Kauli ya Paul Makonda kuhusu ujumbe uliowekwa kwenye mitandao ya kijamii


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akizungumza kipindi cha Power Breakfast ya Clouds FM na 360 ya Clouds Tv juu ya watu ambao wanaotengeneza akaunti bandia za mitandao mbalimbali kupitia jina lake amesema:
“Kwanza wanapaswa kujua kuwa sina account ambayo inanza na cheo changu hivyo account zote zangu zimeandikwa kwa jina langu Paul Makonda sio vingine hivyo kila mtu anapaswa kuwa makini na hilo.” 
Anasema agizo lililowekwa katika mitandao ya kijami kuwa wananchi wasiokuwa na kazi watakwenda jela, ni batili na siyo la akaunti yake bali yeye ameagiza Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kuhakikisha kuwa wanafanya uhakiki wa wakazi wao nyumba kwa nyumba kwa ajili ya usalama wa maeneo wanayokaa.

Anataja kuwa kutokana matatizo yaliyopo kamwe hataacha kupambana na mafisadi katika Halmashauri zote tatu, wauza dawa za kulevya "unga", wafanyabiashara wa shisha na mashoga.

Hivyo aliwataka:
wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam kuwa makini na kufuata maelekezo ya wenyeviti mitaa amabayo nimewapa hili tuweze kuimarisha ulinzi kuanzi ngazi ya chini kabisa.
Makonda, amesema tangu alipotangaza kuanza kukamatwa kwa mashoga, amebaini kuna mkakati unawaohusisha watu hao zaidi ya 150 kutaka kumwangamiza.

Alisema kuwa baada ya kubainika kwa mipango hiyo, mashoga wanane wamekamatwa na Jeshi la Polisi kwa hatua zaidi.
“Lazima watu wajue jitihada na harakati za kusimamia katiba na usawa hapa nchini. Hakuna anayezipenda, vita inakuwa kubwa… Nimebaini kuwa mashoga zaidi ya 150 waliketi katika baa moja Kinondoni wakipanga njama za kunimaliza kwa namna moja ama nyingine, lakini kutokana na taarifa za kiintelijensia, watu kadhaa, wengi wao wakiwa ni mashoga wameshakamatwa,” alisema Makonda.
Akizungumzia ajira, alisema kuna mpango wa kuwachukua vijana zaidi ya 1,200 ambapo watapatiwa mafunzo ya ujasiriamali ambao watapatikana kwa uchambuzi maalum.
“Tuna mkakati wa kuwachukua vijana zaidi ya 1,200 kwa ajili ya kuwapeleka katika mafunzo ya ujasiriamali, lakini ni lazima tuwatambue kwanza watu hao,” alisema.
Alidokeza kuwa kuna mpango wa kupanua muda wa kufanya biashara jijini tangu asubuhi hadi saa nne za usiku ili kuwapatia watu huduma kwa muda mrefu na kwamba kilichotakiwa ni kuimarishwa kwa usalama ikiwa ni pamoja na kuongeza taa sehemu mbalimbali za jiji.

Mambo mengine aliyozungumzia ni dhamira ya kuwawezesha walimu wa mkoani kwake waanze kusafiri bure katika mabasi ya mwendo kasi na kutowapa pesa ombaomba mitaani ili kuwafanya waondoke jijini.

Kuhusu maovu mbalimbali yanayofanyika jijini, Makonda alishutumu ushoga, utapeli na uvutaji wa madawa ya kulevya ikiwa ni pamoja na shisha.
“Ushoga umepingwa na vitabu vya dini na hakuna sheria inayoruhusu ushoga, kwa hili najua watu watanitukana sana lakini nguvu niliyo nayo hakuna wa kunisimamisha,” 
alisisitiza huku akiwaonya watu wanaojiingiza katika utapeli kwa kutumia majina ya watu wengine, likiwemo jina lake.