Mahojiano na Dk Mponda kuhusu mgomo wa madaktari: Sijakosea popote nikiwa Waziri wa Afya

Rais Magufuli na Dk Mponda
Sehemu ifuatayo ni ya mahojiano ya baina ya gazeti la MTANZANIA na aliyekuwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda (bado ni Mbunge wa Malinyi (CCM)) baada ya kukumbana na mgomo wa madaktari uliodumu kwa awamu mbalimbali zaidi ya miezi mitatu ukimtaka yeye na Naibu wake, Dk. Lucy Nkya kujiuzulu, ambapo Rais Jakaya Kikwete aliridhia na nafasi zao kuchukuliwa na Dk.Husein Mwinyi na Dk. Seif Rashid.

Tangu alipojiuzulu nafasi hiyo, Dk Mponda hajapata kuzungumzia mgomo huo wa madktari uliosababisha akapoteza nafasi hiyo hadi mwaka huu na ifuatayo ni sehemu kama ilivyonukuliwa kutoka kwenye chapisho lenye mahojiano kwa kina...

MTANZANIA: Ulipata kuwa Waziri wa Afya, unadhani ulikosea wapi mpaka ukang’olewa katika nafasi hiyo?
MPONDA: Hapana sijakosea mahali popote wakati nikiwa Waziri wa Afya ilikuwa katika kutekeleza majukumu yangu ya uwaziri.
Aidha, sijang’olewa kwa nafasi hiyo bali mimi mwenyewe ndiye nilimwomba aliyeniteua nijiuzulu katika nafasi hiyo baada ya mwendelezo wa mgomo wa madaktari mwaka 2012. Rais alitekeleza ombi langu baadaye katika mabadiliko aliyofanya katika baraza lake la Mawaziri.
MTANZANIA: Ni kweli kwamba ulishindwa kutatua kero za madaktari mpaka ikasababisha ukapoteza uwaziri?
MPONDA: Kwanza naomba niseme wazi kwamba si kweli kuwa nilishindwa kutatua kero za madaktari na ndio ikawa sababu ya kupoteza uwaziri. Kero za madaktari ni za muda mrefu ni mwendelezo wa madai ya muda mrefu kama utakumbuka tangu ule mgomo wa mwaka 2005.
Maelezo ya kina kuhusu suala la kuondoka kwangu katika nafasi ya uwaziri yalishatolewa na Rais Jakaya Kikwete wakati alipofanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri Mei mwaka 2012.
Sioni sababu ya kurudia aliyosema kiongozi wangu. Lakini kwa Kifupi kwa mazingira yale ya mgomo wa madaktari ilipaswa busara zitumike kwa faida ya Watanzania.
MTANZANIA: Pengine unadhani ulionewa au nini kilikuwa kikwazo kikubwa mpaka ikafikia hali ile?
MPONDA: Nafikiri haikuwa sahihi sana kwa madaktari katika mgomo wao kuweka sharti kwamba Waziri na Naibu wajiuzulu kwa kuwa sisi hatukuwa chanzo cha kutotimizwa kwa madai yao.
Haya ndio yalikuwa madai ya Madaktari mwaka 2012
(a) Posho ya Kulala Kazini (on Call Allowance)
(b) Posho ya Kufanya Kazi katika Mazingira Hatarishi (Risk Allowance)
(c) Posho ya Nyumba
(d) Posho ya Kufanya Kazi katika Mazingira Magumu (Hardship Allowance)
(e) Kupatiwa posho ya usafiri
(f) Nyongeza ya Mshahara.Wanadai mshahara wa Sh 700,000 kwa Daktari anayeanza kazi ni mdogo sana, hivyo wanapendekeza Daktari anayeanza kazi alipwe Sh. 3,500,000 kwa mwezi.
(g) Kupatiwa Bima ya Afya
Inapendkezwa Madaktari pamoja na familia zao wapewe kadi za kijani za Bima ya Afya.
(h) Kutaka wenzao warudishwe Muhimbili. Dai hili linahusu Madaktari waliokuwa katika mafunzo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na baadaye kurudishwa wizarani, warejeshwe Muhimbili bila masharti yoyote.
(iI) Kutaka Waziri, Naibu Waziri, Katibu mkuu na Mganga Mkuu wa Serikali wajiuzulu
MTANZANIA: Ulikuwa unajisikiaje pale madaktari walipokutaka wewe na Naibu wako kujiuzulu lakini hamkufanya hivyo mpaka pale mlipong’olewa?
MPONDA: Nilijisikia kawaida tu kwa kuwa kila kitu kina mwanzo na mwisho wake. Aidha, ninamshukuru Mungu kwa kuniwezesha kumaliza kazi yangu ya uwaziri kwa ufanisi na ubunifu katika changamoto, mfano uboreshaji wa mfumo wa usambazaji dawa, uhaba wa watumishi nakadhalika.
Lakini pia kuondoka kwangu nafasi hii imenipa nafasi zaidi ya kuwatumikia wananchi niliowekeana nao mkataba kwa kupitia kura zao kwa kuwawakilisha bungeni katika utatuzi wa kero zao.
Vinginevyo ningekuwa na wakati mgumu kurudi tena bungeni awamu ya pili. Tumeshuhudia mawaziri wengi wameanguka au kupata wakati mgumu katika chaguzi zilizopita. Kuna changamoto kubwa kuwatumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja.