Bodi MSD yamfuta kazi Mkurugenzi wa Shughuli za Kanda na Huduma kwa Wateja


BODI ya wadhamini ya Bohari ya Dawa (MSD), imemfukuza kazi aliyekuwa Mkurugenzi wa Shughuli za Kanda na Huduma kwa Wateja, Cosmas Mwaifwani baada ya kupatikana na makosa huku maofisa wengine wakiondolewa kwenye nyadhifa zao na uhamishiwa idara zingine.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo kwa vyombo vya habari Mwaifwani ameachishwa kazi kuanzia Julai 8 mwaka huu. Februari 15 mwaka huu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu alitoa maelekezo kwa Bodi ya wadhamini wa Bohari ya Dawa (MSD) kuwasimamisha kazi Wakurugenzi wanne (4) wa Taasisi hiyo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zilizokuwa zinawakabili.

Wakurugenzi waliokuwa wamesimamishwa ni pamoja na Mkurugenzi wa Shughuli za Kanda na Huduma kwa Wateja Cosmas Mwaifwani, Mkurugenzi wa Fedha na Mipango, Joseph Tesha, Mkurugenzi wa Ugavi, Misanga Muja na Mkurugenzi wa Ununuzi, Heri Mchunga.

Hatua ya kufukuzwa kazi kwa Mwaifwani kunanokana na kukamilika kwa uchunguzi juu ya Wakurugenzi hao.

Kikao cha bodi hiyo kilichofanyika Julai 8 mwaka huu kilibaini kuwa Heri Mchunga ameonekana hana makosa, hivyo anarudi kazini kuanzia Julai 12 mwaka huu ambapo amehamishiwa Kurugenzi ya Ugavi kuwa Mkurugenzi wakati Joseph Tesha anarejeshwa kazini kuanzia tarehe hiyo lakini uteuzi wake wa nafasi ya Ukurugenzi umetenguliwa, hivyo atapangiwa kazi nyingine.

Katika hatua nyingine bodi hiyo imemrejesha kazini Misanga Muja aliyekuwa Mkurugenzi wa Ugavi hata hivyo uteuzi wake wa nafasi ya Ukurugenzi umetenguliwa na atapangiwa kazi nyingine.

Maamuzi ya Bodi ya Wadhamini yamezingatia Kifungu cha 12(a) cha Sheria ya Bohari ya Dawa
Na.13 ya mwaka 1993 ikisomwa pamoja na Kanuni ya 7 na ya 73(2) za Utumishi wa MSD