Dah! Anakesha kuwalinda wanawe maalbino "kuna muda napatwa na machungu watoto wangu wanaponiuliza..."

Mwanje na mke wake Florence wakiwa na watoto wao maalbino.
Na Leonard Msigwa

Ni mwendo wa saa nne toka jiji la Kampala nchini Uganda hadi kuyafikia makazi ya bwana Mwanje na wake zake wawili Lynda na Florence. Ni katika makazi haya bwana Mwanje ndipo anaishi na watoto wake nane wanaokadiriwa kuwa na miaka mitano hadi kumi na tatu huku watano kati yao wakiwa na ulemavu wa ngozi.

Na watoto wote watano wenye ulemavu wa ngozi amezaa na mkewe mkubwa Florence, wataalam wanaeleza kuwa ulemavu wa ngozi unatokana na upungufu wa madini ya melanin yanayohusika kuweka rangi ya ngozi, macho na nywele.

“Mara ya kwanza kupata mtoto mwenye matatizo ya ulemavu wa ngozi niliogopa sana, sikujua nini nitafanya, mwishowe niliamua kumpenda, nilimpenda zaidi” alisema bwana Mwanje.


Katika familia nyingi kumpata mtoto mwenye ulemavu wa ngozi ni tatizo, wengi wao huwaficha ndani kwa kuogopwa kuchekwa na majirani, hii inatokana na imani potofu inayoenezwa dhidi ya watoto wenye ulemavu wa ngozi. Kuna baadhi ya wanaume ambao huwatelekeza wake zao baada ya kuzaliwa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi” kuna mambo mengi yasiyo ya kweli katika jamii yangu kuhusiana na wanangu watano kuwa walemavu wa ngozi, wanasema nilimcheka mtu mwenye ulemavu wa ngozi nilipokuwa kijana na akanipa laana na ndiyo sababu ya wanangu kuwa na ulemavu wa ngozi” alisema Florence mke mkubwa wa bwana Mwanje.

Kumekuwa na imani potofu kuhusu watu wenye ulemavu wa ngozi katika nchi zote za Afrika Mashariki, wapo wanaoamini miili ya watu wenye ulemavu ina nguvu ya kutajirisha watu maskini na kuwa matajiri wakubwa. Pia wapo wanaoamini wao ni mizimu ya kweli na siyo binadamu.

Katika nchi ya Tanzania na Malawi kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya kutekwa na baadaye kuuwawa kwa watu wenye ulemavu wa ngozi na baadhi wakikatwa viungo vyao wa mapanga wangali wazima, kifupi watu wenye ulemavu wanaishi kwa hofu kubwa kulingana na imani hizo kandamizi na potofu.


Nchini Uganda hali tofauti na nchini Tanzania na Malawi lakini ubaguzi wa wazi wa watu wenye ulemavu nchini Uganda ni jambo la kawaida. Katika shule nyingi wanafunzi wanagoma kukaa na watu wenye ulemavu wa ngozi kwenye dawati moja.

“Nilitaka wanangu wapate elimu bora, nikaamua kuwapeleka shule bora lakini tatizo shule iko mbali na makazi yangu, hivyo nilihofia wanangu wanaweza kutekwa. Kwasasa wanasoma shule ya kawaida iliyo jirani na makazi yangu” alisema bwana Mwanje.


“Jambo lililowahi kunitia hofu zaidi, siku moja mwanagu Robert na wenzake walikuwa wakicheza jirani na shamba langu la mpunga. Mpaka jua linazama walikuwa bado porini wakicheza ghafla walimwona mtu kajificha na akaanza kuwafukuza hali iliyosababisha kila mmoja akimbilie uelekeo wake. Robert alikimbilia uelekeo wake na wenzake uelekeo mmoja, kutokana na kelele za watoto yule mtu naye alikimbia na mpaka leo hatutajua alikuwa nani na lengo lake lilikuwa nini.” Alisema bwana Mwanje huku akionesha hali ya huzuni na wasiwasi.

“Tangu tukio hilo litoke natumia muda mwingi kukaa jirani na watoto wangu kuhakikisha usalama wao. ” “Kuna muda napatwa na machungu watoto wangu wanaponiuliza kwa nini wako tofauti na sisi, nawajibu kuwa hakuna kitu kibaya, wote tupo sawa ndani ya miili yetu.