Dodoma ni mbali kutoka wapi?


RAIS John Magufuli amewatangazia vita watendaji wote wa serikali. Agizo lake la kutaka serikali ihamie Dodoma ifikapo Septemba mwaka huu kwa sasa limewafanya watendaji wengi wapatwe na homa za matundo ya ghafla.

Naam. Suala la kuhamia Dodoma, ambalo Rais Magufuli ameamua kulivalia njuga safari hii, ni jipu sugu ambalo limedumu kwa miaka 42 mpaka sasa.

Ni jipu kwa sababu watendaji wengi katika serikali zilizotangulia walikuwa wanatumia fursa hiyo kupiga dili ndefu za kimya kimya, ambayo zinaidhinishwa na zina Baraka zote mpaka kwenye Bajeti.

Siyo siri kwamba miaka 42 ni mingi kwa umri wa binadamu, lakini ni kipindi ambacho Serikali imeshindwa kutekeleza jambo moja tu – kuhamisha makao makuu yake kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma huku siasa ikitawala na kodi za wananchi zikiendelea kuteketea kwa bajeti ya ‘kufanikisha’ ustawishaji wa mji huo.

Tangu wazo la kuhamisha makao makuu kwenda Dodoma lilipokuja mwaka 1973 baada ya vikao kadhaa vya chama tawala cha wakati huo Tanzania Bara – Tanganyika African National Union (TANU) – idara karibu zote za serikali zimeshindwa kutekeleza uamuzi huo ambao baadaye ulitungiwa Sheria iliyounda Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu (CDA).

Katika awamu nne za serikali zilizopita, kila moja imekuwa ikitoa sababu kadha wa kadha, huku ikijitahidi kuuendeleza mji wa Dodoma, lakini uthubutu wa kweli wa kuhamisha makao makuu haujaonekana zaidi ya kushuhudia kauli za kisiasa.

Visingizio visivyo na kichwa wala miguu ndivyo vilivyotawala na kukwamisha zoezi hilo ambalo siyo la kisiasa.

Wapo wanaosingizia kwamba mji wa Dodoma hauna miundombinu mizuri, lakini ni hao hao ambao kila mwaka huketi Bungeni kupitisha Bajeti kwa ajili ya CDA kuendeleza mji huo.

Barabara zimejengwa, ingawa siyo kwa wingi, lakini hakuna anayeweza kusingizia kwamba amechelewa kwa ajili ya foleni, maana atakuwa muongo.

Viwanja vimepimwa vya kutosha, maeneo ya umma yametengwa, lakini badala ya wakubwa hao kuhamia huko wengi wananunua viwanja vyao binafsi na kuendelea kuipuuza sharia inaiyowataka wahamishie serikali Dodoma.

Miundombinu mingi imeboreshwa katika mji huo na huduma za kijamii zinapatikana kwa urahisi tofauti na miaka 20 iliyopita kabla hata Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania halijahamishia vikao vyake huko mwaka 1996 kutoka kwenye ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.

Wapo baadhi ya wanaogoma kuhamia Dodoma ambao wanasingizia kwamba eti ‘Dodoma ni mbali’ – hivi ni mbali kutoka wapi? Kutoka Dar es Salaam? Wanapenda kupunga upepo wa baharini au kuna sababu nyingine?

Asilimia karibu 100 ya watendaji wa serikali siyo wenyeji wala wazaliwa wa Dar es Salaam, bali wametoka kila pembe ya nchi hii, lakini ndio hao hao ambao wamekwenda Dar es Salaam kikazi kutoka Karagwe, Kambanzite kule Sumbawanga, Kyela, Lituhi na Mtwara ambao leo hii wanasema Dodoma ni mbali. Hawauoni umbali wa Dar es Salaam, bali umbali wa Dodoma!

Kama ambavyo mtu anaweza kwenda Ileje kufanya kazi kutoka Pangani, ndivyo ambavyo anaweza kufanya kazi akiwa Dodoma, ambayo kisheria ndiyo makao makuu ya serikali.

Wanasingizia umbali na miundombinu duni kwa sababu tu wanaona hawatapata tena fursa ya kupiga dili na kupata posho, hakuna ingine cha ziada.

Kuhamisha makao makuu ni moja ya njia sahihi za ujenzi wa dola na utambulisho wa kitaifa, lakini kutokana na mchakato wake kuwa mkubwa, viongozi wengi huhofia kuchukua hatua kutokana na gharama kubwa za kifedha, kijamii, na hata kisiasa.

Mara nyingi miji mipya mikuu hushindwa kustawi kwa sababu hulazimu serikali kutumia gharama kubwa zaidi kuhamisha serikali yote na idara zake,” anaongeza.

Ni kweli, majaribio mengi ya kuhamisha makao makuu yamekwama ama kudumaa na kubaki kama magofu tu ya mawazo sadifu ya wahenga, kama ilivyo kwa suala la Tanzania.

Kuanzia mwaka 1950 hadi 2000, nchi 13 zimeshabadilisha makao yao makuu ambazo ni Brazil (1956 – kutoka Rio de Janeiro kwenda Brasilia), Mauritania (1957 – kutoka Saint Louis (Senegal) kwenda Nouakchott), Pakistan (1959 – kutoka Karachi kwenda Islamabad), Botswana (1961 – kutoka Mafeking kwenda Gaborone), Libya (1963 – kutoka Benghazi kwenda Tripoli), Malawi (1965 – kutoka Zomba kwenda Lilongwe), na Belize (1970 – kutoka Belize City kwenda Belmopan).

Nyingine, mbali ya Tanzania, ni Nigeria (1975 – kutoka Lagos kwenda Abuja), Ivory Coast (1983 – kutoka Abidjan kwenda Yamoussoukro), Ujerumani (1990 – kutoka Bonn kwenda Berlin), Kazakhstan (1997 – kutoka Almaty kwenda Astana), na Malaysia (2000 – kutoka Kuala Lumpur kwenda Putrajaya).

Mara baada ya Dodoma kuwa makao makuu, mnamo Oktoba 1973 Sir George Kahama akateuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa CDA na Chifu Adam Sapi Mkwawa akateuliwa kuwa waziri wa kwanza wa wizara mpya ya Ustawishaji Makao Makuu ikiwa chini ya Ofisi ya Rais.

Wachunguzi wa mambo wanasema, gharama za uhamishaji huo zilikuwa chini kwa wakati ule lakini ghafla zikaanza kupanda, hata pale Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, aliposema hakuna fedha zaidi zitakazoongezwa kwenye gharama hizo kutoka kwenye bajeti ya serikali.

Kwa kadiri mataifa ya magharibi yalipoufahamu utawala wa Nyerere na tabia zake, ndivyo kadiri uamuzi wa kuhamisha makao makuu ulivyozidi kupata kigugumizi na kutegemea kudra tu.

Serikali ya awamu ya kwanza ilihakikisha sekta ya miundombinu inapewa kipaumbele katika bajeti ya CDA. Wizara na taasisi za umma zikapewa miaka mitano ziwe zimeshahamishia ofisi zao mjini Dodoma, kwa kuanzia na Ofisi ya Waziri Mkuu, wakati huo akiwa Rashid Kawawa. Baadaye Ofisi ya Rais (Ikulu) ikajengwa Chamwino.

Inaonekana hakukuwa na dhamira ya dhati ya kuhamia huko kwani Wizara ya Ujenzi (sasa Miundombinu) badala ya kujenga ofisi yake mjini Dodoma, mnamo mwaka 1979 ikaamua kukarabati jengo la makao makuu yake na kuwa la ghorofa pale Holland House. Na naamini mpaka leo hii wizara ya Miundombinu haina mpango wala ndoto za kuhamia Dodoma.

Kwa mujibu wa Sensa ya Taifa ya mwaka 2012, Wilaya ya Dodoma Mjini ina wakazi 410,939 badala ya 324,347 kwa sensa ya mwaka 2002, ukilinganisha na wakazi takriban milioni 5 wa sasa wa Dar es Salaam.

Wizara chache zina ofisi mbili; moja mjini Dodoma (‘makao makuu jina tu’) na Dar es Salaam. Wizara hizi ni Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi; Sera, Uratibu na Bunge), Wizara ya Fedha na Uchumi; Wizara ya Nishati na Madini; Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika; Wizara ya Mipango; na Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Mawaziri karibu wote wana nyumba zao (Rest House) kule Area D na nyingine Kilimani, sijui kisingizio ni nini?

CDA chini ya Sir George iliamini kulikuwa na dhati kubwa ya kuhamia Dodoma kwa sababu tayari viongozi wachache kama Mwalimu Nyerere na Rashid Kawawa walikuwa wamekwishahamia. Ucheleweshaji huu wa kuhamia huko umeisababishia serikali hasara kubwa kwa kuongeza bajeti yake kila mwaka.

Mtumishi wa umma anapangiwa Dodoma kama kituo chake kipya cha kazi. Lakini kila wakati lazima asafiri kwenda Dar es Salaam kumwona waziri ama katibu mkuu ama wizara nyingine, hivyo kuongeza gharama kubwa ambazo ni mzigo kwa serikali.

Kuhamia Dodoma limekuwa tatizo kubwa kwa maofisa wengi wa serikali. Sababu za kuhamia Dodoma kwa siku za karibuni nazo zimeonekana kutokuwa na maana ama nguvu kubwa kwa baadhi ya watu tofauti na wakati ule. Fedha nyingine zimetolewa kwa ajili ya mji huo ambao unaendelea kujengwa.

Maswali mengi ya msingi yanaendelea kujitokeza kuhusu dhamira halisi ya serikali kuhamia huko wakati tayari ilikwishatangaza kujenga nyumba 80 za wizara kadhaa jijini Dar es Salaam.

Mtu angeweza kufikiri kwamba, lingekuwa ni wazo jema kwa serikali kujenga nyumba hizo 80 mjini Dodoma kama kuonyesha nia yake ya kuhamishia serikali huko.

Kila mwaka wa fedha, Serikali kupitia Wizara ya Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa hutenga mamilioni ya fedha za walipa kodi kwenye bajeti kwa ajili ya CDA.

Aliyekuwa Waziri wa Nchini katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Phillip Marmo, alisema mwaka 2008 kwamba serikali ilikuwa imetenga Shs. 2.4 bilioni kwa ajili ya uendelezaji makao makuu kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2008/09, kulinganisha na Shs. 400 milioni za bajeti ya mwaka 2005/06. Fedha hizo, alisema, zingetumiwa na CDA kwa ajili ya upimaji wa viwanja 10,000 huko Nzuguni, Mnadani na Mkalama na tayari vimekwishapimwa.

Bunge la Bajeti kila mwaka hutumia zaidi ya Shs. 1.2 bilioni, ambazo ni fedha nyingi kwa nchi ambayo wananchi wake wako katika ufukara.

Mara nyingi fedha hizi hufujwa na maofisa wasio waadilifu na pengine ndiyo maana wamekuwa wakikwepa suala la kuhamia Dodoma kwa kuwa hawawezi kuzipata tena, jambo ambalo wakati fulani limewafanya wakurugenzi wa CDA kuachia ngazi kutokana na ubadhirifu.

CDA imetumia fedha nyingi kuwalipa wataalamu kutoka Canada kukagua mpango-mji wa makao hayo makuu. Balozi mbalimbali zilikwishapewa maeneo ya kujenga ofisi zao mjini Dodoma, lakini badala yake zikaamua kujenga kwenye mitaa mbalimbali hasa Garden Avenue mjini Dar es Salaam. Nyingine ziko Masaki upepo unakovuma.

Mtu utajiuliza, kwa nini tutumie miaka mingi kiasi hicho kuhamisha makao makuu? Hivi tuseme Tanzania inasubiri Mwalimu Nyerere afufuke kutoka kwa wafu na kutuhimiza tuhamie Dodoma? Au tunayapuuza mawazo ya Mwalimu? Kuna maswali mengi ambayo yanahitaji majibu.

Viongozi wetu hawana budi kutambua kwamba taifa bado lina hamu ya kuona makao makuu yanahamishiwa Dodoma haraka iwezekanavyo na ndiyo maana ninasema rais wa awamu ya tano lazima awe na ujasiri wa kuihamishia serikali Dodoma.

Serikali kuhamishia makao makuu Dodoma kutasaidia pia maendeleo kwa mikoa ya jirani kama Singida, Iringa, Tabora, Manyara na Shinyanga ambayo kwa miaka mingi imeonekana nyuma kimaendeleo.