Imani anaainisha mambo 4 ya msingi kuyajua kabla hujaacha kazi kuuendea ujasiriamali

Inawezekana umechoshwa sana na kazi unayoifanya na una hamasa kubwa ya kutaka kuwa mjasiriamali kwa kujiajiri. Kama hayo ndiyo mawazo yako, kwanza hongera sana, kwani unachagua njia sahihi itakayokufikisha kwenye ndoto zako za kweli.

Nasema hivyo kwa sababu, watu wenye mafanikio makubwa duniani ni wajasiriamali na si vinginevyo. Lakini pamoja na kwamba umekuwa umechagua njia sahihi ya kukufikisha kwenye ndoto zako, ipo haja ya wewe kujua mambo ya msingi kwenye ujasiriamali kabla hujaingia huko.

Kwa kujua mambo hayo itakusaidia wewe kujiwekea misingi imara itakayokufanya usitetereke. Naamini kwa kusoma makala haya, itakusaidia usiwe na maamuzi ya kukurupuka ikiwa upo kazini na unataka kuachana na kazi yako na kuingia kwenye ujasiriamali moja kwa moja.

Sasa bila kupoteza muda, twende pamoja kujua mambo ya msingi unayotakiwa kujua kuhusu ujasiriamali, kabla hujaacha kazi.

1. Ujasiriamali unataka kujituma sana

Hakuna ubishi katika hili kama umemua kuwa mjasiriamali wa kweli ni lazima kujituma sana kila siku. Bila kufanya hivyo hutafika kilele cha mafanikio. Kuna wakati unatakiwa kufanya kazi kuliko kawaida ili kuweza kufikia kilele cha mafanikio yako.

Kama upo kazini na unataka kuingia kwenye ujasiriamali huku ukiamini utakuja kujiachia sana utakuwa unajipoteza. Hivyo, unachotakiwa kujua kama una mpango wa kuacha kazi na kuingia kwenye ujasiriamali, elewa unaingia kwenye kambi inayokutaka kujituma sana ili kuweza kufanikiwa.

Kujituma ni muhimu sana kwa mafanikio ya mjasiriamali yeyote.

2. Ujasiriamali hautakupa uhuru wote

Kama ilivyo kwa mwajiri wako kuna wakati anaweza kukubana, halikadhalika nao ujasiriamali uko hivyohivyo. Hata kama unafanya kazi ya kwako kuna mambo ambayo huwezi kuwa huru kwa asilimia zote, kwani ukifanya hivyo utapoteza mengi.

Kuna kipindi ambacho utatakiwa kuamka asubuhi na mapema. Pia kuna wakati itatakiwa kujinyima baadhi ya mambo ili kufikia mafanikio yako. Hiyo yote hutokea, kwani bila kufanya hivyo, utakaa sana kwa muda mrefu eneo moja bila kufanikiwa, kwa sababu utakuwa kama unazunguka tu.

3. Ujasiriamali unataka juhudi ya kujifunza kila siku

Ili uweze kuwa mjasiriamali bora na mwenye mafanikio ni lazima ukubali kujifunza kila siku. Kila wakati ubongo wako ni lazima upokee vitu vitakavyokusaidia kukubadilisha wewe ili ukubaliane na hali yoyote ya shindani.

Mjasiriamali wa kweli ni yule anayekubali kujifunza na kurekebisha udhaifu wake pale unapohitajika. Kujifunza huko hakuishii kwenye maandishi peke yake ila mpaka kwenye vitendo. Binafsi jiulize upo tayarii kujifunza kila siku? Kama ni ndiyo endelea na safari yako ya ujasiriamali bila kuchoka.

4. Hutakiwi kukata tamaa mapema

Unapoamua kuwa mjasirimali na kuchagua njia yako mwenyewe, kitu cha kimojawapo cha cha kukijua, ni kwamba hutakiwi kukata tamaa mapema. Kuna wakati mambo na mipango yako inakuwa inakwenda hovyo sana lakini unatakiwa kuvumilia bila kuchoka.

Ukiingia kwenye ujasiriamali halafu huku ukawa una roho ile ya kukata tamaa mapema hutafika popote. Kwa hiyo ingia kwenye ujasiriamali ukiwa tayari kwa lolote. Ikitokea hasara vumilia na kisha chukua jukumu la kuweza kusonga mbele bila kukata tamaa.

Hayo ndiyo mambo ya msingi unayaotakiwa kujifunza kabla hujaingia kwenye ujasiriamali. Chukua hatua sitahiki za kubadili maisha yako na endelea kujifunza kupitia DIRA YA MAFANIKIO kila siku.

----

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE
Ni wako rafiki,
Imani Ngwangwalu,
Simu; 0713 048035,
Email: [email protected]