Mkuu wa Wilaya azuia mikutano ya kisiasa wilayani kwakeMKUU wa Wilaya Iringa, Richard Kasesela amesema kamati yake ya ulinzi na usalama haitaruhusu mikutano ya hadhara itakayoombwa na vyama vya siasa wilayani humo ili kuipa serikali na wananchi nafasi ya kujiletea maendeleo baada ya kumaliza salama Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Pamoja na uamuzi huo, Kasesela amesema kamati hiyo itawasaka na kuwafikisha katika vyombo vya dola watu wanaomkashifu Rais Dk John Magufuli na viongozi wengine wa serikali, siasa na dini kwa namna yoyote ile.

“Tuendelee na majukwa ya utendaji, majukwaa ya mipasho ya siasa tupumzike ili tuiache serikali ifanye kazi zake,” alisema baada ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza kuwaapisha wakuu wa wilaya za mkoa wa Iringa mapema jana.

Kasesela alisema uchaguzi wa 2015 ulimalizika salama kwa kumpata rais, wabunge na madiwani na kwamba kazi inayofanywa na Rais kwasasa ni kumalizia kuunda serikali yake.

“Kama tunataka mbwembwe za siasa majukwani aidha tusubiri uchaguzi wa serikali za mitaa au Uchaguzi Mkuu wa 2020,” alisema huku akivitangazia vyama vya siasa ruksa ya kufanya mikutano yao ya ndani akiahidi hawataiingilia kama itafanyika kwa amani.

Wakati huo huo, Kasesela amewataka viongozi wa taasisi mbalimbali za dini ambazo hakuzitaja kumaliza migogoro yao ya uongozi aliyosema inaelekea kuhatarisha amani ya wilaya. [via Frank Leonard bog]