[update] Kuna huyu kaelekezewa bunduki, analabuliwa, anataja ndugu zake wako Magomeni


Anasema, “Nakaa Magomeni mtaa wa Chem Chem na Idrisa kwa hiyo Mwambieni Juma, mama yangu anaitwa Rukia Daudi, baba yangu anaitwa Akida anakaa Idrisa na Chem Chem mwambieni Juma amekula hela za watu, mimi kaniweka 'guarantor' (bondi ). Mma yangu anaitwa Rukia Daudi, mama yake Juma anaitwa Mariamu Rauwa. Kwa hiyo Juma afanye arudishe hela za watu. Juma anakaa Kunduchi.”

______________________

*Mtanzania awekwa rehani Pakistan

Na Jonas Mushi, Dar es Salaam - Gazeti MTANZANIA

NI biashara haramu ya unga, ndivyo tunavyoweza kusema baada ya kijana Mtanzania aliyejitambulisha kwa jina la Adamu Akida, mkazi wa Magomeni jijini Dar es Salaam kudai kutekwa nyara na kundi la maharamia nchini Pakistan.

Katika kile kinachoonekana kuwa ni dhuluma za kibiashara, inadaiwa kuwa Adamu alichukuliwa na mfanyabiashara mmoja anayejihusisha na biashara ya mihadarati, aliyemtaja kwa jina moja la Juma mkazi wa Kunduchi Dar es Salaam na kumweka rehani kwa maharamia hao, kwa ahadi kwamba angemfuata baada ya kumalizana nao kibiashara.

Taarifa zilizopatikana kwa watu wa karibu na Adamu waishio Dar es Salaam, walisema kijana huyo alikwenda na mfanyabiashara huyo nchini humo, lakini baadaye alimwacha katika mikono ya maharamia hao kama dhamana ili baadaye awapelekee fedha zao.

Akitoa maelezo yake kwenye video ya sekunde 33 ambayo ilianza kusambaa juzi katika mitandao ya kijamii, Adamu anasikika akiomba msaada huku watu waliokuwa wamevalia mavazi ya ‘kininja’ wakiwa wamemshikia mitutu ya bunduki upande wa kushoto na kulia.

Katika video hiyo, kijana huyo alipofika katika eneo la kuanza kutaja mahali alipo watu hao walianza kumshambulia kwa mateke na ngumi, huku wakiahidi kutoa video nyingine ikionesha akiwa anachinjwa, iwapo fedha hazitatumwa.

Katika maelezo yake mafupi, Adamu alisema yupo Garita nchini Pakistani ambako aliachwa kama dhamana na mfanyabiashara huyo ambaye ni mkazi wa Kunduchi, jijini Dar es Salaam.

Kijana huyo alisikika katika video hiyo akitaja majina ya wazazi wake na eneo wanaloishi jijini Dar es Salaam pamoja na jina la mtu huyo aliyemweka rehani ughaibuni.
“Nakaa Magomeni Mtaa wa Idrisa na Chemchem, Mama yangu anaitwa Rukia Daudi na baba yangu anaitwa Akida namwomba Juma ambaye mama yake anaitwa Mariamu alipe hela za watu kaniweka ‘Gerenta’ huku Juma anakaa Kunduchi,” alisikika kijana huyo akisema katika video hiyo huku watu hao wakimpiga alipoanza kutaja eneo alipo.

MTANZANIA yafika nyumbani kwao

Kutokana na video hiyo, gazeti hili lilifanya uchunguzi ili kubaini ukweli wa tukio hilo, ambapo lilifika Magomeni nyumbani kwao na Adamu na kukutana na mmoja wa ndugu zake ambaye alithibitisha taarifa hizo.

MTANZANIA lilifika Mtaa wa Idrisa na Chemchem nyumba namba 3 Kata ya Magomeni Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, ambapo majirani wa wazazi wa Adamu walisema wazazi wa kijana huyo wamehama na kumwacha baba yake mdogo aliyefahamika kwa jina la Kessy Baharia.

Baada ya kubisha hodi katika nyumba hiyo alitoka mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Khadija Katundu, ambaye ni mke wa Baharia.

Baada ya kuulizwa kama anamfahamu Adam ambaye ametekwa nchini Pakistani, Khadija alikiri kumfahamu na kusema kuwa ni mtoto wa shemeji yake, Akida (baba wa Adamu).

Mama huyo alisema, kwa sasa mzee Akida haishi katika nyumba hiyo kwani alishaiuza na kuhamia Bagamoyo mkoani Pwani.
“Hapa ni nyumbani kwao Adamu kwa sababu alizaliwa hapa na kukulia hapa, lakini baadaye nyumba hii iliuzwa na aliyenunua ni baba yake mdogo ambaye ndiye mume wangu,” alisema Khadija.
Maisha yake
Alipoulizwa wanapoishi wazazi na ndugu wa kijana huyo alisema baada ya nyumba hiyo kuuzwa uliibuka mgogoro baina ya ndugu hao na kusababisha wazazi wa kijana huyo kuondoka bila kuaga na kwamba hawana mawasiliano hadi sasa zaidi ya kusikia kuwa walihamia Bagamoyo.

Kuhusu anavyomfahamu Adamu, Khadija alisema kijana huyo ni kinyozi na ana mke na watoto wawili ambao walikuwa wanaishi bonde la Mkwajuni ambalo hivi sasa nyumba katika eneo hilo zimebomolewa, hivyo kwa sasa hajui mahali wanapoishi.

Polisi wafika

Taarifa za mkanda huo wa video zimelishtua Jeshi la Polisi ambapo tayari askari polisi jana walifika katika nyumba hiyo na kumuhoji mama huyo kuhusu Adamu na kumwonyesha video hiyo.
“Nilikuwa nasikia tu lakini sikuamini sana lakini leo (jana) askari walifika hapa na kunihoji na wakanionyesha video hiyo ndiyo nikaamini kuwa ni kweli Adamu ametekwa,” alisema Khadija.
Kuhusu watu waliotajwa na kijana huyo kwa jina la Juma na mama yake Mariamu, alisema hawafahamu watu hao.

Akielezea hisia zake baada ya kupata taarifa za kijana huyo alisema anasikitika sana na kwamba kijana huyo yupo katika hatari ya kuuawa kama suala hilo halitapewa uzito na kufuatiliwa kwa kina.
“Kwakweli nimeshtushwa sana na taarifa hiyo na nilivyomwona Adamu yupo katika hatari ya kuuliwa kama hatofuatiliwa lakini naamini kwa sababu suala hili limekwisha enea dunia nzima ufumbuzi wake utapatikana na wazazi wake watajulikana walipo,” alisema Khadija.
MTANZANIA ilipomtafuta Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk. Augustine Mahiga, hakupatina. Hata hivyo mmoja wa maofisa wa Kitengo cha Habari katika wizara hiyo, alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwani yupo likizo.
“Mimi niko likizo na leo ni ‘wekiend’ (mwisho wa wiki) binafsi siwezi kulisemea suala hilo sina taarifa rasmi juu ya suala hilo,” alisema ofisa huyo ambaye aliomba asitajwe jina lake gazetini.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba hakupatikana kwani simu yake iliita kwa muda mrefu bila kupokewa na baadaye alituma ujumbe mfupi wa simu kwamba yupo kikaoni.

Hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu ili kutoa ufafanuzi kuhusu suala hilo hakujibu hadi tunakwenda mitamboni.

---------------------------------

Gazeti la MTANZANIA Julai 18, 2016

Timu ya MTANZANIA ilipiga kambi jana katika eneo la Magomeni, Mtaa wa Idrissa, ambako pamoja na mambo mengine, ilifanikiwa kuzungumza na kaka wa Adamu aliyejitambulisha kwa jina la Hemed Abdallah (si jina lake halisi).

Akisimulia mkasa huo, alisema miezi minane iliyopita, Adamu alikwenda kwa kaka yake ambaye ni mtoto wa mama yake mdogo aliyetambulika kwa jina la Juma, na kuomba msaada wa mtaji kwani kazi yake ya kinyozi haikuwa ikilipa na hali ya maisha ilikuwa ngumu.

Baada ya kueleza shida yake hiyo, kaka yake huyo (Juma) alimuhoji kama yupo tayari kwa ajili ya kutafuta maisha nje ya nchi, na Adamu alikubali kufanya kazi ya aina yoyote ili mradi aweze kupata pesa.
“Adamu kwa sasa ameshikiliwa kwa muda wa miezi minane, hatujui kama alikuwa ameingia katika janga hili hadi pale tulipoona video zake katika mitandao ya kijamii. Hapa aliyepo ni baba yake mdogo, Kessy Baharia na baba yake mzazi yupo Bagamoyo Mlingotini, ndiko anakoendelea na maisha yake.
“Awali alikwenda kwa kaka yake mtoto wa mama yake mdogo anaitwa Juma na kuomba asaidiwe mtaji kwani amekuwa na maisha magumu sana. Baada ya hali hiyo aliambiwa kuna safari ya kwenda Pakistan ambayo waliondoka wakiwa wameambatana watu watatu pamoja na Juma na kijana mwengine ambaye jina lake limenitoka, ila anaishi Kinondoni.
“Walipofika kule, Juma akachukua mzigo akiwa na yule kijana wa Kinondoni, huku Adamu akiachwa Pakistan kwa maelezo kuwa baada ya siku tano atakuja nchini na mzigo mwingine. Muda wote hata tukihoji alipo Adamu tunaambiwa yupo anaendelea na kazi huko aliko ana angerudi mwezi wa tisa nane.
“Sasa hii video ndiyo imetupa picha halisi ya Adamu, maskini sijui kama tutampata akiwa hai. Hata hivyo kwa kipindi cha hivi karibuni, tulikuwa tukishangazwa na mwenendo wa Juma kwani amekuwa na fedha nyingi sana hadi kufikia kuwajengea nyumba dada zake pamoja na kuwanunulia magari,” alisema Abdallah huku akibubujikwa na machozi.
Mke wake

Inaelezwa kuwa mke wa Adamu ambaye alikuwa akiishi Mtaa wa Sunna, Magomeni, alihamia Kijitonyama.

Kwamba alihamishwa na shemeji yake, Juma ambaye ndiye aliyempangia nyumba nyingine Kijitonyama.
“Katika suala hilo, tuna shaka kuwa hata mke wa Adamu anajua kinachoendelea, maana miezi mitatu iliyopita alihama Magomeni na kuhamia Kijitonyama, tena huku akisema mume wake karibu anarejea nchini.
“Lakini baada ya video kuanza kuonekana, sasa hata kupatikana hapatikani, na hatujui amehamia nyumba gani huko Kijitonyama,” alisema Abdallah.
Serikali ya Mtaa

Akizungumza na MTANZANIA, Mwenyekiti wa Srikali ya Mtaa wa Idrissa, Issa Mpangile, alisema kuwa jana askari kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi walifika katika ofisi yake na kumtaka waongozane kwenda katika nyumba ya baba mdogo wa Adamu.

Alisema walipofika nyumbani kwa Kessy Baharia, ambaye ndiye baba mdogo wa Adamu, polisi walichukua maelezo yake na baadaye wakarudi katika ofisi ya Serikali ya Mtaa kuchukua maelezo ya mwenyekiti huyo.

Akizungumza kuhusu kijana huyo, Mpangile alisema kuwa ni mzaliwa wa mtaa huo, lakini baadaye alihamia Mtaa wa Suna ambao ni jirani na Mtaa wa Idrissa, Kata ya Magomeni.

Alisema wakati kijana huyo anahama mtaa huo, alikuwa bado ni kinyozi na hakuwa na rekodi ya kusafiri kwenda nje ya nchi.
“Wakati Adamu anahama Mtaa wa Idrissa, alikuwa bado ni kinyozi na hakuna rekodi kwamba alikuwa anasafiri nje ya nchi,” alisema Mpangile.
Alisema katika mazungumzo na Baharia, alimweleza kuwa amewasiliana na baba wa kijana huyo ambaye anaishi Bagamoyo mkoani Pwani.

Mpangile alisema kwa mujibu wa Baharia, baba wa kijana huyo anayejulikana kwa jina la Akida, amesikia habari za mtoto wake na kwamba atakwenda kuripoti kituo cha polisi.

Naye mama mdogo wa Adamu, aliyetambulika kwa jina la Khadija Katundu, alikiri maofisa wa polisi kumuhoji mume wake.

Alisema wameendelea kutoa ushirikiano kwa watu wanaofika nyumbani kuhoji kuhusu suala hilo, na kwamba wanaamini ufumbuzi utapatikana.

Serikali yahaha

Baada ya taarifa hizo kuripotiwa na gazeti hili jana, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Polisi wanafanya mawasiliano na Serikali ya Pakistan ili kuangalia namna ya kumwokoa Adamu katika mikono ya maharamia hao.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Msemaji wa Polisi, Advera Bulimba, alisema tayari wamepata taarifa dhidi ya Mtanzania huyo.
“Kwa sasa tunafanya mawasiliano na wenzetu wa Pakistan tuone namna ya kumtoa kijana huyo katika mikono ya hao watekaji, na tukikamilisha hilo tutatoa taarifa rasmi juu ya jambo hili,” alisema Advera.
Wakati hayo yakiendelea, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, kupitia mmoja wa maofisa wa idara ya habari ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini, alisema wamepata taarifa ya tukio hilo, na sasa wanafanya mawasiliano na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

---------------------------------
UPDATE - Julai 22, 2016

KIJANA Juma Neti anayedaiwa kumweka rehani mdogo wake, Adamu Akida, kwa maharamia wa dawa za kulevya nchini Pakistan, ametoroka nchini na kukimbilia Afrika Kusini.

Taarifa za uhakika ambazo MTANZANIA inazo kutoka kwa mtu wa karibu wa Neti, zimeeleza kuwa alitoroka usiku wa Julai 19 mwaka huu kwa kutumia gari binafsi hadi Kenya ambako alipanda ndege kwenda Afrika Kusini.

Neti anadaiwa alitoroka nchini ikiwa ni siku moja kabla ya polisi na vyombo vingine vya usalama kuvamia nyumbani kwake Kunduchi Ununio wilayani Kinondoni Dar es Salaam juzi, kwa ajili ya kutaka kumkamata.

Chanzo hicho kilisema polsi waliambulia patupu kwa vile tayari Neti alikuwa ameondoka siku moja kabla.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, kabla ya kutoroka, Neti alionekana akiwa na mshirika wake wa biashara (jina linahifadhiwa kwa sasa) ambaye humtambulisha kuwa ni ofisa masoko wa moja ya kampuni zake za ndani na nje ya Tanzania.

Inadaiwa pia kuwa mshirika huyo ndiye msambazaji hodari wa madawa ya kulevya katika Ukanda wa Afrika Mashariki.

Taarifa zinasema kwamba watu hao kwa pamoja waliweza kutoroka kwa kutumia gari ndogo kupitia mipaka isiyo rasmi kati ya Namanga na Horohoro na kuingia Kenya.

Baadaye waliingia Nairobi kwa kutumia gari tofauti na walilotoka nalo Tanzania. Jijini Nairobi walipanda ndege kupitia Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta.

Mtoa taarifa huyo alieleza kuwa haikuweza kufahamika haraka ni ndege gani waliitumia kutoka Nairobi hadi Afrika Kusini.

Neti anadaiwa kumweka rehani Akida ambaye ni mtoto wa mama yake mdogo, nchini Pakistani, kwa gharama ya Dola za Marekani 700,000 (zaidi ya Sh bilioni 1.5) baada ya kuchukua madawa ya kulevya kutoka kwa maharamia wanaomshikilia Mtanzania huyo.

Taarifa zinaeleza kuwa polisi wamekuwa wakimtafuta Neti kwa mda mrefu bila mafanikio kwa tabia yake hiyo ya kujihusisha na biashara hiyo haramu.

Inaelezwa kwamba Neti amekuwa na utajiri wa kutisha ghafla na amekuwa miongoni mwa Watanzania wenye ukwasi mkubwa tofauti na miaka michache iliyopita ambako alikuwa mtu wa kipato cha kawaida.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, hivi karibuni Neti aliingia ubia na kampuni moja ya nchini China (jina halijafahamika) baada ya kuwekeza Dola za Marekani 400,000 (zaidi ya Sh milioni 800).

Katika mlolongo huo wa matukio kuna taarifa za kuwapo mtandao mkubwa unaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya ambao huwapeleka vijana katika nchi zinazotengeneza dawa hizo na kuwaweka rehani.

Kwa mujibu wa mtandao huo, vijana wengi hupoteza maisha kwa kuuawa na maharamia hao wakuu wa biashara hiyo ya ‘unga’ baada ya waliowaweka rehani kushindwa kupeleka fedha.