao kummiminia risasi na kukimbia kusikojulikana.

Wakati wa uhai wake Mossi alishika nyadhifa mbalimbali serikalini kabla ya kuwa mbunge wa EALA kuanzia Juni mwaka 2012 ambapo kabla ya hapo alikuwa Waziri wa Ofisi ya Rais anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki kwa miaka miwili kuanzia 2009 mpaka 2011.

Pia alihudumu kama Waziri wa Mawasiliano, Habari, Uhusiano na Bunge na msemaji wa Serikali 2005 mpaka 2007.

Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza amenukuliwa na vyombo vya habari akielezea mauaji hayo yametekelezwa na waoga wabaya.

Katibu Mkuu wa EAC, Liberat Mfumukeko, alituma salamu za rambirambi kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa ‘Twitter’ akielezea masikitiko yake juu ya kifo cha kiongozi huyo.

Mbunge wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Adam Kimbisa alisema kuwa wamepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha kiongozi huyo ambaye wamekuwa wakishirikiana naye katika kutekeleza majukumu ya uwakilishi wa wananchi wa EAC.

Msemaji wa serikali ya Burundi, Burundi Willy Nyamitwe alielezea masikitiko yake juu ya kifo cha kiongozi huyo ambaye alikuwa mwanachama wa chama tawala cha CNDD-FDD.

Mosi aliwahi kuwa mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Shirika Utangazaji la Uingereza (BBC).

Mossi atakumbukwa kwa kuwa mtetezi wa haki za wanawake pia ni mwanasiasa wa kwanza kuuawa tangu kuanza kwa machafuko nchini Burundi mwaka jana .

Hata hivyo, tangu Aprili mwaka 2015, Burundi imekuwa ikiandamwa na matukio ya mauaji ya kupigwa risasi ya maofisa wa juu wa jeshi akiwemo Jenerali Athanase Kararuza, Meja Didier Mihimpundu, Kanali Darius Ikurakure na Kanali mstaafu Colonel Jean Bikomagu.

Mauaji hayo yametokea siku moja baada ya sintofahamu kuibuka kwenye mazungumzo ya kutafutia suluhu mgogoro wa Burundi kutokana na hatua ya ujumbe wa Serikali ya nchi hiyo ukiongozwa na Waziri wa mambo ya nje, Alain Nyamitwa kutishia kususia.

Walitishia kususia awamu ya pili ya majadiliano hayo yaliyoanza juzi jiji hapa wakipinga hatua ya Mwezeshaji wa mazungumzo hayo, Rais Mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa ya kuwaalika watu watatu wanaotuhumiwa kuhusika na jaribio la kumpindua Rais Nkurunziza.