Mpango maalum kupima na kurasimisha ardhi kwenye maeneo yasiyopimwa Dar kuanza

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Mozes Kusiluka
Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeandaa mpango maalumu wa upimaji wa Ardhi na Urasimishaji wa maeneo yote yasiyopimwa katika jiji la Dar es Salaam ambapo viwanja zaidi ya laki tatu (300,000) vitapimwa na wamiliki wake kupewa Hati.

Akizungumza leo jijini Dar es salaam kuhusu zoezi hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Mozes Kusiluka amesema kuwa Serikali imeamua kuja na mpango huo kwa sababu ya ukubwa wa jiji hilo na wingi wa watu ulioambatana na ujenzi wa makazi holela.
“Katika mwaka wa fedha 2016/2017 tumepanga kuwa na mpango maalum wa jiji la Dar es salaam ambapo wataalam wetu watakwenda, kuhakiki mipaka na kupima maeneo yote ambayo hayajapimwa na kutengeneza ramani zitakazoonyesha maeneo ya barabara na maeneo ya huduma nyingine kwa kushirikiana na wananchi husika.
Amesema kuwa baada ya zoezi la uhakiki Serikali itatoa hati za maeneo hayo na kusisitiza kuwa zoezi hilo litafanyika pia katika maeneo mengine ya miji mikubwa nchini yenye watu wengi ikiwemo jiji la Mwanza.

Dkt. Kusiluka amesisitiza kuwa urasimishaji utakuwa shirikishi kwa kuwahusisha watu wote wa maeneo yatakayopimwa na Serikali ambapo wananchi wenye nyumba watashirikiana na viongozi wa Serikali katika mitaa kupanga na kuimarisha mindombinu ya maeneo yao pamoja na kukubaliana maeneo ambayo barabara za mitaa zitapita, mitaro ya maji machafu, magari ya kupitishia huduma za dharula kama Zimamoto nay ale ya kubebea wagonjwa.
“Mpango wa urasimishaji ni Shirikishi, wataalam wa ardhi watakwenda kwenye maeneo yote yatakayopimwa hususan katika jiji la Dar es salaam na kukaa na wananchi wote,kupitia mipaka wakishirikiana na wananchi wote kwa uwazi ili zoezi hilo liwe na manufaa na tija kwa wananchi wote” Amesisitiza Dkt. Kusiluka. 
Amesema kuwa licha ya kuwepo kwa sheria zinazoisimamia sekta ya Ardhi nchini Tanzania bado sekta hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo migogoro ya Wakulima na wafugaji, migogoro ya kijinai ya mtu mm kuvunja nyumba au kuvamia eneo la mtu bila idhini, migogoro ya mipaka kati ya majirani na ile inayosababishwa na wananchi kutokujua sheria.

Mbali na sababu hizo amebainisha kuwa idadi ya watu na matumizi ya ardhi kwa shughuli mbalimbali imekuwa ikiongezeka wakati ardhi ikibakia ileile jambo linaloifanya sekta hiyo kuja na mikakati mbalimbali ya kukabiliana na changamoto hizo kupitia watalaam waliopo.

Amesema kuwa serikali imefanya mambo mbalimbali kuhakikisha kuwa inatatua kero za wakulima na wafugaji katika maeneo mbalimbali kwa kuwatumia wataalam wake kupima na kupanga maeneo ya vijiji mbalimbali, kutoa elimu pia kuajiri wataalam wa masuala ya Ardhi katika Halmashauri zote nchini.

Aidha amesisitiza kuwa Serikali imejipanga kupima maeneo yote ya ardhi nchini ambayo hayajapimwa kupitia mpango wa miaka 10.
  • Aron Msigwa –MAELEZO.