Maana ya Parole, Madhumuni na Sheria za Bodi

Na; Lucas Mboje – Jeshi la Magereza,

PAROLE ni utaratibu wa kisheria unaompa fursa mfungwa aliyehukumiwa kutumikia kifungo Gerezani cha miaka minne na kuendelea kutumikia sehemu ya kifungo chake katika jamii kwa masharti maalum baada ya kukidhi vigezo vifuatavyo:-

i). Awe ametumikia theluthi (1/3) ya kifungo chake na kuonesha mwenendo wa kurekebika kurudi katika jamii kumalizia sehemu ya kifungo chake kwa masharti maalum. Masharti hayo ni kuwa chini ya uangalizi maalum kuhakikisha kuwa hatendi kosa lolote mpaka atakapomaliza kifungo chake, kuzingatia masharti ya Parole anayopewa kikamilifu pamoja na kuwa raia mwema na kuishi kwa kujipatia kipato halali katika jamii;

ii). Awe ameonesha kujutia kosa, kurekebika tabia na kuonesha mwenendo mzuri gerezani na;
iii). Mamlaka husika kujiridhisha kuwa hatahatarisha usalama wa jamii.

Parole ni moja kati ya adhabu mbadala na imeonesha mafanikio makubwa katika nchi nyingi duniani. Utaratibu huu ni wa kipekee kwa kuwa unawagusa wafungwa wa vifungo virefu ambao ndio wengi waliopo magerezani. Aidha, ni utaratibu unaoshirikisha jamii katika urekebishaji kwa kuzingatia usalama wa jamii na dhana kwamba uhalifu ni zao katika jamii.

Madhumuni ya kuanzishwa kwa utaratibu wa Parole nchini hayatofautiani na madhumuni ya kuanzishwa kwa utaratibu huu kwenye nchi nyingine Duniani zikiwepo nchi za Afrika kama vile: Afrika kusini, Zambia na Namibia. Mfumo wa Parole ulioainishwa hapa nchini unatokana na uzoefu wa Parole unaotumika nchini Canada. Sababu zilizopelekea kuanzishwa kwa Parole hapa Nchini ni:-
i. Kuhusisha jamii katika suala zima la urekebishaji wa wafungwa badala ya kutegemea serikali peke yake kwani chanzo cha uhalifu ni mazingira yanayotokana na jamii yenyewe.

ii. Kuwepo na kuendelea kuongezeka kwa idadi ya wafungwa wenye vifungo virefu magerezani ambao kutokana na urefu wa vifungo vyao hawawezi kufaidika na programu zilizopo za urekebishaji kwa sababu ama watatoka magerezani wakiwa wazee wasiojiweza, watakutana na mabadiliko makubwa kijamii, kiuchumi na kisera wasiyoweza kuyamudu haraka/ipasavyo kwenda na wakati au watafia gerezani.

Wafungwa wa aina hii hukata tamaa kwani hawaoni sababu ya kuwa na nidhamu wawapo gerezani, hivyo kusababisha usalama magerezani kuwa mashakani. Parole ilikusudiwa kuwarejeshea matumaini ya kurejea katika jamii na kuishi maisha ya kawaida na kupunguza tishio la kiusalama magerezani na katika jamii kwa ujumla.

Jeshi la Magereza kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi liliwasilisha mapendekezo ya kutungwa Sheria ya Bodi za Parole nchini. Mapendekezo hayo yalijenga hoja ambayo hatimaye iliwasilishwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Novemba, 1994 na kupitishwa rasmi kuwa Sheria ya Bodi za Parole Na. 25/1994.

Sambamba na kutungwa kwa Sheria hiyo, kanuni za Bodi za Parole ziliandaliwa na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali tarehe 29 Agosti, 1997 (GN. 563/1997) hivyo kuwezesha Sheria hiyo kuanza kutumika rasmi. Hata hivyo Sheria iliyopitishwa haikuzingatia mapendekezo yaliyotolewa na Jeshi la Magereza ambayo yaliwalenga wafungwa wote kunufaika na Parole bila kujali aina na uzito wa makosa. Aidha, Sheria husika haikuanza kutumika mara moja kutokana na sababu zifuatazo:-

i. Bodi ya Taifa ya Parole na Bodi za Parole za Mikoa zilizokuwa zimeundwa kwa mara ya kwanza zilivunjwa na kuundwa upya na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kulalamikiwa kuwa uteuzi wa Wajumbe wake haukuzingatia uwiano wa jinsia na dini.

ii. Kutokamilika kwa maandalizi ya nyaraka mbalimbali muhimu katika utekelezaji wa mpango wa Parole ikiwa ni pamoja na uendeshaji wa semina kwa wajumbe wa Bodi za Parole za Mikoa yote nchini ili kufanikisha uanzishwaji na utekelezaji wa Sheria hiyo.

Baada ya matukio hayo, kikao cha kwanza cha Bodi ya Taifa ya Parole kilifanyika tarehe 19 Agosti, 1999 ambacho kiliwajadili wafungwa watano (5) na kupitisha watatu(3) walioonekana kutimiza masharti ya kuachiliwa kwa Parole nchi nzima. Idadi hiyo ni ndogo hasa ikizingatiwa kwamba wakati huo magereza yote nchini yalikadiriwa kuwa na wafungwa 27,000. Kutokana na Wafungwa hao watano waliojadiliwa, ilidhihirisha kuwa Sheria yenyewe ilikuwa haitekelezeki kama ilivyokusudiwa katika mapendekezo yaliyowasilishwa na Jeshi la Magereza hapo awali.

Matokeo haya yalisababisha Bodi ya Taifa ya Parole kuishauri Serikali kupanua wigo wa sheria hii ili wafungwa wengi zaidi waweze kunufaika. Mapendekezo haya yalilenga kifungu cha nne cha sheria ya Bodi za Parole vifungu vidogo (a),(b) na (c) ambavyo vinataja kuwa wafungwa wanaotumikia vifungo vya maisha, waliofungwa kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha, madawa ya kulevya, kujamiiana na adhabu ya kifo iliyobadilishwa kuwa kifungo kwamba hawawezi kupata msamaha wa Parole. Ilipendekezwa kwamba kifungu hicho kirekebishwe ili wafungwa wote wa makosa hayo nao wafikiriwe kunufaika na utaratibu wa Parole bila kujali makosa waliyotenda.

Kutokana na mapendekezo yaliyotolewa na Bodi ya Taifa ya Parole, Sheria Na. 25/1994 ilifanyiwa marekebisho kwa Sheria Na. 5/2002 ambayo ilijihusisha na eneo dogo tu kwamba badala ya mfungwa anayestahili Parole kuwa amehukumiwa kifungo cha miaka nane (8) na kuendelea, ilirekebishwa na kuwa awe amehukumiwa kifungo cha miaka minne (4) na kuendelea.

Chini ya marekebisho hayo Wakili wa Serikali Mfawidhi wa kanda aliongezezwa kuwa mjumbe wa Bodi ya Parole ya Mkoa. Hata hivyo suala la aina ya makosa na urefu wa kifungo katika kufikiriwa kunufaika kwa mpango wa Parole lilibaki kama lilivyokuwa hapo awali. Baada ya marekebisho hayo ya Sheria ya Bodi za Parole, Bodi za Parole za Taifa na Bodi za Mikoa zilizinduliwa upya mwaka 2003, na Bodi ya Taifa ya Parole ilifanya kikao chake cha kwanza mwezi Agosti, 2003 ambacho kilikuwa cha pili tangu Sheria hii ilipoanza kutumika rasmi nchini mwaka 1999.

Kwa mujibu wa Sheria na Sera za kitaifa kuhusu uboreshaji wa Magereza zinazotolewa kufuatia kuridhiwa kwa maazimio mbalimbali ya Kimataifa katika kuboresha hali za wafungwa magerezani, imeonekana kuwa vifungo siyo njia pekee ya kumrekebisha mhalifu. Adhabu mbadala zimeonekana ni bora zaidi kuliko kifungo kwa vile jamii huhusishwa katika suala zima la kumrekebisha mhalifu.

Adhabu mbadala zinazotumika hapa nchini ni pamoja na kulipishwa faini, Kuachiliwa kwa masharti, Probation, Kuachiliwa kwa matazamio, Kifungo cha Nje (EML), Parole, Huduma kwa Jamii n.k. Aidha, katika adhabu mbadala zilizoainishwa, Utaratibu wa Parole umeonekana unafaa zaidi kwa kuwa ndugu, uongozi wa mtaa/kijiji na mwathirika wa uhalifu hushirikishwa kutoa maoni kabla ya mfungwa husika kunufaika na mpango huu. Aidha, ni adhabu mbadala pekee inayohusika na wafungwa wanaotumikia vifungo virefu magerezani. Itaendelea …………wiki ijayo……!.

MWANDISHI WA MAKALA HII NI AFISA NGAZI YA JUU WA JESHI LA MAGEREZA, KWA MAONI NA USHAURI – 0754 871084, [email protected] or [email protected]


UPDATE - Mwendelezo...:

Na, Lucas Mboje – Jeshi la Magereza,

SIFA ZA MFUNGWA WA PAROLE

Sheria ya Bodi za Parole Sura 400 ya mwaka 2002 na Kanuni zake za mwaka 1997 inaainisha kuwa mfungwa anayetumikia kifungo cha kuanzia miaka minne (4) na kuendelea anastahili kunufaika na mpango wa Parole kama atakuwa na sifa zifuatazo:-

i) Asiwe amehukumiwa kifungo cha maisha;
ii) Asiwe ni mfungwa anayetumikia kifungo kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha, madawa ya kulevya na makosa yanayohusiana na kujamiiana;
iii) Asiwe ni mfungwa ambaye kifungo chake kimebatilishwa kutoka kwenye kifungo cha kunyongwa;
iv) Awe anatumikia kifungo kisichopungua miaka minne (4) au zaidi na awe ametumikia 1/3 ya kifungo chake;
v) Awe ameonesha tabia na mwenendo mzuri kwa muda wote aliokaa gerezani na;
vi) Asiwe na pingamizi la kimahakama la kukataliwa kunufaika na utaratibu wa Parole chini ya Kifungu cha 67 cha Sheria ya makosa ya Jinai.

UAMUZI WA BODI ZA PAROLE UNAVYOFANYIKA HAPA NCHINI


Kimsingi mfungwa anapoingia gerezani kwa mara ya kwanza hujulishwa kuhusu haki zake ikiwemo haki ya kuingizwa kwenye mpango wa Parole kama ana sifa kulingana na kosa lake na muda wa kifungo chake gerezani.

Mfungwa mwenye sifa ya kuingizwa kwenye mchakato wa Parole anapotimiza 1/3 ya kifungo chake, Afisa Parole hukusanya taarifa mbalimbali zinazomuwezesha kujadiliwa katika Bodi za Parole; Taarifa hizo ni maoni kutoka kwa wazazi/ndugu zake, maoni ya mwathirika wa uhalifu, nakala ya hukumu, hati ya kifungo, maoni kutoka uongozi wa kijiji anachotarajia kwenda kuishi na maoni/taarifa kutoka Kituo cha Polisi kilichomkamata na pia matokeo ya uchunguzi wa alama zake za vidole kuhusu kumbukumbu zake za uhalifu. Taarifa hizi zote huwa ni kwa ajili ya kudumisha usalama wa jamii na wa mfungwa mwenyewe anufaikapo kwa Parole.

Baada ya Taarifa hizi zote kukamilika kila mfungwa anayependekezwa kunufaika na Parole hufunguliwa jalada (Prison Form. 64) kwa ajili ya kutunza kumbukumbu zake pamoja na taarifa za tabia na mwenendo wa mfungwa. Mchakato wa kumjadili mfungwa huanzia katika Kamati za Urekebishaji ya Gereza. Kamati hiyo hupitia taarifa hizo na kutoa maoni na mapendekezo kwenda Bodi ya Parole ya Mkoa. Bodi ya Parole ya Mkoa hupitia maoni na mapendekezo hayo na baada ya uchambuzi wa kina, hutoa mapendekezo yake kwa Bodi ya Taifa ya Parole kupitia kwa Sekretarieti ya Bodi ya Taifa ya Parole.

Sekretarieti ya Taifa ya Parole ina jukumu la kuratibu shughuli zote za Bodi. Hivyo hupokea taarifa za wafungwa waliopendekezwa au kutopendekezwa kunufaika na Parole kutoka katika Bodi za mikoa. Huchambua taarifa hizo na kuandaa taarifa ya kila mfungwa kwa ajili kujadiliwa na Bodi ya Taifa ya Parole.

Bodi hiyo kwa kutumia taaluma mbalimbali walizonazo wajumbe wake na nyadhifa zao hufanya uchambuzi wa kina wa mawasilisho hayo na kutoa uamuzi wa mfungwa anufaike au asinufaike na Parole. Uamuzi wa Bodi ya Taifa ya Parole huwasilishwa kwa Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwa uamuzi wa mwisho kwa mujibu wa Kifungu cha 6(4) cha Sheria ya Bodi za Parole Na. 25 ya mwaka 1994 (Sura ya 400 R. E 2002).

Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi hupitia taarifa za kila mfungwa na kutoa uamuzi wa mwisho wa kukubaliwa au kukataliwa kunufaika kwa mpango wa parole. Uamuzi huo huwasilishwa kwa Katibu wa Bodi ya Taifa ya Parole ambaye ni Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Tanzania. Itaendelea…… !.

MWANDISHI WA MAKALA HII NI AFISA NGAZI YA JUU WA JESHI LA MAGEREZA, KWA MAONI NA USHAURI – 0754 871084, [email protected] or [email protected]