Mbwa akimnusuru kifo mtu aliyeshambuliwa na chui huko Bunda

MTU mmoja, Makang’ha Mandazi (32), amenusurika kuuawa na chui aliyetoka katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kuvamia makazi ya watu katika kijiji cha Kihumbu, kata ya Hunyari, wilaya ya Bunda, mkoani Mara.

Mandazi mkazi wa kijiji hicho, alinusurika kifo baada ya mnyama huyo kumvamia nyumbani kwake juzi saa 4:00 asubuhi na kuanza kushambuliwa huku akiwa ameangushwa chini, lakini akaokolewa na mbwa wake aliyemng’ata mkia mnyama huyo hatari.

Akizungumzia tukio hilo lililovuta hisia za watu wengi kijijini hapo, Diwani wa Kata ya Hunyari, Magina Josephat, alisema lilitokea katika kijiji cha Kihumbu.
“Alinusurika kifo baada ya kuokolewa na mbwa wake aliyemng’ata mkia mnyama huyo, hali ambayo ilipelekea kumwachia na kuanza kushambuliana wanyama wenyewe na kutoa nafasi kwa majeruhi huyo kukimbia kuokoa maisha yake,” alisema.
Alisema wakati chui huyo kupambana na mbwa, wananchi walifika katika eneo la tukio na kuanza kumshambulia na kufanikiwa kumuua.

Josephat alisema Mandazi amejeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake na amelazwa hospitalini kwa matibabu.

Diwani huyo alisema wanyama wakiwamo tembo wamekuwa wakitoka mara kwa mara katika hifadhi hiyo na kuleta mdhara kwa wananchi, pamoja kushambulia mazao ya wakulima mashambani mifugo yao.

Kufuatia hali hiyo aliiomba serikali kuwadhibiti wanyama hao na kuwasihi askari wa wanyamapori wanapopewa taarifa juu ya wanyama hao wawe wanawahi mapema kufika katika eneo la tukio ili kuokoa masiaha ya watu na mazao yao.

Ofisa Wanyamapori katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Marwa Kitende, alisema baada ya kupata taarifa hiyo walifika mapema katika eneo la tukio na kutoa mwongozo juu ya ulipaji fidia kwa mwananchi aliyejeruhiwa.

Alisema tayari wataalamu wanafanya uchunguzi wa kina kama mnyama huyo alikuwa na kichaa au la na kwamba ngozi yake kwa sababu ni nyara ya serikali imehifadhiwa sehemu maalumu na kuongeza kuwa wamekuwa wakifanya doria za mara kwa mara kwa ajili ya kudhibiti wanyama hao wanaotoka hifadhini.
  • NIPASHE